Breaking News

ILEMELA YAENDELEA KUTENGA FEDHA ZA LISHE KWAAJILI YA WATOTO

 

Na Tonny Alphonce,Mwanza

Mwaka wa fedha 2022/2023 halmashauri ya wilaya ya Ilemela jijini Mwanza kupitia idara ya afya ilitenga kiasi cha shilingi milioni 85.8 kutoka mapato ya ndani kwaajili  ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ili waweze kupata lishe.

katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2022/2023 Januari – Machi utekelezaji wa shughuli za lishe katika halmashauri ya Ilemela ulifikia asilimia 77.5

Taarifa hiyo  ya utekelezaji wa shughuli za lishe katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2022/23 ulilenga kutekeleza shughuli mbalimbali ambazo ni kutoa elimu ya lishe kwa wazazi/walezi katika kata tatu za Nyamhongolo, Bugogwa na Ilemela, usimamizi shirikishi pamoja na uhakiki wa ubora wa takwimu za viashiria vya lishe kwa vituo vya kutolea huduma za afya ya mama na mtoto, ununuzi wa chakula dawa kwa ajili ya kutibu watoto wenye umri chini ya miaka 5 wenye utapiamlo pamoja na shughuli nyingine.

Jitihada hizo za kutokomeza Utapiamlo zimeendelea ambapo tarehe 13/10/2023 halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kupitia kitengo cha lishe imeanzisha zoezi la ugawaji wa chakula lishe kwa watoto wenye utapiamlo mkali katika mitaa yote 171 inayounda Manispaa hiyo.

Sehemu ya vyakula lishe kwaajili ya watoto wenye utapiamlo mkali vilivyogawiwa  katika mitaa yote 171 inayounda Manispaa hiyo.

Katika zoezi hilo la ugawaji wa chakula lishe kwa watoto wanaoishi katika Manispaa ya Ilemela lililongozwa na Bi Mariam Msengi ambae ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela katika Kituo cha Afya cha Buswelu amesema  kuwa Manispaa ya Ilemela inaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita za uboreshaji wa  huduma za lishe kwa kutoa fedha katika sekta hiyo kwa kutambua umuhimu wa wananchi wote kuwa na lishe bora tangu wakiwa wadogo ili kuwa na nguvu kazi imara katika ujenzi wa taifa.

Mmoja wa wananchi wa wilaya ya Ilemela akipokea chakula lishe kwaajili ya watoto.

Bi Mariam, amewapongeza pia wanaume wenye watoto waliofika katika kituo cha afya Buswelu kwa ajili ya kupata huduma za kliniki pamoja na kusikiliza elimu ya lishe huku akiwasihi kina baba waliopo nyumbani kuhamasika na kutenga muda wa kuwa na watoto wao.

" Nawapongeza kina baba waliojitokeza hapa leo kuleta watoto wao kupata huduma za kliniki na pia kusikiliza elimu ya lishe inayotolewa na wataalam ni kitu kizuri na kinajenga upendo wa mtoto kwa wazazi wote wawili baba na mama”.alisema Bi Mariam

Akiwasilisha taarifa ya hali ya lishe ya wilaya ya Ilemela Bi.Pili Kassim amesema Halmashauri imeendelea kutenga kiasi cha shilingi 1000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka 5 katika kuhakikisha watoto wote wanafikiwa kwa lengo la kupunguza na kutokomeza Utapiamlo na kuendelea kuhamasisha jamii kulima mazao yenye viini lishe kwa wingi ili kuimarisha afya zao.

Bwana na Bibi Nzobana ni wakazi wa kata ya Kahama katika mtaa wa Buyombe wao wanaipongeza serikali kwa kuanzisha utaratibu wa ugawaji wa chakula lishe kwa watoto sambamba na utoaji wa elimu endelevu ya lishe kwa wananchi.

Hadi sasa kiasi cha Shilingi Milioni 7.45 kimetumika kununua chakula lishe hicho ambacho kimetolewa kwa watoto 40 wenye umri wa kuanzia miezi sita hadi miaka 5 wenye utapiamlo  mkali ambapo lengo ikiwa ni kuwafikia watoto 100 kwa kila robo ya mwaka.

CREDIT: Manispaa ya Ilemela.

No comments