Breaking News

WAPELELEZI NA WAENDESHA MASHTAKA WA SERIKALI MKOA WA MARA WANOLEWA

  

Wapelelezi na Waendesha Mashtaka wa Serikali wa mkoa wa Mara wamekumbushwa kutumia weledi na kuzingatia taratibu za kisheria ili kuhakikisha mashauri ya dawa za kulevya yanamalizika katika hali ya kufanikiwa.

Hayo yameelezwa na Kamishna wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Bi. Veronica Matikila wakati akiwasilisha mada juu ya upelelezi na uendeshaji wa mashauri ya dawa za kulevya kwa kundi hilo yaliyofanyika leo tarehe 04 Oktoba, 2023 katika ukumbi wa bwalo la polisi mjini Musoma.

Mada zilizojadiliwa ni pamoja na aina za ushahidi, namna kuthibitisha makosa ya dawa za kulevya na maeneo muhimu ya kuzingatia kwa Waendesha Mashtaka katika kuongoza upelelezi wa kesi za dawa za kulevya.

Aidha, akizugumzia mafunzo hayo, Mkuu wa Mashtaka mkoa wa Mtwara Joseph Mauggo amesema mafunzo haya yanafanyika kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya Jinai kuhakikisha wanafanya mafunzo endelevu kwa Maafisa wanaopeleleza na wanaoendesha mashauri ya dawa za kulevya ili kukabiliana na changamoto za kiutendaji pamoja na kubadilishana uzoefu juu ya upelelezi na uendeshaji mashauri hayo.

"Mnamo mwezi Juni mwaka 2023 Mheshimwa Waziri Mkuu ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya alielekeza kuundwa kwa Tume ili kufanya tathmini ya mwenendo wa kesi za dawa za kulevya. Miongoni mwa mambo yaliyobainika na Tume hiyo ni kwamba, Serikali inapoteza kesi nyingi kwa sababu ya kutokuwa na uelewa wa pamoja kwa watendaji muhimu kwenye masuala ya dawa za kulevya" amesema Maugo.

Ameongeza kuwa, nia ni kujengeana uelewa wa pamoja, kutatua changamoto na malalamiko ya wananchi ili jamii ione na kutambua jitihada zinazofanyika kwenye na Serikali katika kulishughulikia tatizo la dawa za kulevya hapa nchini.

Mafunzo haya ya waendesha Mashtaka na Wapelelezi mkoani Mara ni muendelezo wa mafunzo yaliyotangulia katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, na Iringa yanayoratibiwa na kutolewa kwa ushirikiano kati ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) ambapo jumla ya washiriki 101 wamehudhuria mafunzo haya.

No comments