Breaking News

VIJANA WAFUNGA MWAKA KWA KUFANYA USAFI NA KUPANDA MIKOKO ENEO LA SALENDAR BRIDGE




Na Mwandishi wetu ETE

Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Ecoblue Conservancy kwa kushirikiana na ETE, HUDEFO, Mazingira Plus, TCCI , MBRC the Ocean, Chuo cha NIT, wanafunzi wengine wa vyuo mbalimbali pamoja na wananchi mbalimbali wamefanya usafi katika eneo la Mikoko Salendar bridge pamoja na shughuli nyingine ikiwa ni pamoja na upandaji wa mikoko katika eneo hilo.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Uhifadhi wa TFS Prof. Dossantos Silayo wakati wa zoezi hilo linaendelea Afisa Mhifadhi Mkuu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS), Frank Sima amesema zoezi hilo ni utekelezaji wa harakati za wadau wa uhifadhi wa mazingira Tanzania kupitia Taasisi na Asasi zisizo za kiserikali ambao wanaruhusiwa na sera ya misitu ya mwaka 1998 na mkakati wake wa mwaka 2021 -2031 ibara ya nne (4) ambao unaelekeza ushirikishwaji wa wadau katika uhifadhi wa misitu ya aina mbalimbali ikiwemo hifadhi za misitu ya mikoko.

"Moja kati ya kazi za hifadhi za misitu ya mikoko Tanzania kwa ujumla wake na kwengineko kokote ulimwenguni ni kuchuja takataka za aina mbalimbali, takataka ngumu pamoja na takataka kemikali ili zisiingie katika mfumo ikolojia wa matumbawe na mfumo wa bahari wa kina kirefu ambayo ndiyo sehemu ya upatikanaji wa samaki wa aina mbalimbali" alisema Sima

Aliongeza kuwa inapotekea takataka zinakuwa nyingi kutokana na kushindwa kudhibiti taka za majumbani na maeneo ambayo mito inaanzia katika vilele vya milima na katika miji mbalimbali ambapo mito inapita zinasababisha taka nyingi na kupelekea mikoko kuelemewa kutokana na uwepo wa taka hizo ngumu

Sima alitoa rai kwa jamii kuwa ili mazingira ya mikoko yaendelee kuwa salama wanajamii mbalimbali kupitia asasi mbalimbali za kiraia wana wajibu wa kuhamasisha umma kushiriki katika kusafisha mazingira ya ardhi ya mikoko ambayo imeelemewa na Taka ngumu kwa kuendelea kuzitoa ili zisiendelee kuathiri bahari.

Wakati huo huo ETE walishiriki katika kufanya usafi eneo hilo kwa lengo la kuweka mazingira safi lakini pia kutumia Dijitali kuyasemea mazingira ambayo hayawezi kujisemea yenyewe, kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa mbalimbali ya mtandaoni kwa lengo la kufikisha ujumbe wa kukumbusha jamii kuendelea kutunza mazingira na kuyapenda ili yaendelee kuwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo

PICHA ZOTE NA ETE (instagram @official.ete)


No comments