Breaking News

WAZAZI WATAKIWA KUZINGATIA MAHITAJI YA AFYA YA MTOTO ILI KUMKINGA NA ULEMAVU

 

Na Tonny Alphonce,Mwanza

Wazazi wametakiwa kuzingatia mahitaji ya kiafya ya mtoto kuanzia kipindi cha ujauzito ili kumkinga na magonjwa ambayo yanaweza kumsababishia kifo au ulemavu katika makuzi yake.

Afisa  program wa Children In Crossfire (CIC) Isack Idama amesema hayo alipokuwa akizungumzia namna ambavyo  program jumuishi ya taifa ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto inavyowagusa watoto wenye ulemavu katika makuzi yao.

Akitoa mfano Isack amesema  mtoto anapokosa chanjo muhimu za magonjwa mbalimbali mara baada ya kuzaliwa  anaweza kushambuliwa na magonjwa kama Polio,Pepopunda,Kifadulo  na magonjwa mengine ambayo  hupelekea mtoto kupata ulemavu.

Aidha amewataka wazazi   kuwa na utaratibu wa kuwakagua watoto ili kujua iwapo  mtoto ana ulemavu hususani milango  mitano ya fahamu kabla ya kuwa mtu mzima ili waweze kupatiwa matibu kulingana na uhitaji wao.

“Inatakiwa mzazi ujue  iwapo mtoto wako anasikia vizuri,anaona vizuri anatofautisha harufu nzuri na mbaya lakini pia ujue iwapo mtoto wako anauwezo wa kutofautisha ladha mbalimbali mambo ambayo wengi wetu hatufanyi”.alisema Idama

Amesema mtoto akigundulika  na ulemavu mapema atapatiwa afua mbalimbali kama mazoezi tiba,upasuaji pamoja na elimu inayoendana na ulemavu wake ambayo itamsaidia mtoto mwenye ulemavu kupata kazi na kujitegemea.

“Kwa hiyo tunasema kwamba afya bora inajumuisha chanjo kwa mama mjamzito chanjo kwa mtoto kwa hiyo tuepuke ulemavu usio wa lazima vile vile tunasisitiza jamii ihakikishe kwamba afya ya mtoto na afya ya mama mjamzito inazingatiwa”.alisema Idama

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana akizungumzia ukuaji wa mtoto amesema binadamu huanza kujengeka anapokuwa na umri wa  miaka 0-8 ambao  ndio umri muhimu  kwa wazazi na walezi kuwekeza kwa watoto  kwa manufaa ya familia na taifa kwa ujumla.

Elikana amesema serikali inatambua umuhimu wa kuwekeza katika afya na lishe kwa maendeleo ya mtoto kwa kuwa lishe duni huzalisha magonjwa kama udumavu na lishe bora humjengea kinga mtoto na kuwa na afya njema na kupelekea ukuaji mzuri wa mwili.

Lucy Michael mkazi wa Mabatini Jijini Mwanza ambae anaishi na mtoto aliyepata ulemavu miezi michache mara baada ya kujifungua anasema hakujua kama kama mtoto wake ni mlemavu hadi pale alipoambaiwa na jirani yake kuwa mtoto wake hayupo sawa.

“Hii ilikuwa mimba yangu ya kwanza kwa hiyo vitu vingi nilikuwa sijui siku moja jirani yangu alikuja nyumbani alipomuangalia mtoto wangu akaniambia mbona mtoto wako hajaanza kukaa na viungo vyake mbona havipo sawa? hapo ndio nikagundua mtoto wangu hayupo sawa”.alisema Lucy

Lucy anasema mtoto wake alidumaa hakuongezeka kimwili na hakuwa na uwezo wa kukaa wala kuongea muda wote alikuwa analala na alipompeleka hospitali aliambiwa mtoto wake ana utindio wa ubongo hivyo ajaribu kumfanyisha mazoezi pamoja na kumchua hata hivyo mambo hayakubadilika.

“Mimi wakati nilipopata ujauzito sikujua hadi ujauzito ulipofikisha miezi mitatu ndio nilijitambua na hakuna dawa yoyote niliyokunywa na sikuwa naenda kliniki hadi nilipokaribia kujifungua ndio nilianza kwenda hospitali labda ndio maana mtoto wangu alipata alipata ulemavu”.alisema Lucy

Getrude John Ndalifashe Mkunga na mtaalamu wa masuala ya mama,uzazi na mtoto kutoka shirika la Uzao Wetu amesema sababu za mtoto kuzaliwa akiwa na ulemavu au mtindio wa ubongo mara baada ya kuzaliwa inaweza kusababishwa na vitu vingi kama vile mama kutotumia vidonge vya folic Acid wakati wa ujauzito,mtoto kutokulia wakati wa kuzaliwa pamoja na ubongo wa mtoto kutikisika wakati wa kuzaliwa kutokana na sababu mbalimbali. 

"Mtoto anaweza kudondoka na kutikisa ubungo wakati wa kuzaliwa na mara nyingi hutokea mama anapojifungulia nyumbani lakini pia mtoto kubanwa kichwa wakati wa kuzaliwa na mtoto kunywa maji ya uzazi wakati wa kuzaliwa haya yote yanaweza kuleta dosari za ukuaji kwa mtoto na hata kusababisha ulemavu".alisema Getrude

Akizungumzia umuhimu wa chanjo mara baada ya mtoto kuzaliwa Getrude amesema chanjo huokoa maisha ya hadi milioni 3 kila mwaka hivyo  ni muhimu mtoto kuchanjwa chanjo mbalimbali ili kumkinga mtoto na maradhi,ulemavu na vifo vitokanavyo na magonjwa yanayozuilika kama Polio,Surua,Homa ya ini,Dondakoo,Kifadulo,Nimonia,kuhara kunakosababishwa na virusi vya rota,Rubela na Pepopunda. 

"Kuna mambo mengi ya kuangalia mara baada ya mtoto kuzaliwa,huwa tunaangalia rangi,tunaangalia kama mtoto amelia,tunaangalia pia kama mtoto amepata maambukizi kwenye kitovu wakati wa kuzaliwa tofauti yoyote inaweza kusababisha tofauti katika ukuaji wake".alisema Getrude

Getrude amesema kila chanjo inaumuhimu kwa mtoto na endapo mtoto asipopatiwa chanjo lazima ataathirika kwa mfano asipopata chanjo ya Surua mtoto atapata utapiamlo,udhaifu wa maendeleo ya ubongo na huweza kumfanya mtoto kuwa kiziwi au kipofu.

Tafiti katika kanda ya ziwa zinaonyesha kuwa watoto wenye ulemavu na wale wenye ualbino wanachangamoto kubwa katika kupata elimu na huduma za afya,pia wanakabiliwa na ukatili na kuishi katika hali ya umaskini.


No comments