Breaking News

TACEC YAJA NA KAMPENI YA MALEZI, MAKUZI NA MAENDELEO YA AWALI YA MTOTO MIAKA 2-3

Na Tonny Alphonce, Mwanza

Shirika la Tanzania Early Childhood Education and Care (TACEC) limeanzisha kampeni ya dakika 30 za kucheza na kujifunza na mtoto nyumbani kila siku ikiwa na lengo la mzazi kushiriki kumuandaa mtoto mwenye umri wa kuanzia miaka 2-3 kwa ajili ya elimu ya awali na kuendelea.

    Bi Ester Macha  ambaye ni mtaalamu wa elimu ya awali 30 za kucheza na kujifunza na mtoto akizungumza na walezi kuhusu umuhimu wa kucheza na mtoto na kumuandaa kwa elimu ya awali

Kampeni hiyo ya TACEC inahusisha mpango jumuishi wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto mwenye umri kati ya miaka 0-8 unaolenga kuhakikisha mtoto anakingwa na hatari zote zinazoweza kuathiri maisha na ustawi wake wa baadae.

Kwa mujibu wa Bi Ester Macha  ambaye ni mtaalamu wa elimu ya awali kutoka TACEC anasema kampeni hiyo ya dakika 30 za kucheza na kujifunza na mtoto nyumbani,kampeni ambayo itamsaidia mzazi kujua uwezo wa mtoto wake katika kutoa maamuzi,kufanya jambo,kutatua tatizo kupitia michezo zaidi ya 30 ambayo wameiandaa kupitia kitabu ambacho kinatoa maelekezo ya michezo hiyo.

Bi Ester Macha mtaalamu wa elimu ya awali kutoka TACEC akizungumzia namna kampeni ya dakika 30 za kucheza na kujifunza na mtoto nyuumbani kwa walezi

Ester amesema kupitia kampeni hiyo wamekuwa wakiwatembelea wazazi majumbani kwa lengo la kutoa elimu namna gani wanaweza kucheza na watoto michezo ambayo itamjenga mtoto kiakili ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya elimu yake ya awali.

“Sisi tuliona kuna pengo hilo la huyu mtoto kutopata maandalizi yoyote ya kumuandaa na elimu ya awali lakini pia katika umri huu wa miaka 2-3 ndio umri ambao mzazi anaweza kugundua kipaji cha mtoto wake kwa kuchezanae lakini pia mzazi anaweza kuelewa uwezo wa mtoto wake katika kujifunza au kufanya vitu na hii itasaidia hata kujua kama mtoto wake anaelewa haraka au taratibu”.alisema Ester

Ester amewataka pia wazazi na walezi kuwa makini katika kuwaadhibu watoto wenye umri huu pale wanapofanya makosa kwa kuwa watoto katika umri huo hujifunza kwa kuona na baadae hujaribu kufanya na ndipo hutokea uharibifu.

“Mtoto ukiona anachukua unga au nchele anajaribu kupika usimchape mkataze kwa maneno ukijaribu kumuelekeza kwamba akitaka kupika achukue mchanga ndio apike asitumie unga au mchele kwasababu atahitaji kula baadae mtoto atakuelewa”.alisema Ester

Nae mkurugenzi wa shirika la Uzao Wetu Yusuph Mtobela amewataka wazazi wenye watoto wa umri wa miaka 2-3 kujua lugha ya mtoto ambayo ni michezo ili kugundua kipaji alichonacho mtoto kupitia michezo anayocheza.

“Binadamu kiasili anavipaji vinane na kuendelea kiasili hivyo mzazi anaweza kugundua na kuendeleza kipaji cha wake wakati anapochezanae  cha msingi michezo hiyo lazima inazingatie usalama wa mtoto na iwe  uhusiano na namna ya kumuendeleza kielimu”.alisema Mtobela

Amesema ili kuhakikisha kuwa kundi hili la watoto linasaidiwa na walezi  shirika la Uzao Wetu limeanzisha mafunzo ya malezi na makuzi ya mtoto mahali pa kazi ambapo wamewalenga wazazi na walezi ambao wanapewa mafunzo ya kujenga mahusiano baina yao na mtoto kwa lengo la kumuandaa na elimu ya awali.

