Breaking News

WADAU WA UVUVI BUSEKERA WAUPOKEA MRADI WA KUZUIA VIFO VYA WAVUVI KWA FURAHA

 Na Tonny Alphonce,Busekera Mara

Wadau,Wamiliki wa Mitumbwi na wavuvi wa Kijiji cha Busekela wilayani Bunda mkoani Mara wameahidi kuchukua tahadhari za kiusalama wanapokuwa katika shughuli zao za  Uvuvi ili kupunguza ajali za majini na vifo vinavyoweza kuzuilika.

Wametoa kauli hiyo wakati wa utambulisho wa mradi wa kupunguza vifo vya wavuvi vinavyotokana na kuzama maji katika Ziwa Victoria unaofadhiriwa na shirika Royal National Lifeboat Institution (RNLI) kuroka wingereza na kutekelezwa na shirika la usimamizi wa mazingira na maendeleo (EMEDO) uliofanyikia leo  katika mwalo wa Busekera.

Akizungumza wakati wa utambulisho wa  mradi huo Diwani wa kata ya Bakumi,Munubi Mussa amelipongeza shirika hilo la EMEDO kwa kuwapelekea mradi huo ambao utawasaidia wavuvi waweze kufanya shughuli zao katika hali ya usalama.

‘Kumekuwa na matukio ya kuzama mara kwa mara na kupoteza wavuvi na mali kwa hiyo kwenye mradi huu wananchi sasa wanapewa uelewa wa namna gani waweze kukabiliana na mazingira yao’.alisema Diwani Mussa.

Zawadi Song’ola ambae ni mmiliki wa Mitumbwi amesema wamekuwa wakichukua taadhari kabla ya kuingia majini lakini kupitia mradi wa huu wa kuzuia ajali ya majini kuna haja ya kuongeza vifaa vya uokozi katika mitumbwi.

Kwa upande wake meneja Mradi wa kutoka EMEDO Arthur Mugema amesema mradi huo utashirikiana na makundi mbalimbali yanayohusiana na uvuvi wakiwemo viongozi wa BMU kwa lengo la kuwa jengea uwezo wa kiongozi na kifedha ili waweze kutatua kero mbalimbali za wavuvi.

‘Mradi huu ni wenu,sisi EMEDO ni wasimamizi tu kwa maaana hiyo tutawashirikisha katika kila hatua na  hata miaka 3 itakapopita basi mradi huu uweze kuendelea bila tatizo lolote na hata wadau watakapohitajika lazima kwanza tuanze na wenyeji’.alisema Mugema.

Nae mkurugenzi wa shirika la EMEDO Editrudith Lukanga amesema hatua ambazo wameanza kuzichukua wadau wa uvuvi katika Kijiji cha Busekela zitapewa nguvu na mradi huo ambao lengo lake ni kupunguza vifo  vya wavuvi vinavyotokana na kuzama maji


Amesema pamoja na mambo mengine lakini elimu itatolewa juu ya namna ya kujikinga na ajali za majini ambapo wataalamu watatoa mafunzo ya kuogolea,namna ya kujiokoa na kuokoa wengine ajali inapotokea pamoja na kutumia vifaa vya kujikinga kuzama.

Shirika la EMEDO hadi sasa limeutambulisha mradi wa huo  katika ngazi ya Wilaya na sasa mradi umeanza kutambulishwa katika ngazi ya jamii ambako ndiyo utekelezaji wake utafanyika kwa kushirikisha jamii husika.

No comments