Breaking News

ASILIMIA 29 YA WATOTO MWANZA WANA UDUMAVU.


Na Tonny Alphonce,Mwanza

Mkoa wa Mwanza umetajwa kuwa ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa tatizo la Utampiamlo, utafiti uliofanywa (TNNS,2018) ulionyesha kiwango cha Udumavu Mkoani Mwanza ni asilimia 29 hii inamaanisha kwamba kati ya watoto 100 watoto 29 wana udumavu.

Afisa Tawala Mkoa wa Mwanza Bw Ngusa Samike 

Akizungumza katika kikao cha ufatiliaji na usimamizi wa utekelezaji wa matumizi ya vyakula vilivyoongezwa virutubisho Mashuleni Afisa Tawala mkoa wa Mwanza Bw Ngusa Samike amesema kiwango hicho ni kikubwa na kuwataka wadau wa elimu na wazazi kuweka mikakati ya kumaliza tatizo hilo.

Afisa Tawala Mkoa wa Mwanza Bw Ngusa Samike akifungua kikao cha ufatiliaji na usimamizi wa utekelezaji wa matumizi ya vyakula vilivyoongezwa virutubisho Mashuleni.

Amesema kutokana na hali hii walimu wahakikishe wanaongeza virutubishi katika unga wa Mahindi ikiwemo madini Joto,Zinki ,Madini ya Chuma na Vitamini B 12.

Amesema mkoa wa Mwanza una shule za sekondari 303, shule za bweni 50 na shule za kutwa ni 253 na shule zinazotumia vyakula vilivyoongezwa virutubishi ni 50 sawa na asilimia 16 pekee kiwango ambacho hakiridhishi.

Bwana Ngusa amesema upande wa shule za msingi,Mwanza ina shule za msingi 1019 kati ya hizo za bweni 158 na shule za kutwa ni 861 na kati ya hizo shule zinazotumia vyakula vilivyoongezwa virutubishi ni shule 158 sawa na asilimia 15.

‘Tujiulize namna gani tunaweza kuongeza jitihada za matumizi ya vyakula vyenye virutubishi,maafisa lishe mpo,maafisa elimu wilaya mpo sasa tuna kwama wapi  na mnashindwa vipi  kupita huko mashuleni kuhakikisha vyakula vinavirutubisho.alisema Ngusa.

Bw Ngusa amesema pia mkoa wa Mwanza una changamoto ya watoto wenye upungufu wa damu wenye umri wa kuanzia chini ya miaka 5 ambao ni asilimia 46 na wanawake wenye umri wa miaka 15 - 46 ni asilimia 52 ikiwa ni Zaidi ya nusu ya wanawake waliopo Mwanza.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza Dr Thomas Rutachunzibwa amewataka wanawake kubadili mtazamo na kuhakikisha anaanza kuhudhuria kliniki ndani ya miezi miwili mara baada ya kushika ujauzito ili aweze kusaidiwa namna ya ulaji wake katika kipindi chote cha ujauzito.

Mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza Dr Thomas Rutachunzibwa (kulia)akifatilia kikao cha ufatiliaji na usimamizi wa utekelezaji wa matumizi ya vyakula vilivyoongezwa virutubisho Mashuleni.

Dr Rutachunzibwa amesema wanawake wengi wamekuwa na desturi ya kuanza kuhudhuria kliniki mimba ikiwa na miezi minne hadi mitano muda ambao sio mzuri kiafya  na matokeo yake mama anaweza kujifungua mtoto mwenye kasoro kama vile kujifungua mtoto mwenye kichwa kikubwa.

‘Hii kesi ya lishe nipana na kama tunataka kuwa na watoto waliotimamu kiakili lazima mama aanze kula vyakula vyenye virutubishi katika kipindi chote cha ujauzito maana katika kipindi hiki yeye ni kiwanda hivyo tunategemea azalishe bidhaa iliyokamilika ambae ni mtoto asiye na kasoro ya ubongo na mwili’.alisema Dr Rutachunzibwa.

Nae mratibu wa lishe mkoa wa Mwanza Jovither Mwombeki amesema jukumu la mkoa kwa hivi sasa ni kuhakikisha watoto wanaoingia darasa la awali wanaanza kuangaliwa katika suala la lishe na kuwasisitiza wazazi kuchangia chakula ili wanafunzi waweze kujifunza wakiwa wameshiba.

No comments