Breaking News

Makazi Eneo la Igogo Changamoto kwa Utunzaji wa Ziwa Victoria Mkoani Mwanza


 Edwin Soko
 Mwanza

Mkoa wa Mwanza umekuwa ni miongoni mwa Mikoa iliyopitiwa na Ziwa Victoria, ambapo makazi ya milimani ikiwemo eneo la Igogo, kata ya Igogo wilaya ya Nyamagana Mkoa wa Mwanza yamekuwa wakichangia uharibifu wa mazingira kwenye Ziwa Victoria.


Eneo la Igogo kijiografia limekaa mlimani na chini ya eneo hilo kuna Ziwa Victoria, wakazi wake wengi wanatumia vyoo visivyo imara kutokana na eneo hilo kuwa na mawe mengi na hivyo kuleta ugumu wakati wa kuchimba vyoo.

Baadhi ya wakazi wa eneo hilo uwa  na mashimo ya kuhifadhi vinyesi yaliyojengwa juu na kutokuwa imara, wakati wa mvua vyoo hivyo ufunguliwa na kumwaga kinyesi nje na kusukumwa na maji ya mvua kupelekwa katika Ziwa Victoria.

Makala hii imefanikiwa kuongea na Bwana Erasto John Mkazi wa Igogo ambaye alisema kuwa, kweli wakati wa mvua tunafungulia chemba za vinyesi ili kupunguza uchafu uliomo humo kwani tusipofanya hivyo chemba zitajaa mapema na hatuna uwezo wa kuchimba nyingine.

" Ndugu Mwandishi eneo hili sio rafiki kwa kuchimba mashimo ya choo kwenda chini kwani kama unavyoona sehemu kubwa ni mawe hivyo kupata sehemu yenye udongo ni shida sana" aliongeza  John.

Naye Bibi Josephine Mugambo alisema kuwa, wanajua vitendo hivyo sio salama kwa afya ya binadamu na viumbe lakini hawana njia nyingine ya kufanya.

"Hatufanyi jambo hili kwa kupenda bali tumekosa njia mbadala ya kufanya, labda tuiombe Serikali itusaidie kupata vyoo mbadala vya maeneo kama haya ya Igogo" alisema Mugambo.

Sera na sheria ndogondogo za Halmashauri ya Jiji la Mwanza zinabidi zitazame wakazi wa maeneo ya milimani kama ilivyo igogo kwa kuwa changamoto ni nyingi za uhifadhi wa maji taka kwani pasipokuwa na mikakati mathubuti basi uhifadhi wa Ziwa Victoria utakuwa mashakani.
Ziwa Victoria ambalo ni chanzo cha mto Nile ni tegemezi kwa shughuli za kiuchumi kwa wakazi wa Mwanza,wapo wakazi wanaotegemea shughuli za uvuvi kuendesha maisha yao, pia wapo wanaotegemea shughuli za usafirishaji kuendesha shughuli zao, hivyo mikakati ya kulilinda ni muhimu sana.

Utunzaji wa Ziwa Victoria ni muhimu kwa kuwa wakazi wa Aftika ya Mashariki wanategemea sana Ziwa hilo kiuchumi na kihuduma pia Ziwa victoria ni chanzo cha mto Nile ambapo wakazi wengi wa Nchi kama Misri na Ethiopia wanategemea Ziwa hilo kwa uchumi.

No comments