Breaking News

MASOKO YA MADINI YAINGIZA SHILINGI BILIONI 76.2 NDANI YA MIEZI 6


Na Mwandishi wetu

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba 2020 masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini yaliingizia Serikali kiasi cha shilingi bilioni 76.2.


Aliyabainisha hayo jana katika kikao kazi cha Tume ya Madini kilichofanyika jijini Dodoma chenye lengo la kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Madini kwa kipindi cha robo mwaka.


Alieleza kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Disemba, 2020 jumla ya mapato (mrabaha na ada ya ukaguzi) yaliyotokana na mauzo ya madini katika masoko ni shilingi bilioni 76.29 ambapo katika fedha hizo, kiasi cha shilingi bilioni 65.27 zilitokana na mrabaha na shilingi bilioni 11.02 zilitokana na ada ya ukaguzi.


Akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuhuli, Mhandisi Samamba amesema kuwa, katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Disemba, 2020 jumla ya makusanyo ya maduhuli yalikuwa ni shilingi bilioni 317.49 ikiwa ni sawa na asilimia 120.56 ya lengo la nusu mwaka na pia ni sawa na asilimia 60.28 ya lengo la makusanyo kwa mwaka 2020-2021.

 

“Ikumbukwe kuwa Tume ya Madini ilipangiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 526.7 kwa mwaka wa fedha 2020-2021,” alisema Mhandisi Samamba.


Kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula kilishirikisha makamishna ambao walikuwa ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mary Makondo, Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamhanga, Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA) Haroun Kinega, Profesa Abdulkarim Mruma, Dkt. Athanas Macheyeki, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Makao Makuu ya Tume ya Madini.


No comments