Breaking News

MAONESHO YA KWANZA YA UTPC YAFANA, WADAU WAITWA

Na Mwandishi Wetu Dodoma

Maonyesho ya kwanza ya Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) yamefunguliwa rasmi jijini Dodoma huku klabu za waandishi wa habari kutoka mikoa mbalimbali zikionyesha shughuli zao  wanazozifanya.


Maonyesho hayo ambayo yamehudhuriwa na klabu 28 za waandishi wa habari nchini, yanafanyika leo Jumamosi Desemba 9,2023 jijini humo.

Katika mabanda ya klabu hizo, shughuli mbalimbali za klabu zinaonyeshwa ikiwemo kuwasilisha mpango mikakati wake ambao unalenga kuiweka kauli mbiu ya UTPC ya 'Moving from Good to Great' kwenye vitendo.

Mweka Hazina wa Mwanza Press Club Paulina David kushoto, Mwenyekiti wa Mwanza Press Club Edwin Soko na Mratibu wa Mwanza Press Club Lurencia Bernard wakijadiliana jambo  wakati wa maonyesho ya Kwanza ya MPC.

Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Keneth Simbaya amesema maonyesho hayo yatakuwa endelevu huku akidokeza kuwa yanalenga kutoa fursa kwa klabu kuonyesha shughuli wanazofanya katika mikoa yao.


Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Keneth Simbaya akiongea na wanahabari kuhusiana na maonyesho ya kwanza ya UTPC yaliyofanyika katika viwanja vya ofisi hizo zilizopo Uzunguni mjini Dodoma.

"Dhumuni kubwa ni kutoa fursa kama ambavyo ukipita kwenye kila banda kuna fursa nyingi zinaonyeshwa. Jukumu la klabu pamoja na kutoa taarifa wanaweza kuwa sehemu ya kuchochea uchumi wa nchi na ndicho kinachoonyeshws hapa," amesema Simbaya
Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Keneth Simbaya akiongea na wanahabari kuhusiana na maonyesho ya kwanza ya UTPC yaliyofanyika katika viwanja vya ofisi hizo zilizopo Uzunguni mjini Dodoma.

Simbaya amesema UTPC itakusanya majumuisho ya shughuli zinazofanywa na klabu hizo na kuangalia namna itakavyoboresha ili kuziwezesha kuweka falsafa ya 'Moving from Good to Great' kwenye vitendo.

"Wadau hii fursa kwenu kujitangaza na kushirikana na waandishi wa habari, katika maonyesho ya mwaka kesho tunaamini wadau watamiminika ili kuhakikisha wanafikia watu wengi zaidi," amesema Simbaya

Kwa upande wake rais wa UTPC Bw Deogratus Nsokolo amesema maonyesho hayo yanatoa dira na majibu ya namna klabu za waandishi wa habari zinavyojihusisha na jamii huku akiahidi kwamba nguvu itaongezwa katika maonyesho ya mwaka 2024.

"Moja ya vitu vinavyotutia nguvu UTPC ni kuona klabu zinaanzisha vikundi vya kuweka na kukopa. Vikundi hivi vitakuwa mwarobaini wa vyombo visivyolipa mshahara na kutoa  mikataba, hii itasaidia kuongeza uandishi wa habari wenye uhuru na weledi," amesema Nsokolo.

 
 Rais wa UTPC Bw Deogratus Nsokolo akiangalia moja ya vipeperushi katika banda la mmoja wa washiriki wa maonyesho hayo ya kwanza ya UTPC.

Mwenyekiti wa Mwanza Press Club Edwin Soko akielezea mipango ya Mwanza Press Club kwa bodi ya UTPC uliotembelea banda hilo kujua shughuli mbalimbali zinazofanywa na club hiyo.

Mshiriki wa maonyesho hayo, Fatuma Maumba kutoka mkoani Lindi, amesema maonyesho hayo yalichelewa kuanza kufanyika kwa kile alichodai klabu zilikuwa na nafasi ya kujifunza na kubadilishana uzoefu hivyo akaiomba UTPC yawe endelevu.


"Tunawapongeza MPC kwa hatua ambazo wamefikia katika ujenzi wa Ofisi, ambayo sisi LPC tumejifunza kupitia maonyesho haya, nasi tumevutiwa tutalianza hilo," amesema Maumba ambaye ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari (LPC).

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa MPC, Mgongo Kaitira ameipongeza MPC kwa kuja na ubunifu huo huku akidokeza kuwa mbali na kuwakutanisha wanahabari, pia yanatoa mwanya wa kuonyesha fursa zilizopo katika kila klabu nchini.
"Kwa mara ya kwanza tumefanya maonyesho haya tunaamini mwakani, UTPC kwa kushirikiana na klabu za waandishi wa habari nchini, tutafikia lengo la kuandika habari zenye tija na kuleta Maendeleo nchini," amesema Kaitira.

Mwisho.

No comments