Breaking News

WATOTO WANAOZALIWA NA VVU WAONGEZEKA BUCHOSA,SERIKALI YA WILAYA YAOMBA MUDA KUCHUNGUZA JAMBO HILO

 Na Tonny Alphonce,Mwanza

Serikali ya wilaya ya Buchosa mkoani Mwanza imeomba kufatilia taarifa ya kuongezeka kwa idadi ya Watoto wanaozaliwa na VVU iliyotolewa katika kikao cha baraza la madiwani lililoketi wilayani humo  ili kujua sababu za kuongezeka kwa maambukizi hayo.


Katika taarifa ya Kamati ya UKIMWI ya Baraza hilo ilionyesha  watoto 86 wamekutwa na VVU huku Watoto 14 wakiendelea kupatiwa dawa ya kufubaza virusi vya UKIMWI.

Akichangia ripoti hiyo diwani wa viti maalumu kata ya Nyahunge,Grace Erenest amesema idadi hiyo ni kubwa na haikubaliki kwa kuwa Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa kina mama wajawazito na wataalamu wa afya namna ya kuzuia maambukizi kutoa kwa mama kwenda kwa mtoto.

Diwani wa viti maalumu kata ya Nyahunge,Grace Erenest akielezea mstuko wake baada ya kupokea taarifa ya idadi ya watoto wanazaliwa VVU kuongezeka.

'Taarifa hii inashangaza sana inawezekana vipi mtoto azaliwa na maambukizi ya VVU wakati idadi kubwa ya kina mama kwa sasa wanajifungua kupitia vituo vya afya,nahisi kuna shida kwa wataalamu wetu wa afya’.alisema Grace.

Diwani Grace amesema kwa namna Serikali ilivyowekeza katika sekta ya afya ni aibu kusikia ongezeko la Watoto wanaozaliwa wakiwa na maambukizi ya VVU kwa kuwa vifaa na mazingira mazuri ya mama mjamzito kujifungua salama yapo.

Akitoa ufafanuzi juu ya taarifa hiyo DMO wa Buchosa Irene Mkerebe ameliomba baraza la madiwani kumpa muda wa kufatilia suala hilo la kuongezeka kwa idadi ya Watoto wanaozaliwa na VVU katika halmashauri ya Buchosa ili kupata ukweli kuhusu taarifa hiyo.

DMO wa Buchosa Irene Mkerebe akitoa ufafanuzi kuhusu idadi ya watoto wanaozaliwa na VVU kuongezeka.

Irene amesema anachojua ni kuwa idadi hiyo ya watoto 86 ni wale Watoto ambao wamezaliwa na kina mama wenyewe VVU na wamekuwa wakipatiwa dawa ili kuwakinga Watoto hao wasiweze kupata maambukizi kutoka kwa mama.

‘Ukiangalia Watoto hawa huwa tunaendelea kuwapatia dawa katika kipindi chote hata wakati ananyonya ili kuendelea kumkinga asije kupata maambukizi kwa maana hiyo niwatoe hofu waheshimiwa madiwani ukiona mtoto anapatiwa dawa mara baada ya kuzaliwa sio kwamba tayari kaambukizwa bali tunamkinga asipate maambukizi’.alisema Irene.

Akizungumzia vituo vya tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU Irene amesema hadi sasa kuna vituo 18 ambavyo vimekidhi vigezo vya kuwahudumia watu wanaoishi na VVU.

Tanzania ina Watoto na watu wazima milioni 1.7 wanaoishi na VVU na mnamo 2019 kulikuwa na maambukizi mapya  ya VVU 77,000 nchini.

Kwa mujibu wa utafiti wa kitaifa wa athari ya VVU wa mwaka 2018 idadi ya wanawake wote waliohudhuria kliniki ya wajawazito  saw ana asilimia 98 .9 kati yao asilimia 92.4 walishauriwa juu ya hali yao ya maambukizi ya VVU.

Makadirio yanaonyesha kuwa maambukizi ya VVU kutoka kwa mama na mtoto  yamepungua hadi asilimia 8 mwaka 2015 na kuongezeka hadi kufikia asilimia 11 mnamo mwaka 2020 kulingana na makadirio ya UNAIDS dhidi ya malengo ya ulimwengu ya asilimia 5.

No comments