Breaking News

MTWARA BADO INAKABILIWA NA CHANGAMOTO YA VIFO VYA WATOTO WACHANGA

 

Na Gregory Millanzi,Mtwara

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abasi amesema changamoto inayowakabili watoto kwa mkoa huu ni kuendelea kuwepo kwa vifo vingi vya watoto wachanga, na kwa mujibu wa taarifa za MTUHA kuanzia julai, 2022 hadi Juni 2023, jumla ya watoto waliozaliwa ni 44,253 kati yao vifo 557 vilivotokea na kuripotiwa  sawa na asilimia 1.2.

Kanali Abasia amesema hayo wakati akizungumza na wadau wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya wali ya Mtoto ambapo ametaja kuwa chanzo cha vifo vingi vya watoto wachanga ni uzazi pingamizi unaosababishwa na kuchelewa  kufika kwenye vituo vya huduma za afya.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abasi

Pia ameongeza kuwa sababu nyingine ni watoto kuzaliwa kabla ya wakati njiti, watoto kuzaliwa  na ulemavu wa viungo, mtoto kushindwa kupumua  mara baada ya kuzaliwa  na kina mama kuchelewa kuanza kliniki kwa wakati mara wanapopata ujauzito ambapo hupelekea  kushindwa kuzibaini dalili za hatari na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abasi amesema kuwa takwimu hizi zinaashiria kuwa bado kuna changamoto kubwa katika eneo hili, na amsesema sio ishara nzuri kwa nustakabali wa Taifa endelevu kama inavytarajiwa .

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa Kanali Ahmed Abasi ametoa wito kwa wadau na jamii kwa ujumla kuhakikisha hatua stahiki  na za makusudi zinachukuliwa katika kupambana na changamoto hii ili kunusuru vifo vya watoto wachanga.

Dkt Enjoy Nsolo Mlekani Daktari kitengo cha magonjwa ya wanawake na uzazi katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya kusini iliyopo Mkoani Mtwara amesema kuwa changamoto hiyo inaweza ikapungua au kama kila mama mjamzito atafuata  taratibu bora za kliniki na anahudhuria kliniki kwa wakati, maana kuna vifo ambavyo vinasababishwa na kukosa uangalizi wa awali wa mama mjamzito.

Ameongeza kuwa kuna vifo ambavyo ni mipango ya Mungu na kuna ambavyo vinatokana na sababu za kiafya kwa mfano mama mjamzito anaposhindwa kuhudhuria kliniki kwa wakati  anaweza akasababisha matatizo kwa mtoto bila yeye mwenyewe kujua na wengi wao wanapokuja kliniki nyakati za mwisho wakiwa wanakaribia kujifungua ndio yanapotokea matatizo ya vifo vya mtoto tumboni.

Dkt Enjoy Mlekani amewaasa jamii kuhakikisha wanahudhuria kliniki mara baada tu ya kuhisi ujauzito au kugundua amebeba mimba na afatilie ushauri wa watoa huduma ya afya ya mama na mtoto ili kumlinda mtoto akiwa tumboni na pia kuzuia vifo vya watoto wachanga.

Kwasasa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini iliyopo Mkoani Mtwara ina kliniki ya magonjwa ya wanawake na uzazi ambayo inafanyika kila jumatatu na Alhamis kuanzia saa moja na nusu asubuhi hadi saa tisa na nusu alasiri, huduma hii imeboreshwa sana na wananchi endapo wataitumia kwa ufasaha itapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya vifo vya watoto wachanga mkoani Mtwara.

Mwajuma Mussa ni mama wa watoto 5, amesema wanawake wengi wa sikuhizi hawapendi kwenda kwenye vituo vya afya wakiwa wajawazito, hali inayopelekea changamoto ya vifo vya watoto wachanga kuongezeka.

‘’Wanawake wengi sikuizi hawapendi kuhudhuria kliniki kwa wakati, hasa hawa mabinti, sijui wanaona fasheni kutokwenda zahanati?  Wanazulula tu mitaani mpaka mimba inafika miezi 8 au wengine wanakaribia kujifungua miezi 9 ndio wanaenda zahanati, na ndio maana kuna baadhi ya wauguzi wanawagomea mabinti kisa hawahudhurii kliniki kwa wakati’’ amesema Mwajuma Mussa mkazi wa Tandika Mtwara.

Kiwango cha vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa kipindi cha miaka 5 kabla ya Utafiti wa TDHS-MIS wa Mwaka 2022 ni vifo 43 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai. Kiwango cha vifo vya watoto wachanga kabla ya kutimiza mwaka mmoja ni vifo 33 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai. Kiwango cha vifo vya watoto wachanga kabla ya kutimiza mwezi mmoja ni vifo 24 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai. Hii inaonesha kwamba vifo vya watoto wachanga kabla ya kutimiza mwezi mmoja baada ya kuzaliwa vinachangia zaidi ya nusu ya vifo vyote vya watoto wachanga.


No comments