MBUNGE LUCY MAYENGA ATOA MSAADA MIFUKO YA SARUJI UJENZI WA BWENI LA WASICHANA SHULE YA SEKONDARI NGOFILA
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Shinyanga Mhe. Lucy Thomas Mayenga(katikati aliyevaa kiremba) akikabidhi Mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari Ngofila
Na Mwandishi wetu - Kishapu
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Shinyanga Mhe. Lucy Thomas Mayenga amekabidhi Mifuko 100 ya saruji yenye thamani ya shilingi Milioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari Ngofila iliyopo katika kata ya Ngofila wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidi mifuko hiyo ya saruji iliyohudhuriwa pia na Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Shinyanga Grace Bizulu na katibu wa UWT mkoa Asha Kitandala,Julai 8,2023, Mbunge huyo maarufu kwa jina la 'Dada Mkubwa' amesema ametoa msaada huo ili kuitikia wito wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu wa kuhakikisha watoto wa kike wanapata mazingira mazuri ya kusoma ili kuepukana na changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mhe. Mayenga amesema shule hiyo yenye matokeo mazuri ya ufaulu haina budi kuwa na bweni kwa ajili ya watoto hao wa kike kwani kwa sasa baadhi yao wamekuwa wakipata ujauzito wakiwa masomoni hali inayosababisha jamii kupoteza wanawake ambao wangeweza kuwa msaada kwao endapo wangeendelea na masomo.
" Nilipokea mapendekezo kutoka kwa diwani wa Viti Maalum Mhe. Devotha Jilala kuwa bweni linatakiwa kujengwa hapa, na mimi nikasema kutokana na maendeleo yao lazima niwaunge mkono ndiyo maana leo nimekuja kukabidhi mifuko ya saruji ili kuchangia ujenzi wa bweni la wanafunzi",amesema Mhe. Mayenga.
Kwa upande wake Diwani wa Viti Maalum Mhe. Devotha Jilala amesema msaada huo utatumika kama ulivyotarajiwa ili kuhakikisha kuwa watoto wa kike wanakuwa salama watimize ndoto zao.
Aidha amemshukuru Mhe. Mayenga kwa kuwa mstari wa mbele pindi anapoombwa msaada wa masuala ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Shinyanga Mhe. Lucy Thomas Mayenga(katikati aliyevaa kiremba) akikabidhi Mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari Ngofila iliyopo katika kata ya Ngofila wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga.
No comments