Breaking News

WANANCHI WALIA KITUO CHA AFYA HAKITOI HUDUMA LICHA YA UJENZI WAKE KUKAMILIKA

 Na Tonny Alphonce, Sengerema

Wananchi wa kijiji cha Kanyerere wilayani Sengerema Mkoani Mwanza wamekuwa wakilazimika kutembea umbali wa kilometa 15 kufuata huduma za mama na mtoto kutokana na kituo cha afya cha Kanyerere kutofanyakazi licha ya ujenzi wake kukamilika.

Kituo cha afya cha Kanyerere ambacho ujenzi wake ukamilika

Marrytilida Mpina ambae ni mkazi wa kijiji cha Kanyerere amesema pamoja na kuchangia fedha kwaajili ya ujenzi huo unaosimamiwa na mradi wa TASAF bado hakuna dalili zozote za kuanza kufanyakazi kwa kituo hicho.
Marrytilida Mpina mkazi wa kijiji cha Kanyerere akielezea changamoto wanazokutananazo kutokana na kituo cha afya cha Kanyerere kutokufanyakazi licha ya kukamilika

“Kama unavyoona kila kitu wananchi tumechangia lakini hakuna daktari yoyote aliyeletwa hapa hakuna dalili ya dawa kuletwa hapa na kina mama wajawazito na watoto ndio wanaoteseka katika upatikanaji wa huduma za afya”.alisema Marrytilida

Marrytilida amesema kutokana na umbali wa kupata huduma za mama mjamzito katika kijiji hicho wananchi wamekuwa wakilazimika kwenda kupata huduma Busilasoga au Igaka na kusababisha baadhi ya kina mama kujifungua wakiwa njiani na kuhatarisha maisha ya mama na mtoto.

Kwa upande wake Nassari Mkoloka mkazi wa kijiji hicho cha Kanyerere amesema wanachohitaji hivi sasa ni wataalamu wa afya ambao watatoa huduma katika kituo hicho.

Nassari Mkoloka mkazi wa kijiji hicho cha Kanyerere akitoa wito kwa Serikali ihakikishe kituo cha afya Kanyerere kinaanza kufanyakazi

 “Haiwezekani tukaendelea kuishi hapa bila kupata huduma wakati michango ya kufanikisha ujenzi tulitoa sasa tunashangaa jengo limekamilika lakini bado hakuna dalili zozote za kuanza kutupa huduma hapa”.alisema Mkoloka

Akitolea ufafanuzi wa kuchelewa kuanza kutoa huduma kwa kituo hicho cha afya Kanyerere mkurugenzi wa halmashauri ya Sengerema Binuru Shekidele kuchelewa kuanza kazi kwa kituo hicho kumesababishwa na baadhi ya vijiji kushindwa kuchangia fedha za kukamilisha ujenzi wa kituo hicho cha afya.

“Mhe waziri  kwa mujibu wa mujibu wa taratibu za TASAF ,mradi huu wananchi walitakiwa kuchangia asilimia 10 na TASAF asilimia 90 ,sasa  kuna baadhi ya vijiji vinasuasua kuweka nguvu zao ndio maana mradi huu unachelewa kuanza kwa wakati”. Alisema Binuru

Nae mwenyekiti wa CCM wilaya ya Sengerema Marco Makoye amesema kitendo cha jengo kukamilika na kutokutoa huduma ni kitendo cha watendaji kuichonganisha serikali na wananchi.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Sengerema Marco Makoye akielezea hisia zake kuokana na kituo cha afya Kanyerere kutokufanyakazi licha ya ujenzi wake kukamilika

“Hapa watu wanaona majengo tena yamekamilika na watu wanatembea kilometa 15 kwenda kupata huduma hivi CCM tukirudi kuomba kura tutapewa kweli”.alisema Makoye

Akizungumza na wanachi hao wa kijiji cha Kanyerere Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mohammed Mchengerwa amesema haoni sababu ya msingi ya kucheleweshewa wananchi huduma wakati kituo kimekamilika kwa asilimia 96.

Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mohammed Mchengerwa akitoa maagizo ya nini kifanyike kuhakikisha kituo cha afya Kanyerere kinaanza kutoa huduma

“Kwa hiyo maelekezo yangu mkurugenzi jiongeze na ujiamini nikirudi tena na kukuta jambo hili halijafanyiwa kazi nitakusimamisha umepewa nafasi hii na Mh Rais msaidie wananchi wasikose huduma kwa uzembe wa watu wachache”.alisema Mchenjerwa

Kutokana na kutoridhika na maelezo ya mkurugenzi Mchenjerwa amesema kinachoonekana katika mradi huo ni waliopewa dhamana kushindwa kusimamia zoezi la ujenzi wa kituo hicho na akatoa siku 14 kuhakikisha kituo hicho kinaanza kutoa huduma za awali kwa wananchi.

“Katibu tawala nakuagiza simamia zoezhili waandikie barua wahusika wote ili mradi huu uanze,h atuna sababu ya kuwapa hasira wananchi wetu kituo wanakiona lakini wanaendelea kuteseka kupata huduma za afya”.alisema Mchenjerwa

Pamoja na changamoto ya kijiji cha Kanyerere huduma za afya ya mama na mtoto  zimeendelea kuimarika wilayani Sengerema huku kiwango cha wajawazito  wanaojifungulia katika vituo vya afya ikiongezeka ambapo kati ya wanawake wajawazito  wanane hadi kumi hujifungulia hospitali kila siku.

vifo vya kinamama wajawazito navyo vimepungua kutoka 11/100000 mwaka 2014,8/100000 disemba 2015,6/100000 hadi kufikia juni 2017 vifo vimeripotiwa 3/100000.

Kutatuliwa kwa changamoto hiyo ya kituo cha afya katika kijiji cha Kanyerere wilayani Sengerema mkoani Mwanza kutaenda sambamba na malengo ya mpango wa Taifa wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ambao unajikita katika kutatua changamoto za ukuaji wa mtoto katika ukamilifu wake kuanzia mwaka 0-8

No comments