WADAU WA ELIMU NA WAZAZI WATAKIWA KUWEKEZA KATIKA ZANA CHANGAMSHI ZA WATOTO.
Na Tonny Alphonce,Mwanza
Wazazi na Serikali wametakiwa kuwekeza katika eneo la Uchangamshi
kwa Watoto wadogo ili iwasaidie Watoto katika makuzi yao na kupata uelewa wa
haraka katika mambo mbalimbali.
Kimsingi Watoto wadogo wanahitaji Uchangamshi na hivyo
wanahitaji zana zitakazowasaidia katika kujifunza kwa haraka tofauti na mtoto
ambae hatapitishwa katika eneo hili la Uchangamshi.
Kauli hiyo imetolewa na Mwl Alex Rwabigene ambapo amesisitiza
suala la ubunifu wa Zana za kufundishia wasiachiwe walimu peke yao kwa kuwa
suala la ubunifu ni zaidi ya suala la maelekezo na linatakiwa kutoka ndani ya
moyo mwalimu husika.
‘tunachotakiwa kufanya sasa ni kuwatambua wabunifu wa zana hizi za Watoto ili wasaidie ubunifu wao uwasaidie walimu ambao sio wabunifu ili kuwa na zana muhimu za kuamsha uchangamshi kwa Watoto kwa kuwa tunaamini mazingira mazuri ya mtoto katika makuzi yake ya utoto ni muhimu sana na yanahusika kumfanya nani baadae.alisema Mwl Rwabigene.
Akizungumzia nafasi yake kama mbunifu wa zana za
kufundishia Watoto, Mwl Rwabigene amesema kwa sasa Zana zao zimekuwa msaada mkubwa kwa
baadhi ya shule na wazazi ambao wameanza kuzitumia na kupata matokeo mazuri.
‘Baadaya kuhangaika kwa muda mrefu kuielimisha
jamii juu ya umuhimu wa Zana za kufundishia,sasa Zana zetu zimesambaa sana na
ni baada ya serikali kuona umuhimu wetu katika eneo hili la Uchangamshi kwa
Watoto na zana zetu zimesambaa katika maeneo mbalimbali kama
Kagera,Tabora,Kigoma,Dar es Salaam na maeneo mengine wamekuwa wanaomba tuwatumie
na wamekuwa wakikiri kuwa zana zetu zinawasaidia.Alisema Mwl Rwabigene.’
Akizungumzia mpango Jumuishi
wa Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto (MMMAM) Mwl Alex amesema mpango
huo wa serikali kupitia Wizara ya Afya ni mkubwa na serikali imeonyesha dhamila
ya dhati katika kulisukuma suala hili la kuwajengea msingi wa malezi Watoto
kuanzia umri wa mwaka 0 hadi 8.
‘Malezi Jumuishi ya mtoto yana mambo mengi kuna
habari ya Afya,Kuna habari ya Lishe,kuna habari Mahusiano,Malezi yao lakini pia
kuna eneo la Uchangamshi na mpango huu umelibeba katika uzima wake kwamba
Watoto wapate kutenda matendo,wapate kuchangamshwa wakianza katika umri
mdogo,mambo yote hayo ndio yanamjengea hisia na kumfanya ukubwani kuwa mtu
maalumu.alisema Mwl Rwabigene”
Bosco Bosco ambae ni mwanasaikolojia amesema suala la Uchangamshi kwa mtoto linaanzia pale mtoto anapokuwa tumboni ,hasa kipindi ambacho mtoto anaanza kucheza tumboni katika hatua hiyo anakuwa na uwezo wa kusikia na katika kipindi hicho baba na mama wanaweza kuanza kuongea na mtoto.
‘Wazazi wengi wanafanya makosa hawana tabia ya
kuongea na mtoto akiwa tumboni na hata baada ya kuzaliwa,wengine wanadhani
mtoto wa mwaka sifuri au miezi mitatu au mwaka mmoja haelewi ukimsemesha,sio
kweli kitendo cha kumzungumza nae kinamfanya awe na hisia na uchangamfu kitu
ambacho ni kikubwa sana katika ukuaji wa mtoto.alisema Bosco.’
Bosco amesema kitendo cha mlezi kutozungumza na mtoto au kuto kucheza nae kunaathiri ubongo wa mtoto kuchelewa kuku ana kutokuwa na uwezo wa kufikiri na kuchanganua mambo hata anapokuwa mkubwa.
Kwa upande wa Zana za kujifunzia Watoto Bw Bosco
amesema mzazi anaweza kutumia vitu mbalimbali kama makopo,magome ya miti na
vitu vingine ambavyo haviwezi kuleta madhara kwa mtoto na kwaajili ya kuchezea
ambapo husaidia ubongo wa mtoto kuchangamka.
Mzazi Fredy Kabamba ambae ni mkazi Swea jijini Mwanza
ambae ni mmoja wa wazazi ambaye amenunua Zana kwaajili ya mtoto wake mwenye
umri wa miaka miwili na nusu amesema
zana hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa Mtoto wake pamoja na mfanyakazi wake wa
ndani kwa kuwa muda wote wamekuwa wakichezea zana hizo ambazo bila wao kujua
zimekuwa zikijenga pia kiakili.
‘Mimi nilinunua zana za shilingi laki moja na
nusu na nilivutiwa baada ya kupewa elimu kidogo na mwl Alex juu ya umuhimu wa
Zana hizi kwa mtoto hasa katika eneo la Uchangamshi,dada wa kazi na mtoto wangu
wamezipenda muda mwingi wamekuwa wakitumia kuunganisha maumbo mbalimbali pamoja
na kupanga herufi na namba kwa usahihi,nimeona hata dada wa kazi imemsaidia
maana hakubahatika kusoma kwa maana hiyo zana hizi zinamsaidia mtoto wangu na
dada wa kazi.alisema Fredy’
Wadau mbalimbali bado wana nafasi ya kushirikiana na serikali
katika kutekeleza mpango wa MMMAM kama ilivyo kwa SHIRIKA linaloangazia Malezi
,Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto (CiC ) ambalo kwa upande wake limefanikiwa
kuongeza uwezo kwa walimu wa awali katika wilaya za Kongwa na Chamwino mkoani
Dodoma kumudu mbinu za ujifunzaji na ufundishaji wa Elimu ya awali kutoka
asilimia 50 Aprili, 2020 hadi kufikia asilimia 70 Disemba, 2020.
Nao Mwongozo wa Mwalimu wa kufundishia Elimu ya Awali
unamuelekeza mwalimu umuhimu
utakaomsaidia kuboresha mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji wa umahiri
uliobainishwa katika mtaala na muhtasari wa Elimu ya Awali. Mwongozo huo
umebainisha shughuli za kutenda mtoto ambazo zitamwezesha kujenga umahiri
husika.
No comments