Breaking News

MASHIRIKA 6 YANAYOJIHUSISHA NA MAZINGIRA MWANZA YAUNGANA ILI KUPAMBANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI

Na Tonny Alphonce, Mwanza

Katika kuunga mkono mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi wa mwaka 2021 – 2026 mashirika 6 yanayojihusisha na utunzaji wa mazingira na tabia nchi ya jijini Mwanza yameanza kampeni ya kubadilisha tabia za wananchi  katika utunzaji wa mazingira kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari mwanaharakati wa mazingira na mjumbe wa mtandao wa kijinsia  na mabadiliko ya tabia nchi Tanzania Sophia Donald amesema suala la mabadiliko ya Tabia Nchi linagusa watu wa jinsia zote hivyo mpango walionao ni kuhakikisha wanawafikia wananchi ambao ndio wadau wakubwa wa mazingira.

Sophia amesema hatua ambayo wameichukua kwa hivi sasa ni kuwakutanisha wadau wa mazingira pamoja na maafisa kutoka serikalini kwa lengo la kujadiliana na kupata azimio moja ambalo litafanyiwa kazi mashirika yote 6 yaliyoungana.

Mwanaharakati wa mazingira na mjumbe wa mtandao wa kijinsia  na mabadiliko ya tabia nchi Tanzania Sophia Donald akiongea na wanahabari hawapo pichani.

“Kwa hivi sasa katika kuhakikisha  uhamasishaji unayafikia makundi yote tunatumia mikutano ya hadhara ili kufanya uhamasishaji kwa jamii, kushirikiana na vyombo vya habari  na sekta za Kiserikali zinasimamia masuala ya mazingira  na mabadiliko ya tabia nchi”.alisema Sophia

Kwa upande wake Franklin Kamalamo kutoka Taasisi ya Mazingira Bora amesema Katika kuhakikisha kampeni hii ya kupambana na changamoto za tabia nchi inaleta matokeo chanya watatoa elimu kwa pamoja wadau wote wa mazingira na hii itasaidia elimu kufika kwa urahisi.


Franklin Kamalamo kutoka Taasisi ya Mazingira Bora akielezea njia watakazotumia kutoa elimu kwa wananchi juu ya njia za  kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi

“Safari hii tunaamini elimu itafika kwa urahisi kwa kuwa jamii tayari inaona mabadiliko mfano kuongezeka kwa joto, maeneo ya joto kupata baridi kali hivyo nirahisi wananchi kuelewa tunachokisema lakini pia tutatumia wasanii kufikisha ujumbe kwa wananchi”.alisema Franklin

Nae Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Mikono Yetu Organization Maimuna Kanyamala amesema katika kampeni hii wataelekeza nguvu kubwa pia kwenye shule za msingi ambao ni watumiaji wakubwa wa miti ili wajue umuhimu wa kupandamiti kunakoendana na matumizi yao ya kila mwaka.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Mikono Yetu Organization Maimuna Kanyamala akisisitiza jambo wakati akiongea na wanahabari hawapo pichani

“Katika kujenga tabia lazima tuwaguse na hawa wenzetu wa shuleni ili kuhakikisha wanafunzi wanapanda miti na ikiwezekana lazima kila mwanafunzi awe na mti wake hii itasaidia utunzaji wa mazingira”.alisema Maimuna

Naye Afisa mazingira wa halmashauri ya Magu Ngusa Buyamba amesema katika kuhakikisha mapambano hayo ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi ni lazima wahakikishe wanapata taarifa sahihi kutoka katika malamaka sahihi za serikali.

"Kwa mfano mpango wa serikali kwa sasa ni kuwa kila halmashauri inatakiwa  kuhakikisha inapanda miti milioni moja na laki tano, sasa ukiangalia halmashauri hazina uwezo kupanda miti hiyo na hapa ndio wadau wa mazingira wanatakiwa kuingia".alisema Buyamba

Afisa mazingira wa halmashauri ya Magu Ngusa Buyamba akielezea ushirikiano kati ya serikali na wadau wa mazingira

Mtandao wa kijinsia  na mabadiliko ya tabia nchi Tanzania umejidhatiti kuhakikisha unatoa elimu ya mabadiliko ya tabia nchi na kwa sasa mtandao unaendelea na kampeni ya kuielimisha jamii kwa njia mikutano ya hadhara,kutumia vyombo vya habari  pamoja na mitandao ya kijamii.




No comments