Breaking News

WAZAZI WATAKIWA KUHAKIKISHA WATOTO WANAPATIWA CHANJO ZOTE MUHIMU

 Na Tonny Alphonce, Mwanza

Inaelezwa kuwa utoaji Chanjo kwa watoto kila mwaka huokoa maisha ya watoto wafikiao milioni 3 kila mwaka.

Mtoto akipatiwa Chanjo humkinga maradhi mbalimbali ukiwemo ulemavu na vifo vitokanavyo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ikiwa ni pamoja na surua, homa ya ini (hepatitisi B), dondakoo, kifaduro, nimonia, polio, kuhara kunakosababishwa na virusi vya rota, rubela na pepopunda.

Kisayansi chanjo ni kitendo cha kupewa kinga mwili kwa njia ya kuamsha vitoa kinga viwe tayari kupambana na adui ambaye wanamjua tayari.

Kwa kuliona hilo Shirika la DUNIA RAFIKI lenye makao yake makuu yake mtaa wa veta, Buhongwa, wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza kwa kushirikiana na Zahanati ya Shadi pamoja na wahudumu wa afya liliendesha zoezi la utoaji wa matone ya Vitamin A kwa watoto wenye umri wa miezi 8 hadi miaka 4katika kituo cha malezi MTOTO WETU ambapo watoto 43 walipatiwa matone hayo.

Akizungumzia zoezi hilo mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Sophia Hamisi Asenga amesema mara baada ya kufuangua kituo cha Kijamii cha malezi, MTOTO WETU katika eneo hilo la Luchele na kuanza kupokea watoto na kuwapa huduma za ujifunzaji wa awali, lishe, afya, uchangamshi, malezi pamoja na ulinzi na salama kwa watoto wenye umri wa miaka 3-4 waligundua baadhi ya watoto kuwa na matatizo ya kiafya na ukuaji.

Tulipoanza kuwapokea watoto hawa wenye umri wa miaka 3-4 tulianza kuona changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wanaofika kituoni,wengine walikuwa na changamoto za kiafya na wengine walikuwa na changamoto ya ukuaji na ndipo nikaona ni vema niwalete wataalamu wa afya waweze kuwapima watoto na kuzungumza na wazazi na walezi ili tuweze kuwasaidia watoto ambapo tulibaini kuna watoto hawajapatiwa chanjo yoyote katika ukuaji wao.alisema Sophia

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la DUNIA  RAFIKI Sophia Hamisi Asenga akiongea na wazazi kabla ya zoezi la utoaji chanjo

Kabla ya kuanza Zoezi la kuwapatia chanjo watoto wataalamu wa afya walitoa elimu kwa wazazi na walezi wa watoto zaidi ya 41  juu ya umuhimu wa matone ya Vitamin A kwa watoto wenye umri chini ya miaka 4 ambapo wazazi, walezi na wajawazito walipata elimu hiyo na baadaya elimu hiyo kwa pamoja walikubaliana watoto wao wapatiwe chanjo hiyo yam atone

Akizungumza kabla ya utoaji wa chanjo hiyo mhudumu wa afya wa mtaa wa Nganza. Bi. Consolata Ligola alisema upungufu wa Vitamin A mwilini husababisha madhara mengi kwa mtoto ikiwemo ukosefu wa kinga mwilini, hivyo mtoto kuwa katika hatari ya kupata magonjwa mara kwa mara, kutoona vizuri katika mwanga hafifu.

Bi. Consolata aliendelea kusema, bado elimu inatakiwa kwa jamii ili kuhamasisha wananchi kutumia vyakula vyenye vitamini A kwa watoto, ili kuepukana na matatizo ya lishe duni yanayowakumba watoto wengi wanaoishi pembezoni.

Mhudumu wa afya wa mtaa wa Nganza. Bi. Consolata Ligola akitoa chanjo ya matone kwa watoto

Nae mwenyekiti wa Mtaa wa Nganza, ndugu Phinias Mayingu alisema wao kama viongozi wa serikali ngazi ya chini ni wajibu wao kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.

Nimefurahishwa na zoezi hili la kutoa majone ya Vitamin A kwa watoto hapa kituoni, nawapongeza sana walio ratibu zoezi hili, nina toa wito kwa jamii kujitokeza kwa wingi pale inapotokea fursa kama hizi zinazo walenga watoto kwani ni haki yao ya msingi kupata kupata huduma zote muhimu za afya katika ukuaji wao”alisema Mayigu

Kutokana na umbali wa kufika katika zahanati ya Shadi ambapo wazazi hulazimika kutembea umbali wa kilometa 2-3 na wengi kushindwa kufika wamefurahia kusogezewa huduma hiyo ya utoaji matone kwa watoto wao.

Wazazi na watoto wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupatiwa chanjo 

Ester Tuluchengwa mmoja wa wazazi ambae mtoto wake alipata chanjo ya m atone ameshukuru kwa shirika la DUNIA RAFIKI kwa kuwasogezea huduma hiyo karibu na kutoa fursa ya watoto kupata chanjo hiyo.

“Tuna shukuru sana kwa huduma hii na tunatamani iwafikie watoto wengi zaidi, kuna watoto wengi wapo mtaani hawapati huduma hii kutokana na changamoto mbalimbali za maisha, ukosefu wa elimu juu ya umuhimu wa matone ya Vitamin A na madini lishe mengine elimu niliyo ipata leo sitabaki nayo peke yangu bali nitawaelimisha wengine na kuhamasisha pia”. Alisema Ester

Ester amesema anakiri kuwa kumekuwa na maneno mengi ya upotoshaji kuwa chanjo ama matone yanamadhara kwa watoto ikiwa ni pamoja na kuua kizazi lakini baada ya kupata elimu hiyo amegundua kuwa maneno hayo hayana ukweli wowote.

Mwaka 2022 mkoa wa Mwanza ulitoa chanjo kwa watoto 965229 ili kuwakinga na ugonjwa Polio ambapo mkoa uliweza kuvuka lengo kwa asilimia 114 na hii ilitokana na jamii kupata elimu ya kutosha.

Kutatuliwa kwa changamoto za kiafya kwa watoto ikiwemo kupatiwa chanjo zote muhimu kutaenda sambamba na malengo ya mpango wa Taifa wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ambao unajikita katika kutatua changamoto za ukuaji wa mtoto katika ukamilifu wake kuanzia mwaka 0-8

No comments