Breaking News

WAOMBA HUDUMA YA MAJI WAPATE MUDA WA KUHUDUMIA FAMILIA:

 Na Tonny Alphonce,Shinyanga

Wanawake wa Kijiji cha Mwakilosa Mkoani Shinyanga wameiomba serikali kuwapatia huduma ya maji safi  ili waweze kupata muda wa kuhudumia familia.

Wanawake hao wamesema Kijiji chao kina shida kubwa ya maji kiasi kwamba inawabidi watembea Zaidi ya kilometa 9 kutafuta maji kwaajili ya matumizi ya nyumbani.

Salome Mchila mama wa Watoto wanne amesema Watoto wake wamekuwa na wakati mgumu wa kupata kifungua kinywa kwa kuwa kila siku lazima aamke saa 10 alfajiri kwaajili ya kwenda kutafuta maji ya kutumia.

“Mtoto wangu wanne ana mwaka mmoja nimekuwa sipati hata muda wa kumnywesha uji wakati kwa kuwa kila siku asubuhi lazima nitoke kwenda kutafuta maji na saa 9 alasiri natoka tena kwenda kutafuta maji ndio maana nakosa hata muda wakukaa na Watoto na kuwaandalia chakula kizuri”alisema Salome.

Amesema wakati wa mvua ndio wamekuwa wakipata nafuu kidogo kwa kuwa wamekuwa wakitumia maji ya  mtaro  pale mvua zinapokuwa zimenyesha japo maji hayo bado kiusalama hayapo vizuri na watu wengi wamekuwa wakiugua homo ya matumbo na kuharisha.

Naye mganga mfawidhi wa Zahanati ya Mwakilosa Dkt Antony Marwa amesema takwimu zinaonyesha kuwa katika wagonjwa 10 wanaofika kupatiwa matibabu katika zahanati hiyo wanane kati yao wanasumbuliwa na ugonjwa matumbo na kuhara wakiwemo Watoto wenye umri wa mwaka  02 – 15.

“Tunajaribu kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kuchemsha maji ya kunywa lakini hawafanyi hivyo Pamoja na kuwa wanachota haya maji katika vyanzo vya maji ambavyo havipo salama hivyo wagonjwa wanaougua magonjwa yanayotokana na ukosefu wa maji salama ni wengi hapa”alisema Dkt Marwa.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa mkoa wa Shinyanga Zuwena Omary amesema tayari serikali imeishatenga fedha kwaajili ya kutatua tatizo la maji katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Shinyanga.

Amesema mradi maji kutoka Ziwa Victoria tayari unawasaidia wananchi wengi hasa wale waliokaribu na bomba hilo la maji na adha ya maji waliyokuwanayo imebakia historia.


No comments