Breaking News

Imani za kishirikina chanzo cha mauaji nchini

Na Hellen Mtereko, Mwanza.

Wakati  matukio ya mauaji yakiendelea kutikisa nchini ,Mkoani Mwanza imeelezwa kuwa imani za kishirikiana na watu kutokuwa na hofu ya Mungu kumetajwa kuwa ni sababu mojawapo inayochochea matukio hayo.

Mkuu wa wilaya ya Ilemela, Hassan Masala akizungumza na askari  baadhi ya askari walioshiriki operesheni ya kuwakamata watuhumiwa wa mauaji ya wanawake

Hayo yamebainika wakati wa hafla ya kuwatunuku zawadi na vyeti baadhi ya askari walioshiriki operesheni ya kuwakamata watuhumiwa wa mauaji ya wanawake watatu waliouawa kwa kukatwa mapanga na kisha miili yao kutupwa kwenye bonde la Mto wilayani ilemela usiku wa kuamakia Januari 19 mwaka huu.

Wakizungumza kwenye hafla hiyo baadhi ya watetezi wa haki za binadamu na viongozi wa dini licha ya kulipongeza jeshi la Polisi kwa hatua mbalimbali linazochukua katika kukabiliana na uharifu wametaja baadhi ya sababu za mauaji hayo ni pamoja na umasikini na imani za kishirikina.

“Kwa mfano tukio la kuuawa kwa dereva tax wilayani Sengerema watuhumiwa walikamatwa wakiwa kwa mganga wa Kienyeji ,hiyo ni dalili kwamba nguvu za giza zimekuwa zikiamini kwenye matukio haya,”amesema Flora Lauwo Mtetezi haki za binadamu.

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke  amesema njia pekee inayoweza kubadirisha mtazamo wa raia ,kupunguza matukio ya mauaji na kuimarisha hali ya amani nchini ni pamoja na jamii  kuwa na  hofu ya Mungu.

“Tunaomba vyombo vya habari vitoe nafasi kwa viongozi wa dini ili waweze kutoa elimu na kuzifinyanga nafsi ili ziachane na imani potofu na wamrejee kwa Mungu wao,” amesema Sheikh Kabeke.

Hata hivyo jeshi la polisi mkoani Mwanza limesema halitasita kuwachukulia hatua wahalifu wote wanaojichukulia sheria mkononi ikiwa ni pamoja na kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazowakabili.

Mkuu wa wilaya ya Ilemela, Hassan Masala akimkabidhi cheti  mmoja wa askari  walioshiriki operesheni ya kuwakamata watuhumiwa wa mauaji.

Kamanda wa polisi, Ramadhan Ng’anzi amesema jeshi hilo lipo tayari kuwatumikia wananchi kwa moyo uliotukuka na watafanya kazi kwa kuhakikisha raia na mali zao zinakuwa salama.

“Tutafanya kazi muda wowote kuwatumikia wananchi wa Mwanza na kipaumbele chetu cha kwanza ni kuona matukio yote ya uharifu  hayatokei iwe ni nchi kavu, majini  au angani mahali popote polisi watafika na kiapo chetu ni kilekile kuwa hatutamuonea mtu wala kumpendelea mtu,” amesema Kamanda Ng’anziKamanda huyo ametoa tahadhari kwa wahalifu kuwa Mwanza hawana nafasi wataingia lakini hawatatoka salama huku akiwahakikishia wananchi kuwa jeshi limejipanga kutokomeza uhalifu wa aina yoyote.

Akizungumza baada ya kukabidhi vyeti hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa wilaya ya Ilemela, Hassan Masala amesema uongozi wa mkoa uko tayari kutoa ushirikiano wowote kwa jeshi la polisi watakaouhitaji.

Masalla amesema anatambua jitihada kubwa zinazofanywa na jeshi hilo katika kuwalinda raia wake huku akiwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuwabaini wahalifu.

“Naomba niwahakikishie kwamba jiji la Mwanza liko salama na niwatoe hofu watu wote wanaotaka kuja kuwekeza katika jiji hili kuwa ulinzi na usalama umeimarishwa,” amesema Masalla

Mwisho 

No comments