Breaking News

SARATANI YA MACHO YATAJWA KUWA TISHIO KWA WATOTO

 

Na Tonny Alphonce,Mwanza

Saratani ya macho kwa watoto wenye umri wa miaka 2-8 imetajwa kuwa miongoni mwa saratani ambazo ni tishio kwa watoto wadogo hapa nchini.

Daktari  bingwa  wa  macho  kwa watoto kutoka hospitali ya kanda ya rufaa Bugando Evarista Mgaya aliyesema hayo wakati wa  kampeni ya kuhamasisha na kujenga  uelewa juu ya saratani kwa watoto iliyofanyika  katika hospitali ya wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Daktari Mgaya amesema kuwa changamoto kubwa iliyopo kwenye jamii ni wazazi walio wengi kuwachelewesha watoto kupata matibabu jambo ambalo hupelekea macho ya mtoto kufa na wakati mwingine husababisha kifo kwa mtoto.

Daktari Mgaya amesema watoto hawakosi changamoto za Saratani kama ilivyo kwa rika zingine ambapo kwa mwaka 2022 kwa hospitali ya Bugando pekee walipokea watoto  67 na kati ya hao watoto 30 walikuwa watoto wapya wenye Saratani ya macho na kati yao zaidi ya asilimia 50 hufariki dunia.

“Unaweza kujiuliza kwanini watoto hawa hufariki dunia! watoto wengi wenye saratani ya macho wanafikishwa hospitali wakiwa wamechelewa,wanafikishwa hospitali saratani ikiwa imefika mbali sana”.alisema daktari Mgaya.

Akizungumzia dalili za ugonjwa wa Saratani ya macho daktari Mgaya amesema saratani ya macho ina dalili kama za mtoto wa jicho ambapo katikati ya jicho kunakuwa na kitu cheupe badala ya rangi nyeusi.

“Unaweza ukagundua kama mtoto wako anaugonjwa wa saratani kwa kumpima kwenye mwanga hafifu unaweza kuona jicho la mtoto wako linang’aa kama jicho la Paka lakini pia kuna watoto wengine hupata makengeza ukiona hivyo wewe kama mlezi mlete mtoto wako apatiwe matibabu”.alisema Mgaya

Daktari Mgaya amesema endapo mzazi atamfikisha mapema mtoto wake hospitali mapema anaweza kutibiwa na kupona na akawataka wazazi kujenga tabia ya kupima afya za watoto wao mara kwa mara kwa lengo kuangalia maendeleo ya afya zao.

Kwa upande wa mratibu wa kampeni ya kuhamasisha na kujenga uelewa juu ya saratani kwa watoto kutoka hospitali ya kanda ya rufaa ya Bugando na daktari bingwa na mbobezi wa saratani kwa watoto daktari Heronima Kashaigili amesema kuwa suala la wazazi kupata uelewa juu ya ugonjwa wa saratani husaidia kurahisisha matibabu kwa watoto.

Daktari Kashaigili amesema wazazi wakielewa kuhusiana na saratani na dalali zake itawasaidia kazi madaktari kwa asilimia 50 kwasababu watakuwa wamechangia asilimia 50 ya matibabu ya mtoto na kupona.

Daktari Kashaigili amesema saratani za watoto zipo za aina mbalimbali na katika kupatiwa matibabu hupatiwa ya aina tatu,matibabu ya kemikali,matibabu ya mionzi au matibabu ya upasuaji au akahitaji matibabu yote ya aina tatu inategemea na saratani imefikia katika hatua ipi.

Amesema kwa nchi zinazoendelea takwimu za kitabibu za kidunia zinaonyesha kuwa saratani za watoto zinatibika kwa zaidi ya asilimia 85 huku hapa nchini saratani za watoto zinatibiwa chini ya asilimia 20 na watoto wenye saratani karibia asilimia 80 hufariki dunia.

Jenita Octavian mwenyeji wa Kigoma ambae kwa sasa anaishi mkoani Mwanza amesema mtoto wake alianza kuvimba tumbo akampeleka hospitali akaambiwa ana UTI na wengine walimwambia amerogwa ila baadae madaktari wa wilaya wakamshauri ampeleke mtoto Bugando ambapo alipimwa na kukutwa na saratani ya figo na  alipatiwa matibabu na kupona.

Saratani ni ugonjwa ambao unaathiri watu wa rika na jinsia zote watoto, watu wazima, wanawake na wanaume ambapo takwimu za Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (IARC) na Shirika la Afya Duniani (WHO), 2018 zinaeleza kwamba kila mwaka duniani kote kunatokea wagonjwa wapya wanaokadiriwa kufikia milioni 18.1, na kati ya hao, zaidi ya wagonjwa milioni 9.6 hufariki kutokana na ugonjwa wa saratani kila mwaka ambao ni sawa na takribani asilimia 50.

kampeni ya wiki ya  kuhamasisha na kujenga uelewa juu ya saratani kwa watoto hufanyika kila mwaka septemba  mosi mpaka septemba 30 na mwaka huu imebeba kauli mbiu isemayo  kila mtoto  mwenyewe saratani anastahili  fursa ya tiba.

No comments