Kwa upande wake afisa elimu ya watu wazima wa manispaa ya Ilemela, Recipitius Magembe amesema kiuhalisia serikali bado haijawaingiza kwenye mfumo watoto wenye umri wa miaka 2-3 na badala yake imekuwa ikijenga vituo vya kutwa vya kulelea watoto kwa lengo la wazazi kupata muda wa kufanya shughuli za kiuchumi na kuwaacha watoto wakipatiwa huduma bora zitakazowezesha uchechemuzi wa bongo zao kuwekwa katika mazingira mazuri ya ukuaji.

Magembe amesema suala hili la watoto hao wa miaka 2,3 kusahaulika linaweza kufanyiwa kazi na serikali endapo wadau watatoa hoja za msingi na kuzipeleka kwa watunga sera kwaajili ya kufanyiwa kazi.

Amesema kuanzisha Vituo vya Malezi na Makuzi ya awali kwa watoto wenye umri kati ya miaka miwili, mitatu na minne nchi nzima ni moja ya mikakati ya kumjenga na kumlinda mtoto.

“Ukitaka kujua serikali ni sikivu angalia kuhusu vituo hivi vya kulelea watoto,baada ya kuonekana vinahitajika takwimu zinaonyesha kuwa Mwaka 2020, Serikali ilisajili vituo 134 vya kulelea watoto wadogo mchana ikilinganishwa na vituo 373 mwaka 2019 na kufanya jumla ya vituo vilivyosajiliwa kufikia 1,677”.alisema Magembe.

Neema Thodas mtaa wa Kasamiko kata ya Luchelele akizungumzia namna alivyonufaika na kampeni ya dakika 30 za kucheza na kujifunza na mtoto nyumbani kila siku

Neema Thodas mama mwenye mtoto wa mwaka mmoja na nusu mkazi wa kata ya Luchelele anasema kabla ya kupewa mafunzo hayo ya namna ya kucheza na mtoto wa umri wa miaka 2-3 kwaajili ya kumuandaa na elimu kumekuwa na mabadiliko makubwa katika malezi yake kwa kuwa hivi sasa amekuwa akicheza na mtoto wake michezo ambayo inamuandaa kuanza kuandika, kuhesabu pamoja na kujua vitu mbalimbali na matumizi yake.

Raheli Sengesa mkazi mtaa wa Kasamiko kata ya Luchelele ambae anaishi na wajukuu wake anasema hakujua kama watoto hawa wenye umri wa miaka2-3 wanaweza kundaliwa kwaajili ya elimu ya awali kwasababu alijua hiyo ni kazi ya walimu pale mtoto anapoanza shule.

Raheli Sengesa mkazi mtaa wa Kasamiko kata ya Luchelele akizungumzia namna alivyonufaika na kampeni ya dakika 30 za kucheza na kujifunza na mtoto nyumbani kila   siku
“Kwa kweli tangu nimeanza kuwafundisha wajukuu wangu kupitia michezo nimegundua watoto wanavitu vikubwa ndani yao kwasababu nimegundua wanao uelewa na jambo akiwa halijui atauliza na baadae atajaribu kulifanya jambo hilo kwa vitendo, watoto ni wadadisi sana”.alisema Raheli

Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 na Mpango wa Maendeleo ya Elimu Msingi (MMEM) 2012- 2016, vimebainisha kuwa elimu ya awali ni moja kati ya vipaumbele vya serikali.    

Kwa Tanzania watoto wenye umri wa miaka 4-5 huanza elimu ya awali na umri wa miaka 5-6 mtoto huanza darasa la kwanza huku watoto wenye umri wa miaka 2-3 hawaguswi na Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi.

No comments