NSSF YAPONGEZWA KWA MATUMIZI YA TEHAMA DARAJA LA NYERERE
Na MWANDISHI WETU
Mifumo ya TEHAMA iliyofungwa katika mradi wa Daraja la Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam, imewagusa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) ambao wameonesha kufurahishwa na hatua iliyochukuliwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kufunga mifumo hiyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari tarehe 16 Novemba, 2023, wakati wa ziara ya wajumbe wa kamati hiyo katika Daraja la Nyerere, baadhi ya wajumbe hao akiwemo Mhe. George Malima (Mpwapwa CCM), amesema wanaipongeza NSSF kwa kufunga mifumo ya TEHAMA katika mradi huo wenye tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.
“Tuwapongeze NSSF kwa usimamizi nzuri wa daraja hili, tumeona kumewekwa mifumo mbalimbali ya TEHAMA na magari hayachukui muda mrefu yakifika taratibu zinafanyika haraka za kulipia na kuondoka,” amesema.
Mhe. Malima amesema mradi huo unaendana na kiwango cha fedha kilichotumika na umechangia maendeleo ya wananchi hususan wakazi wa Wilaya ya Kigamboni na watumiaji wengine kwa ujumla.
Naye, Dkt. Oscar Kikoyo (Mulemba Kusini- CCM) amewaomba wananchi wa Kigamboni na watumiaji daraja hilo kutumia mifumo ya kidijitali iliyofungwa ikiwemo wa kulipa kwa bando ili kupunguza msongamano.
Kwa upande wake, Masha Mshomba, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF amesema Mfuko kwa kuutumia wataalamu wa ndani wa TEHAMA, umetengeneza mfumo wa makusanyo ya tozo ambao umeunganishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya utambuzi wa magari na mfumo wa kielektroniki wa malipo wa Serikali (GePG).
“Mfumo huu unatoa fursa kwa wateja kuchagua aina ya huduma waipendayo ikiwemo malipo ya vifurushi (bundle), malipo ya kabla na mfumo wa fedha taslimu,” amesema Mshomba.
Amesema NSSF itaendelea kufanya kazi kwa juhudi na kuhakikisha huduma katika daraja hilo zinazidi kuboreshwa siku hadi siku na kukidhi matarajio ya watanzania wote kwa ujumla.
Mshomba amesema Mfuko uko imara, endelevu na uwekezaji unaendelea kukua kwa kasi hasa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita jambo ambalo limechangiwa na uongozi wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa PIC, Mhe. Vuma Augustine amesema
mradi wa daraja hilo una tija kwa Taifa kwa sababu ni endelevu na imara na kwamba umejengwa kwa viwango vizuri na umeleta faida nyingi zikiwemo za kiuchumi na kijamii.
“Nichukuie nafasi hii kuipongeza Serikali kwa uamuzi nzuri wa kujenga daraja hili na pia niipongeze NSSF kwa maamuzi mazuri na ya kizalendo kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja, huu ni uamuzi mzuri kufadhili mradi ambao una tija kubwa kwa jamii na Taifa,” amesema Mhe. Augustine.
No comments