Breaking News

CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA NYANZA CHAANZA KUVUNA SAMAKI KWA NJIA YA VIZIMBA

Na Tonny Alphonce, Mwanza


Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mwanza, Hilda Boniphace, amekipongeza chama kikuu cha ushirika Nyanza kwa kuanza kuvuna samaki kwa njia ya vizimba. Hii ni awamu ya kwanza ya uvunaji na inatarajiwa kuvuna zaidi ya tani 30 za samaki.

Bi. Boniphace amesema kuwa hatua hii ni kubwa na inaonyesha mafanikio licha ya changamoto zilizopo kwenye ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba. Ameongeza kuwa wengine wameshindwa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na wizi wa samaki, lakini chama cha Nyanza kimefanikiwa.

Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mwanza, Hilda Boniphace akiongea na waandishi wa habari baada ya kuvitembelea Vizimba vya Samaki vinavyosimamiwa na Chama Kikuu Cha Ushirika Nyanza

"Sasa nyinyi ni wazoefu, mmeweza kuuendesha mradi huu wa vizimba vinne. Wengine wamefeli njiani, wengine wamekuwa wakilalamika samaki wanaibiwa lakini Nyanza mmeweza na sasa nyie sio wageni tena maana mnajua samaki wanahitaji nini, wapi mnaweza kupata vifaranga vya samaki na wapi mtapata chakula cha samaki ni vema mkaendelea kujiimarisha katika mradi huu," alisema Bi. Boniphace.

Amewataka viongozi wa chama hicho kuangalia namna ya kuwekeza zaidi kwenye mradi huo kwa kutumia fedha zitakazopatikana kupitia vyanzo vingine vya mapato.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Chama kikuu cha Ushirika Nyanza, Leonard Lyabauma, ameiomba serikali kuendelea kuwawezesha ili waweze kuendeleza mradi huo.

Leonard Lyabauma akizungumzia namna Chama Cha Ushirika Nyanza kilivyoanza kunufaika na Vizimba vya Samaki

Bwana Lyabuma amesema kuwa eneo la ushirika ndilo chombo pekee kinachoweza kuwakomboa watu wengi kwa mara moja na kuiomba serikali kuendelea kuwekeza na kusaidia vyama vya ushirika ili viwe imara kiuchumi kwa faida ya serikali yenyewe na wanaushirika.

"Kwa hivi sasa tumeanza kuvuna samaki, kina mama na vijana wameweza kupata samaki kwa bei nzuri na kwenda kuwauza na hivyo kuunga mkono usemi wa serikali wa uchumi jumuishi ambapo pande zaidi ya mbili zinanufaika kwa pamoja," alisema Bwana Lyabuma.

Maria Herman muuzaji wa Samaki kutoka Kisesa mkoani Mwanza akielezea namna wanavyonufaika na Samaki wa Vizimba

Nao Ally Hemed na Maria Herman, wauzaji wa samaki kutoka maeneo ya Kirumba na Kisesa, wamekiomba chama cha ushirika Nyanza kuongeza vizimba ili samaki waweze kupatikana kwa muda wote na kukidhi mahitaji ya soko la samaki ambayo ni makubwa kwa hivi sasa.


Ally Hemed muuza Samaki Mkazi wa Kirumba Mkoani Mwanza akielezea namna wanavyonufaika na Samaki wa Vizimba

Chama kikuu cha ushirika Nyanza ni miongoni mwa wanufaika na mkopo wa masharti nafuu kupitia wizara ya kilimo na mifugo na walifanikiwa kuanza ufugaji wa samaki katika vizimba vinne ambapo tayari wameanza kuvuna samaki hadi tani 30.

No comments