Breaking News

"MNYONGE MNYONGENI HAKI YAKE MPENI, RAIS SAMIA AMEFANYA MAKUBWA HEKA - MANYONI" - MBUNGE DKT. CHAYA


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza Miradi mikubwa Katika Jimbo la Manyoni Mashariki.


Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa Vijiji vya Chikombo, Mizuchii, na Heka. Mbunge wa Manyoni Mashariki Mhe. Dkt. Pius Chaya mnamo Julai 18, 2023 ameishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali Jimboni humo.


Akieleza Miradi iliyofanyika ndani ya Miaka miwili tangu Rais Samia kuingia madarakani Mhe. Dkt Chaya amesema, zaidi ya Milioni 490 zimetolewa na Serikali ili kujenga Shule mpya ya Msingi ya Heka.
"Kwa wale mnaoenda Heka mmeshaona, tunajenga Shule mpya ya Msingi, haya ni mafanikio makubwa haijawahi kutokea, Heka hawakutegemea wangejengewa Shule mpya ya Msingi",amesema Dkt. Chaya.

Pia, amesema Bilioni Nne(4) zimetolewa kwaajili ya kujenga Shule ya Wasichana Solya, ambapo watoto kutoka Chikombo, Heka, na Mazuchi wataenda kusoma.


"Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni, watoto wetu wale wa Kike watakaofaulu kutoka Chikombo watasoma pale, ni Shule ya Bweni, Mama Samia anataka atengeneze akina Mama Samia wengine baadae", amesema.

Aidha, katika Shule hiyo Wanafunzi hao watapata chakula bila Wazazi kutoa michango wala kuchangia chakula.


Katika nyanja hiyo ya Elimu Jimboni humo, Mhe. Dkt. Chaya amewaeleza wananchi kuwa Zaidi ya Bilioni 1.4 zimetolewa kwaajili ya Ujenzi wa Chuo cha Veta Manyoni.


"Ninyi wenyewe ni mashahidi, Vijana wengi wanamaliza Kidato cha Nne hawaendelei, tunataka hao waliomaliza Kidato cha Nne waende wakasome Ufundi pale Veta, hayo yote Makubwa ameyafanya Mama Samia, Mama Samia hoyeeee",amesema.

Mradi mwingine unaotekelezwa katika Kata hiyo ya Heka ni Ujenzi wa Jengo la Kujifungulia akinamama wajawazito unaoambatana na Vyoo ambao unaogharimu Takribani Milioni 93.

Akiwaeleza Wananchi wa Chikombo kuhusu Barabara ya kwenda Mkondowa ambayo ilikuwa ni kilio cha muda mrefu, amesema kama alivyowaahidi Wananchi hao kuwa atatekeleza ndivyo ambavyo imekuwa ambapo kwa sasa Wamekamilisha Kilometa Tatu kwa kiwango cha Juu, na wanakwenda kumalizia Kilometa Nne.

Ameahidi kuwa ndani ya Mwaka huu wa 2023 watakwenda kuanzisha Ujenzi wa Shule ya Msingi Mkondowa ambapo atatoa Milioni Tano za mfuko wa Jimbo kwaajili ya kuanzisha Ujenzi huo.

Amesema lengo ni kuwaokoa watoto wasitembee umbali mrefu kwenda kupata Elimu.

Katika nyanja ya Michezo, Mbunge huyo ametoa Vifaa vya Michezo ambavyo ni Jezi na Mipira kwaajili ya Timu za Mpira wa Miguu Jimboni humo ambapo katika hilo Kila Kijiji Timu zake zinapata Vifaa hivyo.

Kwa Upande wake Mhe. Diwani wa Kata ya Heka, Haruna Chimanga amesema walipoingia madarakani Mwaka 2020 kulikuwa na changamoto ikiwemo za Madarasa lakini kwa sasa zimeshatatuliwa.


Nao baadhi ya Wananchi wamemshukuru Rais Samia na Mbunge kwa kuwajali na kupeleka maendeleo katika Kata yao, huku wakimpongeza Rais kwa Kazi kubwa anayoendelea kuifanya.

Ziara ya Mbunge Mhe. Chaya inaendelea katika Kata zote 19 za Jimbo la Manyoni Mashariki kwa kufanya Mikutano ya hadhara, kusikiliza, kutatua kero za wananchi.

No comments