Breaking News

WAZAZI, WALIMU NA WANAFUNZI WAPEWA ELIMU YA KUTENGENEZA ZANA ZA KUJIFUNZIA WATOTO WA MADARASA YA AWALI

     Na Tonny Alphonce, Mwanza

Zana za kujifunzia na kufundishia huwakilisha vifaa vyote ambavyo mwalimu hutayarisha na kutumia wakati wa mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji ili zimrahisishie ufundishaji wake na kuwafanya wanafunzi waelewe somo kirahisi zaidi.

Mwalimu anapotumia zana mwanafunzi hupata faida kwa kujifunza zaidi  kwa kuona ,kugusa, kuonja,kunusa na kusikia kwa kutumia njia hii mtoto hufurahia somo pia humpatia mtoto maarifa na ujuzi kwa njia ya mkato na ujuzi wa maarifa hayo huwa vigumu kusahaulika upesi.

Pamoja na faida hizo kumekuwa na tatizo la wazazi kushiriki  katika kutengeneza zana hizo za kujifunzia watoto ambapo baadhi ya wazazi hukwepa wakidhani ni gharama kubwa kuandaa zana hizi ambazo kiuhalisia hutengenezwa na malighafi zilizopo katika mazingira yao yanayowazunguka.

Kwa kuliona hilo Shirika la Tanzania Eary Childhood Education and Care -TECEC kwa kushirikiana na walimu wa madarasa ya awali katika shule ya  msingi ya Luchelele pamoja na wazazi wameunda  zana na vifaa vya kujifunzia na kuchezea kwa watoto wa darasa la awali kwa kutumia vifaa vinavyopatikana katika mazingira ya shule.

Walimu wa madarasa ya awali katika shule ya  msingi ya Luchelele, Wazazi na Wanafunzi wakishiriki kutengeneza zana na vifaa vya kujifunzia na kuchezea watoto.

Mkurugenzi wa TECEC Joel Elphas anasema wao kama shirika wanajua umuhimu watoto  kujifunza na kucheza na kupitia zana mbalimbali za kujifunzia kutaweza kukuza ujuzi wao wa kijamii, kiakili, kimwili na kihisia.

Joel amesema kupitia vifaa hivyo vya ubunifu vinatoa uhakika kwa watoto kupata fursa ya kujifunza kwa njia ya vitendo na kujifurahisha, wakati pia wakichunguza mazingira yao ya karibu.

“Mwanzoni ilikuwa ngumu kuwapata wazazi ili nao washiriki katika utengenezaji wa zana hizi lakini baada ya kuwaelimisha tumepata ushirikiano mkubwa na tumefikia lengo kama taasisi kutengeneza zana nyingi ambazo zitakuwa msaada mkubwa kwa vijana”.alisema Joel

Wazazi na baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Luchelele wakishiriki katika zoezi la utengenezaji wa zana za kujifunzia wanafunzi wa madarasa ya awali.

Amesema wanajivunia kuwa sehemu ya juhudi hizo za kipekee kwa kuwa zimewezesha upatikanaji wa elimu bora na fursa za kujifunza kwa watoto  na amewashukuru  walimu wa madarasa ya awali, wazazi na walezi kwa mchango wao mkubwa na ushirikiano wao katika kufanikisha mradi huo wa kutengeneza zana za kujifunzia.

Joel amewataka wazazi kujenga utamaduni wa kutengeneza zana za kujifunzia wao pamoja watoto wao kwa kuwa malighafi zote zinapatikana katika mazingira waliyopo na kama watahitaji msaada wa kiufundi wanaweza kuwasiliana na shirika la TECEC kwa msaada zaidi.

Ester Macha  ambaye ni mtaalamu wa elimu ya awali kutoka TECEC amesema kuwa katika kutekeleza zoezi hilo wazazi  na wanafunzi walishirikishwa ili kutoa mawazo yao na michango yao ya ubunifu na kwa pamoja wakafanikiwa kutengeneza zana za kujifunza ambazo zilikuwa rahisi kwa watoto kuelewa na kufurahia ujifunzaji shuleni.

Ester Macha  ambaye ni mtaalamu wa elimu ya awali kutoka TECEC akiupamba mti kwa namba kwa lengo la kuwasaidia watoto kujua kuhesabu.

“Tulibaini kwamba vifaa kama vile chupa za plastiki, maboksi,Sponji na vitu vingine vya kawaida vinaweza kutumiwa kutengeneza zana hizi za kuchezea na kujifunza zikiwa zinahitaji ubunifu bila gharama kubwa kwa kuwa  rasilimali zote zipo kinachohitajika ni kutengeneza tu vifaa hivyo”.alisema Ester

Mwalimu Zawadi Kokutangilila amelishukuru shirika la TECEC kwa kuwapa ujuzi wa namna ya kutengeneza zana za kufundishia kwa watoto wa madarasa ya awali na kuwaomba wazazi ambao wamepewa ujuzi kuwa mabalozi wazuri kwa wazazi wengine ili nao wapate ujuzi huo.

Nae mzazi Joel Mafuru na Agness Masanja  walioshiriki katika zoezi  hilo wamesema mwanzoni hakuwakujua kama zana hizo ni muhimu katika ujifunzaji wa mtoto lakini wameshuhudia jinsi watoto walivyochangamka na kupata furaha wanapojifunza kupitia zana hizo.

“Kwa sasa ninao uwezo wa kutengeneza zana hizi na kuanzia leo takuwa namtengenezea mwanangu ili ziweze kumsaidia katika safari yake hii ya masomo ya darasa la awali”.alisema Mafuru

Kanuni za vituo vya kulelea watoto wadogo mchana na watoto wachanga ya mwaka 2012 inahusisha mchakato  wa uandaaji wa kiongozi cha utengenezaji wa vifaa vya michezo na kujifunzia watoto chini ya miaka 5.

Vilevile, uelewa juu ya umuhimu wa ujifunzaji kupitia michezo haukupewa kipaumbele katika ngazi zote za maamuzi, udhibiti ubora, watoa huduma, waelimishaji na jamii kwa ujumla ikiwemo wazazi.

Ukosefu wa vifaa vya kuchezea watoto, vitabu, uelewa na ujuzi kuhusu malezi na wazazi kutokuchangamana na watoto mara kwa mara nayo imeripotiwa kama changamoto.

No comments