Breaking News

DKT. HOSEA-KUPITIA MRADI WA HEET TUNAKWENDA KUONGEZA WATAALAM

 


Mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi kupitia Elimu ya Juu (HEET) unakwenda kusaidia nchi kuongeza idadi ya watalamu kwa upande wa sayansi katika kipindi kifupi kijacho.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Kennedy Hosea, wakati akizindua programu maalumu ya msingi kwa wasichana inayofadhiliwa na mradi wa HEET, leo Oktoba 13, 2023 Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambapo katika tukio hilo Dkt. Hosea amemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Caroline Nombo.

“Tunataka tupandishe idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu nchini, wanaojiunga elimu ya chuo kikuu nchini kwa sasa ni asilimia 7 pekee, tunataka tupandishe hiki kiwango. Huu mradi wa HEET utasaidia kupata wanafunzi ambao hawapo katika mfumo rasmi kwa lengo la kuwawezesha kupata sifa na kuongeza idadi ya wanaojiunga na elimu ya juu nchini na tunataraji kupata wataalamu kutoka kwenye kundi hili siku zijazo.” Amesema Dkt. Hosea.

Aidha, Dr. Hosea, amewataka wanafunzi waliopata fursa hiyo kujiandaa vyema ili waweze kufikia malengo yao ambayo hapo awali yalififishwa kutokana na changamoto mbalimbali zilizowakabili na kuwataka wawe mfano kwa kufanya vyema ili kuipa nguvu serikali iweze kuongeza udahili na ufadhili wa namna hii kwa wasichana wengine wenye uhitaji kutoka jamii ambazo hazijafaidika sana na elimu ya juu. Dkt. Hosea amempongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake yenye mawanda mapana katika kuwaletea maendeleo Watanzania katika nyanja zote na elimu ikipewa nafasi ya juu kabisa.

"Haya yote yanayofanyika katika sekta ya Elimu ni maelekezo kutoka kwa Rais wetu Mama Samia mara tu alipoapa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliagiza kufanya Mapitio ya Mitaala, Sera na sheria ya Elimu nchini na kwa sasa wizara imefika hatua ya juu sana katika kutekeleza maelekezo hayo na sasa tunasubiri vyombo vya maamuzi vijadili na kuridhia ili utekelezaji uanze. Mabadiliko hayo yanalenga katika kuzalisha wahitimu wenye elimu ujuzi ambao wataweza kujiajiri na kuajiri wenzao." Ameongeza Dkt. Hosea.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, ameishukuru Benki ya Dunia kwa kushiriki kwa kiwango kikubwa katika kuchangia maendeleo ya chuo hiki tangu kuanzishwa kwake, ambapo kwa sasa benki hiyo imefadhili hawa wanafunzi elfu moja na ameihakikishia benki hiyo pamoja na wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuwa chuo hiki kimejiandaa vyema kuendesha mafunzo hayo.

“Chuo chetu kimejiandaa vyema kuendelea kuitangaza programu hii tukitarajia baada ya miaka kadhaa mbele tutakuwa tumetayarisha idadi kubwa ya wanawake wanaosoma fani za sayansi katika vyuo vikuu mbalimbali nchini. Ufadhili huu umelenga wasichana wenye mchepuo wa sayansi ili nanyi mshiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya nchi yetu.” Amesema Prof. Bisanda.

Awali akitoa maelezo ya utambulisho wa programu maalumu ya msingi kwa wanafunzi wasichana katika ufunguzi huo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hiki anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Huduma za Ushauri wa Kitaalamu na ambaye pia ndiye mratibu wa mradi wa HEET chuoni, Prof. Deus Ngaruko, amesema, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimejiandaa kutangaza awamu ya pili ya udahili kwa wanafunzi wa programu hii ambao wataanza kusoma mwezi wa Disemba 2023 ikiwa ni mchakato wa kuhakikisha kuwa idadi ya wanafunzi ilivyopangwa na mradi inafikiwa ipasavyo.

“Hivi karibuni tutatangaza tena awamu ya pili ya programu hii ili wakifika idadi ya wanafunzi mia mbili tuweze kuanza mafunzo Disemba 2023 na hatimae awamu ya tatu mwezi wa Aprili 2024. Tunaipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ufadhili kwa wanafunzi hawa. Hakika, ufadhili huu ni muhimu sana na utasiaidia katika kuongeza wataalamu wa fani za sayansi hapa nchini." Amesema Prof. Ngaruko.

Mradi wa HEET umetoa ufadhili wa wanafunzi elfu moja kwa kipindi cha miaka mitano cha mradi huu kusoma progam maalumu ya msingi katika masomo ya sayansi kwa wasichana waliokuwa wamekosa sifa za kujiunga moja kwa moja vyuo vikuu katika ngazi ya shahada za awali, wanfunzi wa kike wapatao 140 wamefanikiwa kujiunga na mafunzo katika awamu ya kwanza na watakaofanikiwa kumaliza vyema watajiunga na elimu ya juu katika vyuo mbalimbali nchini na wanatarajiwa kunufaika na mikopo itolewayo na taasisi mbalimbali za mikopo nchini.

Umaalumu katika programu hii ni kwamba wanafunzi hawa wamepata ufadhili wa masomo yao kwa asilimia mia moja (100%) ikiwa ni ada,viandikwa, malazi, chakula, nauli na vishikwambi kwa ajili ya Kujifunzia katika masomo yao. Mafunzo haya ni ya mwaka mmoja na wanafunzi watakapohitimu na kupata sifa stahiki za ufaulu watajiunga na masomo ya shahada za sayansi, teknolojia, uhandisi na hesabu.

No comments