VIFO VYA KINA MAMA WAJAWAZITO NA WATOTO BADO TATIZO MWANZA RC ATAKA KILA MMOJA AWAJIBIKE.
Na Tonny Alphonce,Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel
amewataka wananchi na wadau wa afya kufanya mageuzi makubwa ya kimaisha na kimatibabu
ili kupunguza vifo vya mama na mtoto ambavyo bado ni tatizo kubwa mkoani
Mwanza.
Amesema takwimu zinaonyesha mwaka 2020 kina mama 157
walifariki dunia wakati wa kujifungua,wakati mwaka 2021 kina mama 164
walifariki dunia na mwaka 2021 watoto wachanga 669 walifariki dunia hali ambayo
sio nzuri.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa makabidhiano ya Zahanati
Lumala Magharibi iliyopo wilayani Ilemela Mkoani Mwanza ambapo kitatoa huduma
kwa wakazi wa kata ya Ilemela na wananchi wa kata za Jirani.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa Zahanati hiyo
Mhandisi Gabriel amewataka wananchi na madaktari kushirikiana pamoja hasa kwa
kina mama wajawazito ili waweze kujifungua salama na kupunguza vifo vya kina
mama na Watoto.
‘Ndugu zangu Mama mjamzito anatakiwa kuripoti
kwenye kituo cha afya mara baada ya kugundua kuwa anaujauzito ili aweze
kuandikishwa na kupimwa afya yake hii itamsaidia mama kusafiri salama katika safari yake ya ujauzito hayo yote kwa
pamoja yakifanyika yatamuhakikishia mama usalama wake pamoja na mtoto.alisema Mhandisi
Gabriel.’
Mhandisi Gabriel amesema kwa upande wa serikali ya mkoa tayari hatua mbalimbali zimeisha chukuliwa ikiwemo kuhakikisha ujenzi wa vituo vya afya na Zahanati vinaendelea,Elimu ya uzazi salama imekuwa ikitolewa pamoja na kutekeleza mipango mbalimbali ya kitaifa ukiwemo mpango Jumuishi wa Taifa wa Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto ambao unagusia pia afya ya mama na mtoto.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Ilemela Hassan Masala
amesema maboresho yote ya afya yanayofanywa na serikali mnufaika wa kwanza huwa
ni mama na mtoto na amemshukuru Rais kwa kuendelea kutoa fedha za ujenzi wa
vituo vya afya.
‘Niombe kina mama mtumie sasa Zahanati hii pale
mnapopata matatizo mbalimbali ya kiafya,msikimbilie hospitali ya mkoa au
Bugando kule nendeni tatizo linapokuwa kubwa tena kwa maelekezo ya madaktari
wenu wa hapa nasema hivyo ili hospitali ya mkoa na Bugando wapumue huko waende
wale watakaokuwa mahututi.alisema Masala’
Akitoa taarifa ya ujenzi wa Zahanati hiyo kaimu Mkurugenzi
wa Manispaa ya Ilemela Mofen Mwakatonga amesema jumla ya shilingi milioni 152
na laki 2 zimetumika kukamilisha ujenzi wa Zahanati hiyo ambayo itawasaidia
wananchi wa mitaa ya Lumala,Masemele na Nyamadoke watapata huduma katika umbali
mfupi na hatimaye kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Naye mmoja wananchi waliofika katika kushuhudia makabidhiano
hayo Rose Mushi amesema kuanza kufanyakazi kwa Zahanati hiyo kutawasaidia kina
mama wengi wenye ujauzito na wenye Watoto wadogo kupata huduma kwa wakati.
Rose amesema pamoja na kuanza kufanyakazi kwa Zahanati
hiyo bado serikali inatakiwa kuhakikisha wahudumu wa afya wanakuwepo pamoja na
kuanzisha huduma nyingine za upasuaji.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imeendelea
kukamilisha ujenzi wa Zahananti mpya
tatu zilizoanzishwa kwa nguvu za wananchi,ujenzi wa Zahanati ya Lumala Magharibi
ulianza rasimi mwaka 2018 na kukamilika mwaka 2022.
Mpango huu wa kuboresha huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini unaendana na lengo la Programu Jumuishi Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto katika kupunguza idadi kubwa ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano.
No comments