Breaking News

Polepole mguu nje, mguu ndani CCM

Ni saa 72 ngumu! Ndivyo unavyoweza kusema juu ya hatima ya Humphrey Polepole, katibu wa zamani wa Itikadi na Uenezi wa CCM, hali ambayo kutokana na mazingira yaliyopo, inaweza kuamua ama awe mguu ndani au nje ya chama hicho.

Mbunge huyo wa kuteuliwa kwa siku za karibuni ametoa kauli tata zenye tuhuma mbalimbali dhidi ya watendaji wa Serikali na makada wenzake wa CCM.

Kauli hizo zimezua mijadala mikali ndani na nje ya chama hicho, huku baadhi ya makada wenzake wakitaka achukuliwe hatua kwa kuwa anakivuruga chama na Serikali.

Mbunge huyo sasa ana uwezekano wa kukabiliwa na kibano kutoka katika vikao vya juu vya CCM vitakavyoanza kuketi leo na kuhitimishwa Desemba 18, 2021 jijini Dodoma, chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.

Polepole, aliyejipambanua ni mkosoaji wa Serikali inayoongozwa na chama chake kupitia mitandao ya kijamii, amekuwa anatoa maudhui na kuyarusha mitandaoni, ambayo vilevile yamemweka matatani.

Taarifa kwa umma ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka ilieleza kuwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa cha Jumamosi, saa 72 kutoka leo, kitatanguliwa na vikao vya Kamati Kuu na kikao cha sekreterieti ya Halmashauri Kuu.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi.

No comments