Breaking News

MKUKI WAITEGA CCM, POLISI BABATI SAKATA LA MBUNGE GEKUL

 


Mratibu wa MKUKI Anna Kulaya

Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (Mkuki) unaojumuisha mashirika yasiyo ya kiserikali zaidi ya 200 chini ya uratibu wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo barani Afrika (WiLDAF) umetoa tamko kuhusu sakata la Mbunge wa Babati Mjini Mhe. Pauline Gekul kudaiwa kuwafanyia ukatili wa kijinsia vijana wawili... Lifuatalo ni tamko la MKUKI


TAARIFA KWA UMMA

 KULAANI UKATILI WA KIJINSIA ULIOTOKEA KWA VIJANA WAWILI WILAYA YA BABATI- MANYARA

Sisi wana Mtandao wa MKUKI tumeguswa na Ukatili waliofanyiwa vijana wawili  huko Wilayani Babati Mkoa wa Manyara kitendo kinachosadikika kufanywa na Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini na aliyekuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Pauline Philipo Gekul.

Kitendo hiki ni cha kikatili, kinyume na maadili , na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Kinatweza na kudhalilisha utu wa mtu na kuathiri kiafya na kisaikolojia. Vilevile ni kosa la Jinai kwa mujibu wa Kanuni ya Adhabu Sura ya 16. 


Tukio hili limetokea hivi karibuni tukiwa tumeanza kampeni ya Siku 16 za Uanaharakati kupinga  ukatili wa Kijinsia. 

 Sisi wana MKUKI tunalaani kitendo cha kinyama walichofanyiwa vijana hawa wawili. Tunashauri uchunguzi wa haraka ufanyike na endapo itathibitika Mbunge kutenda hili kosa tunashauri Serikali, Bunge na mamlaka husika kuchukua hatua zifuatazo;


1. Bunge la Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania kumchukulia hatua kulingana na kanuni na sheria za Bunge. 

2. Jeshi la polisi Tanzania kuwachukulia hatua Askari wote waliohusika kuvunja Sheria ya Ukamataji kwa Mwandishi wa habari pia wachukuliwe hatua stahiki kwa kosa la kutomfungulia mtuhumiwa mashtaka kwa wakati ilihali kijana alifika kituoni pale akiwa na majeraha.

3. Chama Cha Mapinduzi, CCM kimchukulie hatua Mbunge huyo kwa mujibu wa kanuni zao

4. Shauri hili lipelekwe mahakamani ili haki itendeke kwa wakati

5. Vijana hawa wawili  walipwe fidia kwa Ukatili waliofanyiwa , wapatiwe ushauri nasaha , huduma za afya kwenye hospitali kubwa, ulinzi na kuhakikishiwa usalama wao.

6. Walioshiriki kumsaidia mheshimiwa mbunge huu ukatili nao wachukuliwe hatua.

MKUKI tunamshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kufanyia kazi tuhuma hizi haraka. Tunashauri vyombo vya uchunguzi na mamlaka husika viendane na kasi ya Mh. Raisi ili haki itendeke na kupatikana kwa wakati.

Sambamba na hili MKUKI tunaamini ni  wakati Muafaka kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kutunga Sheria Mahsusi ya kushughulikia vitendo vyote vya Ukatili wa Kijinsia.

Tunatoa pole kwa vijana hawa wawili, wazazi wao na watu wote walioguswa na habari hii. 

MKUKI tunashauri wananchi wote waendelee kupaza sauti zao kipindi cha Kampeni za Siku 16 za kupinga ukatili na hata baada ya kipindi cha Kampeni kutoa taarifa kuhusu ukatili wa kijinsia unaoendelea kutokea maeneo yao. MKUKI tutaendelea kuelimisha jamii juu ya madhara ya ukatili na tunatoa wito kwa jamii yote ya Tanzania kuungana kutokomeza vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia katika nchi yetu.

Kwa ufafanuzi, Mtandao wa kupinga Ukatili wa Kijinsia “MKUKI” ni Mtandao wa mashirika takribani 200 yasiyo ya kiserikali yaliyoungana kupinga na kupambana na kila aina ya ukatili wa Kijinsia nchini Tanzania.

Imetolewa na:

Anna Kulaya

Mratibu wa MKUKI

Kwa niaba ya wanachama wa MKUKI

No comments