Breaking News

WATOTO WAZIPAMBA MBIO ZA ROCK CITY MARATHON

 Na Tonny Alphonce,Mwanza

Watoto wadogo wamejitokeza kwa wingi kushiriki mbio za Rock City Marathon na kuwa kivutio kikubwa kwa watu waliojitokeza kushiriki na kushuhudia mbio hizo.

Watoto hao walioshiriki mbio za kilometa 2 wengi wao walikuwa na  umri wa kuanzia miaka 03 – 12 na walionekana kufurahia mbio hizo wakiongozwa na walezi na walimu waliokuwa na jukumu la kuwapa maelekezo namna ya kushiriki mbio hizo.

Akizungumza na washiriki wa mbio hizo,Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Msala amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kushiriki michezo mbalimbali ili kujenga afya zao.

Akizungumzia ushiriki wa watoto katika mbio hizo Dc Masala amewataka wazazi na walimu kuangalia vipaji vya Watoto wanapokuwa nyumbani na shuleni na kisha kuchukua hatua za kuendeleza vipaji hivyo kama ambavyo walivyowashirikisha Watoto katika mbio hizo la Rock City.

“Serikali inaendelea kuweka mazingira Rafiki katika michezo yote ikiwemo mchezo huu wa riadha na lengo hapatunataka kuwaandaa vijana waweze kushiriki mashindano ya kitaifa na yale ya kimataifa.”alisema Dc Msala.

Kwa upande wake mzazi wa mtoto Joyce aliyeshiriki mbio hizo Martin Mahinde amesema mtoto wake anapenda mchezo wa riadha na amekuwa akimruhusu kushiriki katika mbio mbalimbali na matokeo sio mabaya kwa kuwa amekuwa hatoki katika nafasi ya kumi bora.

Mbio za Rock City Marathon hufanyika kila mwaka mkoani Mwanza ambapo mwaka huu Mtanzania Alphonse Simbu ameibuka msindi wa mbio ndefu kilometa 21.

Mbio hizo za Rock City Marathon ambazo zilidhaminiwa pia na KCB BANK zimeshirikisha wakimbiaji zaidi elfu moja wakiwemo watoto na na watu wenye Ualbino.

No comments