Breaking News

SHULE YA SEKONDARI MESSA YASHEREKEA MAHAFALI YA TISA, DC AWAPONGEZA WAZAZI KWA KUWEKEZA KWENYE ELIMU.

 Na Tonny Alphonce,Mwanza.

Wazazi mkoani Mwanza wamepongezwa kwa kuwekeza katika elimu kwa Watoto wao hasa wale wa jinsia ya kike.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza Bi Amina Makilagi wakati akizungumza na wazazi na wanafunzi wa shule ya sekondari ya upili ya Messa katika mahafali ya 9 ya shule hiyo iliyopo kata ya Buhongwa wilayani Nyamagana.

Bi Makilagi amesema mkoa wa Mwanza umepiga hatua kubwa kwa upande wa elimu kwa kuwa wazazi na walezi wamekuwa na mwamko mkubwa wa kuwapeleka watoto shule hali inayopelekea watanzania wenye uchumi mzuri kuwekeza katika elimu na kuisaidia serikali.

“Nimeamua kuja mimi mwenyewe kwenye mahafali haya kwa lengo la kukupongeza wewe mwekezaji kwa niaba ya serikali kwa kuwa mnaisaidia serikali kwa kuwekeza katika elimu kwa sababu serikali peke yake isingeweza”alisema Bi Makilagi.

Wanafunzi wa kidato cha Nne Shule ya Sekondari ya Upili Messa wakitoa burudani wakati wa mahafali ya 9 ya shule hiyo.

Bi Mkilagi amempongeza Mwl Mkurugenzi  wa Shule ya Sekondari ya upili ya Messa kwa uwekezaji mkubwa hasa upande wa maabara na madarasa ambao unawapa nafasi wanafunzi kusoma vizuri bila kujibana.

Akijibu risala iliyosomwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo kuhusiana na changamoto ya barabara Bulale inayopita shuleni hapo pamoja na changamoto ya chemchem katika viwanja vya michezo vya shule hiyo,Bi Makilagi amesema tayari serikali imetenga fedha shilingi milioni 15 za kukarabati barabara ya bulale kwa kiwango cha lami na kuhusu tatizo la chemchem amesema atatuma wataalamu kuchunguza suala hilo na kuangalia namna ya kutatua tatizo hilo.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Upili Messa Bwana Mazula  akisoma Risala ya shule hiyo mbele ya mgeni rasimi Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Bi Amina Makilagi.

Kwa upande wake mkurugenzi wa shule hiyo Geofrey Messanga amewataka wazazi kulipa ada kwa wakati ili kuisaidia shule hiyo kufanikisha mipango yake na kutoa ahadi kwa wazazi wategemee matokeo mazuri kwa mwaka huu kutokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya kati ya walimu na wanafunzi wa kidato cha nne.

Nao baadhi ya wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani yao ya kidato cha nne wamesema wamejiandaa vizuri na wanategemea kupata daraja la kwanza na wakifeli wanategemea kupata daraja la pili.

Wanafunzi wa kidato cha nne shule sekondari ya upili Messa wakifatilia hotuba ya mgeni rasimi.

Katika matokeo ya kidato cha sita ya mwaka jana wanafunzi wote wa shule ya sekondari ya upili Messa walifaulu na kujiunga na masomo ya elimu ya chuo kikuu.

No comments