Breaking News

MWILI WA ASKARI ALIYEFARIKI KWA KUGONGWA GARI WAAGWA, KUZIKWA LEO KAGERA

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza SACP Wilbrod Mutafungwa akizungumza katika ibada ya kuagwa mwili wa marehemu WP. 3984 Sajenti Stella aliyefariki Jana baada ya kugongwa na gari ya shule wakati akitekeleza majukumu yake ya kikazi.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbrod Mutafungwa amewaongoza mamia ya waombolezaji wakiwemo maafisa, wakaguzi, askari wa vyeo mbalimbali na ndugu kuaga mwili wa askari wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, WP. 3984 Sanjenti, Stella Alfonce (49).


WP. 3984 Sanjenti Stella alifariki jana Novemba 1,2023, eneo la Nyamhongolo akitekeleza majukumu yake baada ya kugongwa na gari ya shule ya Nyamuge ya jijini Mwanza.


Ibada ya kuaga mwili wa askari huyo imefanyika katika Kanisa Katoliki Kigango cha Isegeng'he Parokia ya Nyakato Jijini Mwanza ambapo makundi mbalimbali yameshiriki kuuaga mwili wa askari huyo.


Akiwasilisha salamu za rambirambi kamanda Mutafungwa amesema uhai wa Stella ulitoweka akiwa anafanya kazi ya kusimamia sheria barabarani.


"Mwenzetu amefariki akiwa analitumikia Taifa, tuna kila sababu ya kumuombea na kumkumbuka kwa ushujaa wake" amesema Kamanda Mutafungwa 


Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Janeth Magomi akimuwakilisha Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake (TPFNET) Taifa, Kamishna wa Rasilimali Watu na Vifaa (CP), Suzan Kaganda ametoa salamu za pole kwa Kamanda wa Polisi Mkoa na kuungana na waombolezaji katika kuuanga mwili wa Sanjenti Stella.

Mwili wa Stella umesafirishwa kwenda Bukoba mkoani Kagera kwa ajili ya maziko ambayo yanatarajiwa kufanyika kesho Novemba 3, mwaka huu.

*Kutoka Dawati la Habari Polisi Mwanza*











No comments