Breaking News

MATUMIZI SAHIHI YA CHOO KINGA YA MAGONJWA YA KUAMBUKIZA KWA WATOTO.

 Na Tonny Alphonce,Mwanza

Imeelezwa kuwa kumfundisha mtoto mdogo matumizi ya sahihi ya Choo kuna msaidia mtoto kujua umuhimu wa kujistiri,usafi ,kujijali pamoja na kumkinga na magonjwa yanayosababishwa na kula kinyesi.

              Mkurugenzi wa shirika la Ladies Joint Forum (LJF) Francisca Damian.

Matumizi sahihi ya choo kwa watoto wa kuanzia umri wa miaka miwili na kuendelea kuna msaidia pia mtoto kujikinga na magonjwa ya matumbo,kipindupindu pamoja na matatizo ya macho.

Hayo yamesemwa na mkurugenzi wa shirika la Ladies Joint Forum (LJF) Francisca Damian wakati alipokuwa akizungumzia umuhimu matumizi ya Choo kwa wanafamilia.

Amesema mbali taasisi na serikali kusisitiza matumizi sahihi ya Choo lakini wazazi wanajukumu la kuwafundisha watoto umuhimu wa kunawa maji tiririka na sabuni mara baada ya kutoka Chooni.

‘Wazazi wenyewe watoto wadogo tunatakiwa kubadilika kwa sababu tukiwa na watoto mtaani au nyumbani ,mtoto akikuambia amebanwa haja unamwambia vua ujisaidie,hapo tunakosea sana mtoto anaanza kutoona umuhimu wa Choo anajua kumbe nikibanwa haja naweza kujisaidia mahali popote’.alisema Fransica.

Akizungumzia tabia ya shule na baadhi ya nyumba za ibada kutotenganisha Choo cha wanaume na wanawake,Fransca amesema ni lazima kuwa na vyoo vya jinsia zote mbili kwaajili ya Usiri na thamani ya kujenga utu kwa pande zote mbili.

‘Kuchangia vyoo kwa jinsia zote ni sababu pia ya kuibuka kwa matendo ya ulawiti na ubakaji hasa kwa Watoto,maana wakati mwingine Watoto wanajifunza vitu vibaya kwenye Televiheni kwa maana hiyo akikutana na mwenzie wa jinsia tofauti chooni wanaweza kuanza kuchezeana’.alisema Fransca.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi na Dakatari bingwa wa Watoto kutoka hospitali ya mkoa ya Souko Toure Dr Bahati Peter Msaki amesema Choo chenye familia kubwa kinatakiwa kusafishwa wakati wote kwa kutumia sabuni na dawa zingine za kuua bacteria ili kuwa kinga watoto wadogo na magonjwa mbalimbali ikiwemo UTI.

Amesema kwa familia yenye uchumi mzuri watoto wenye umri wa kuanzia miaka miwili wanatakiwa kuwa na Choo chao maalumu hadi pale wanapofikisha umri wa miaka kumi na kuendelea ndio wanarusiwa kuchangia Choo na watu wazima.

‘Kwa kuwa watanzania wengi tunakipato cha kati tunatakiwa kuzingatia suala la usafi wa Choo hata kama ni Choo cha shimo lakini kinatakiwa kuwa safi,maji yawepo pamoja na sabuni,Chooni ni eneo nyeti ambalo mtu anaweza kulitumia kupanga pia namna ya kuyaendesha maisha yake hivyo panatakiwa kuvutia na sio kuchukiza’.alisema Dr Bahati.

Salome Mkaka mkazi wa Igogo Mlimani mkoani Mwanza ameitaka serikali kuja na mradi wa kuwafungia mfumo wa maji taka ili iwasaidie kusafirisha kinyesi kutoka maeneo ya mlimani wanapoishi hadi katika mashimo maalum yatakayojengwa katika maeneo ya tambarare.

‘Sisi tunaoishi milimani tunachangamoto kubwa ya Choo kwa sababu hatuwezi kuchimba kutokana na mawe hivyo tunalazimika kuwa na Vyoo vya kujenga na matofali ambavyo vinajaa mapema na vikijaa ni ngumu kunyonya hicho kinyesi kwa gari maana haiwezi kufika mlimani na matokeo yake huwa tunasubiri wakati wa mvua tunafungulia Vyoo na kinyesi chote kuporomoka kutoka juu kuelekea chini’alisema Salome.

Kutokana na hali hiyo Salome amesema mara nyingi kuna ugomvi wa kifamilia kutokana na tabia hiyo ya kufungulia kinyesi na kinyesi hicho kutiririkia kwenye nyumba za chini na hivyo kuibua ugomvi na magonjwa ya mripuko ukiwemo ugonjwa wa matumbo ambao huwashambulia watoto mara kwa mara.


Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba watu bilioni 3.6 bado wanakosa huduma muhimu ya kujistiri na usafi  kwa kutumia Choo.


No comments