Breaking News

WANANCHI WALIPONGEZA JESHI LA POLISI MWANZA KWA KUWAOKOA WATOTO WAWILI WALIOTEKWA

 Na Tonny Alphonce, Mwanza

Wananchi mkoani Mwanza wamelipongeza jeshi la Polisi mkoani humo kwa kufanikiwa kuwaokoa watoto wawili wanafunzi wa shule ya Blessing waliokuwa wametekwa na watu wasiojulikana wakati wakienda shule.


Wakizungumzia tukio hilo lililotekea tarehe 05/02/2025 wakati watoto Magreth Thobias (8) na Fortunatus Jophrey (5) walipotekwa wakati wakisubiria Bus la shule, wananchi hao wamesema jeshi la Polisi mkoani Mwanza linastahili pongezi kwa kuwa lilianza kufanyakazi usiku na mchana kuhakikisha watoto hao wanapatikana wakiwa hai.

Emmanuel Mlaki mkazi wa Mkolani mkoani Mwanza amesema ushirikiano uliofanya kati ya wananchi na jeshi la Polisi unapaswa kuendelezwa ili kukomesha vitendo vya uhalisi ambavyo vimekuwa vikitokea mkoani Mwanza.

Kamanda wa Polisi tumemsikia akisema jeshi la Polisi limefanikiwa kuwaokoa hao watoto waliokuwa wamefichwa na watekaji katika mtaa Nyarubugoya Nyegezi na tumewaona watoto wakiwa salama lakini watekaji wameuwawa jeshi letu kwa kweli limefanya kazi kubwa sana na linastahili pongezi.alisema Mlaki

Nae Suzan Kimaro mkazi wa Mtaa huo wa Nyarubugoya amesema kila mwananchi anawajibu wa kuwalinda watoto kwa kuwa hawawezi kujipigania wenyewe hasa wanapoenda shule na wakati wa kurudi nyumbani wanakuwa katika hatari zaidi.

Sisi wanajamii tunatakiwa kuwa walinzi wa watoto wetu maana wengine wanaenda shule kwa miguu na ikitokea unaona mtoto analia au anaomba msaada jaribu kumsaidia maana huenda ndio wakawa watekaji wenyewe.alisema Susan

Tarehe 05/02/2025 watoto Magreth Thobias (8) na Fortunatus Jophrey (5) walitekwa  wakiwa njiani kuelekea shuleni majira ya saa 12:30 asubuhi eneo la Kapripoint mkoani Mwanza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la Dunia Rafiki Sophia Asenga amesema suala la usalama na ulinzi wa mtoto ni la jamii nzima na kuwataka wananchi kuwalinda watoto popote wanapokuwa kwa kuwa watu wenyenia mbaya wamekuwa wakiwatumia watoto ili waweze kujipatia kipato jambo ambalo halikubaliki

Akidhibitisha kupatikana kwa watoto hao ,kamanda wa Polisisi mkoani Mwanza  Wilbroad Mtafungwa amesema  watoto hao wamepatikana baada ya Polisi kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema  na kifatilia hadi kwenye nyumba waliokuwa wamehifadhiwa.

Kamanda wa Polisisi mkoani Mwanza  Wilbroad Mtafungwa akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya watoto Magreth Thobias  na Fortunatus Jophrey kuokolewa na polisi kutoka kwa watekaji

Kamanda Mtafungwa alisema polisi walipofika katika nyumba waliyokuwa wamehifadhiwa watoto hao na watekaji ambao majina yao hayakuweza kupatikana walianza kujihami kwa kutumia mapanga,nondo na jambia ndio polisi waliamua kutumia risasi za moto na kufanikiwa kuwaua pale pale.

Watoto Magreth Thobias na Fortunatus Jophrey  baada ya kuokolewa walipelekwa katika hospitali ya Rufaaa ya Mkoa wa Mwanza  Sekou Toure kufanyiwa uchunguzi wa afya zao.

Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT- MMMAM) inasisitiza suala la ulinzi na usalama wa mtoto ikieleza kwa upanda namna jamii na wazazi wanavyopaswa kuwajibika katika suala la ulinzi na usalama wa mtoto huku mzazi akitajwa kama mlinzi wa kwanza wa mtoto ambae atawajibika kuratibu mienendo yote ya mtoto kuanzia asubuhi hadi usiku anapoenda kulala


No comments