Breaking News

KIZAZI CHENYE USAWA WA KIJINSIA KUPUNGUZA VITENDO VYA KIKATILI KWA WATOTO

Na Tonny Alphonce, Mwanza

Imeelezwa kuwa kuongezeka kwa uelewa kwa  jamii  juu ya madhara yatokanayo na ukatili wa kijinsia na kutoa taarifa za matukio ya ukatili ni sababu moja wapo inayopelekea  kuongezeka kwa matukio ya ukatili.

Serikali kuanzisha pia madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya Polisi ambapo hadi sasa madawati 420 yameanzishwa na yanafanya kazi kwa Lengo la kuwawezesha wahanga kupata huduma stahiki katika vituo vya Polisi na kutendewa haki ni sababu nyingine ya inayopelekea kuonyesha kuwa matukio ya ukatili yameongezeka.

Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana akizungumza hivi karibuni katika mafunzo ya kizazi chenye usawa kwa maafisa maendeleo ya jamii kutoka mikoa 15 amewataka wahakikishe wanaunga mkono jitihada za serikali za kutokomeza vitendo vya kikatili kwa wanawake na watoto.

Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana akizungumza katika mafunzo ya kizazi chenye usawa kwa maafisa maendeleo ya jamii kutoka mikoa 15

Balandya alisema uzingatiaji wa masuala ya jinsia ni mojawapo ya nguzo muhimu ili kufikia maendeleo jumuishi na endelevu kiuchumi, kijamii, kisasa na kiutamaduni kwa taifa.

Amesema Serikali kwa kuona umuhimu wa mafunzo hayo imewashirikisha ili kwenda kuleta mageuzi chanya ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake hapa nchini.

“Baada ya mafunzo haya natarajia nyie maafisa maendeleo ya jamii mtaenda kuisaidia jamii hata suala hili la ukatili kwa watoto wadogo ambao wao hawawezi kujitetea nendeni mkawasaidie kwa kuwaelimisha wazazi na walezi wao umuhimu wa kuripoti matukio haya ya kikatili kwa lengo la kuyapunguza matukio haya”.alisema Balandya

Balandya amesema wanawake wakiwezeshwa kiuchumi mambo mengi yatakaa sawa katika jamii likiwemo pia suala la uhakika wa ulinzi na usalama wa mtoto katika jamii.

 Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi Idara ya jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum Juliana Kibonde amesema kipindi cha mafunzo hayo ya siku mbili washiriki wamefundishwa namna ya kubuni na kuandaa mikakati mbalimbali ya kiutekelezaji kwenye maeneo yao ya kazi ikiwemo mkakati wa mawasiliano.

Mkurugenzi msaidizi Idara ya jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum Juliana Kibonde akiongea katika mafunzo ya kizazi chenye usawa kwa maafisa maendeleo ya jamii kutoka mikoa 15

Juliana amesema washiriki pia wamefundishwa njia mbalimbali za kuzuia vitendo vya kikatili kama njia moja wapo ya kuhakikisha wanawake na watoto wanakuwa na salama badala ya kuwekeza nguvu kubwa katika kupambana na vitendo vya kikatili baada ya kutokea.

“Pamoja na kuwa tuna wasisitiza mkatoe elimu kwa wazazi na walezi lakini pia Serikali nayo inajipanga kuongeza vituo vya kuripoti matukio ya ukatili ili kuhakikisha matukio hayo ya ukatili yanapungua katika jamii”.alisema Juliana

Akizungumza kwa niaba ya washiriki, afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Tabora, Panin Kerika amesema mafunzo hayo yamewakumbusha wajibu wao na yamekuwa chachu ya kufanya kazi kwa weledi hasa katika eneo la usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake.

“Tukisimamia haki na kumuwezesha mwanamke ni wazi tunaenda kuwa na jamii yenye maendeleo na salama nasema hivyo kwa sababu mama akiwezeshwa inamaana na mtoto ana kuwa salama katika malezi na makuzi yake”.alisema Panin

Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni miongoni mwa mataifa yaliyoshiriki kupitisha na kukubali kutekeleza Haki na Usawa wa Kiuchumi kama njia ya kufikia usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake.

Mkoa wa Mwanza unajumla ya mabaraza ya watoto 178 katika ngazi ya mkoa na halmashauri zote yenye jumla ya wajumbe 1729, mkoa unawawakilishi ngazi ya taifa na katika kuimarisha masuala ya watoto kuna klabu za watoto 453 kati ya hizo 323 za shule ya msingi na 130 Sekondari zikiwa juhudi mbalimbali ambazo mkoa unafanya upande wa ulinzi na usalama kwa mtoto na wanawake.

No comments