Breaking News

ASILIMIA 75 YA WATOTO WANAOZALIWA UTUMBO UKIWA NJE HUFARIKI DUNIA

 

Na Tonny Alphonce, Mwanza

Imeelezwa kuwa asilimia 75 ya watoto wanaozaliwa wakiwa utumbo nje hufariki dunia kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo watoto hao kucheleweshwa hospitali pamoja na kutopatiwa tiba stahiki.

Akizungumzia tatizo hilo mkurugenzi mkuu wa hospitali ya Bugando Fabian Masaga amesema tangu Bugando ianze kutoa matibabu ya watoto wanaozaliwa utumbo nje ni asilimia 15 tu ya watoto wanaopokelewa katikati hospitali ya Bugando hutibiwa na kupona huku asilimia 75 hufariki dunia.

‘Tunaposema asilimia 15 ni ndogo kwasababu ile asilimia 75 ya hawa watoto tunawapoteza kwa kweli ni uchungu kama ambavyo tulivyoona baadhi ya kina mama hapa wakiongea kwa uchungu wakati wa kutoa shuhuda’.alisema Masaga.

Masaga amesema yawezekana baadhi ya watu wasijue ukubwa wa ugojwa huo lakini kiuhalisia mtoto huzaliwa sehemu ya tumbo ya juu kwenye kitovu ikiwa wazi huku ngozi yote huwa haipo na utumbo wote hutoka nje hali ambayo inatisha na endapo mtoto atacheleweshewa matibabu ni wazi kuwa anaweza kufariki dunia.


Mkurugenzi mkuu wa hospitali ya Bugando Fabian Masaga akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya watoto wanaozaliwa utumbo nje.

Masaga amesema takwimu za kidunia zinaonyesha kuwa kati ya watoto 4000 wanaozaliwa mmoja hukutwa na tatizo hilo na kwa Bugando takwimu zinaonyesha kwa wastani kwa mwaka mzima wanapokea watoto 290  sawa na watoto 10 kwa mwezi huku kwa wiki ni sawa na watoto watatu hadi watano wanapokelewa  hali ambayo inaashiria tatizo hili ni kubwa.

Kwa upande wake Daktari Sister Alicia Masinga kutoka kitengo cha upasuaji wa watoto Bugando amesema ili kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa wakiwa na utumbo nje wamama wajawazito  walio chini ya umri wa miaka 25 wanatakiwa kufanya kipimo cha Utra Sound kwasababu katika umri huo kuna uwezekano wa wao kuzaa mtoto mwenye changamoto hiyo.


Daktari Sister Alicia Masinga kutoka kitengo cha upasuaji wa watoto akizungumzia namna ya kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa wakiwa na utumbo nje.

Sister Masinga amesema hatua nyingine kwa mama endapo atagundulika kuwa na mtoto mwenye utumbo nje anatakiwa kujifungulia katika hospitali inayotoa huduma ya watoto hao kwasababu matibabu huanza mara moja baada ya mtoto kuzaliwa ili kuokoa maisha ya mtoto na kuongeza kuwa kwa sasa hospitali zinazotoa huduma hiyo kwa sasa ni Bugando na Muhimbili.

‘Ukiangalia sababu zisizo rasimi za tatizo hili inawezekana likawa linasababishwa na mabinti wanashika ujauzito wakiwa na umri mdogo kwa sababu tafiti zimewabaini wanaojifungua watoto wakiwa utumbo nje wengi wao umri wao ni chini ya miaka 25’.alisema Sister Msinga

Akizungumzia majukumu wanayotakiwa kufanya wahudumu wa afya mara baada ya kuwapata watoto waliozaliwa utumbo nje sister Masinga amesema ni vema wakawasiliana na hospitali ya Bugando au Muhimbili ili wapewa maelekezo ya namna gani ya kuwapa huduma ya kwanza watoto hao itakayowawezesha kufika salama Bugando au Muhimbili kwaajili ya matibabu.

‘Wakiapata huduma ya kwanza inayopaswa hata wakicheleweshwa inasaidia hawa watoto kufika Bugando wakiwa na hali nzuri na watapatiwa matibabu na kuokoa maisha yao’.alisema Sister Masinga

Jesca James kutoka mkoani Geita ambae alijifungua mtoto ambae utumbo ukiwa nje anasema alijisikia vibaya mara baada ya kujifungua na kugundua kuwa mtoto wake anashida hiyo lakini mtoto alipatiwa matibabu na kupona baada ya miezi miwili.

Jesca amesema majirani baada ya kugundua kuwa amejifungua mtoto akiwa na utumbo nje walimkatisha tamaa kwa kusema kuwa mtoto huyo lazima atakufa lakini hakukata tamaa na kumpeleka Bugando kwa matibabu na akapona.

Naye Reticia Adam kutoka mkoani Kagera amesema alipojifungua mtoto mwenye tatizo hilo la utumbo wazi lilimshangaza hadi daktari aliyemzalisha kwasababu ilikuwa ni mara yake ya kwanza kushuhudia mama akijifungua mtoto mwenye tatizo hilo.

‘Baada ya daktari kuona mtoto wangu utumbo upo nje alishangaa na haraka akanipa rufaa ya kwenda Bugando kwa matibabu zaidi japo baba mkwe wake alishauri tusiahangaike kwenda Bugando kwa kuwa mtoto angefariki kitu ambacho hakikuwa cha kweli kwakuwa tulipata matibabu na mtoto akapona kabisa’.alisema Reticia.

Nao wadau wa Afya Judith Nashon mwanasheria  kutoka shirika la Railway Children Afrika na mkurugenzi wa Desk and Chair Foundation Sibtain Meghji wamesema wataendelea kutoa msaada kwa hospitali ya Bugando pale watakapo lazimika kufanya hivyo kwa lengo la kuokoa maisha ya watoto wanaokumbwa na changamoto mbalimbali za afya.


Mwanasheria  kutoka shirika la Railway Children Afrika Judith Nashon akizungumza namna shirika lao linavyoshirikiana na hospitali ya Bugando katika masuala ya afya kwa watoto.

Hadi hivi sasa bado haifahamiki sababu hasa za mama kujifungua mtoto utumbo ukiwa nje japo tafiti mbalimbali bado zinaendelea kufanyika huku hospitali ya rufaa ya Bugando kupitia chuo chake cha afya nayo ikijipanga kuanza kufanya utafiti ili kujua chanzo cha tatizo hilo la mtoto kuzaliwa akiwa utumbo nje.


No comments