Breaking News

RAIS SAMIA AHUTUBIA MKUTANO WA EITI, ATAKA UWEKEZAJI WENYE MANUFAA SEKTA YA MADINI

Dakar

Rais Samia Suluhu Hassan amehutubia kwa njia ya mtandao mkutano wa kimataifa wa Taasisi ya Uwazi na Uwajibikaji katika Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia (EITI) uliofanyika Jijini Dakar, Senegal.


Mkutano huo ulifanyika chini ya udhamini wa Rais Macky Sall wa Senegal, Bodi ya EITI na wadau wa sekta za uziduaji.


Katika hotuba yake fupi aliyowasilisha mbele ya washiriki zaidi ya 1,500 toka nchi zaidi ya 90; Rais Samia amesisitiza umuhimu wa wavunaji wa rasilimali za madini kuhakikisha kuwa uwekezaji wao unawanufaisha wananchi wanaoishi katika maeneo husika.


Amesisitiza umuhimu wa mataifa yenye rasilimali kuwa na uwazi kwenye uwekezaji na kuweka hadharani kumbukumbu za uzalishaji wao zinazoonyesha mchango stahiki wanaochangia jamii na pato la taifa. 


Kwa sasa nchi 57 duniani ni wanachama hai wa EITI, huku Tanzania ikiwa miongoni mwao kupitia taasisi yetu ya TEITI.


Ujumbe wa Tanzania uliowakilisha taifa letu kwenye Mkutano huo uliongozwa na Dkt. Steven Kiruswa, Naibu Waziri wa Madini.


Wajumbe sita walioambatana na Naibu waziri ni Dkt. Abdulrahaman Mwanga, Kamishna wa Madini, Mhe. Danstan Kitandula, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, pamoja na Mhe. Jesica Kishoa, Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. 


Wengine ni Bi Mariam Mgaya, Kaimu Mtendaji wa TEITI, Ndugu Ludovic Utouh, Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI na Ndugu Adam Anthony, Mjumbe wa Kamati ya TEITI.


Mkutano huu ambao ulifunguliwa na Waziri Mkuu wa Senegal kwa niaba ya Rais Macky Sall pia ulihudhuriwa na mawaziri wakuu toka nchi mbali mbali sambamba na waliohudhuria kwa njia ya mtandao akiwemo Tony Blair, Waziri Mkuu mstaafu wa Uingereza.


Katika mkutano huo, ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Dkt. Kiruswa uliwasilisha mada kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya madini nchini Tanzania.

No comments