Breaking News

UTUMIAJI WA DAWA KALI KIPINDI CHA UJAUZITO SABABU MOJA WAPO YA KUZALIWA MTOTO NJITI.

 

Na Tonny Alphonce,Mwanza

Imeelezwa kuwa matumizi ya Dawa za kienyeji,Maradhi katika njia ya kizazi kwa mama mjamzito ni sababu mojawapo zinazosababisha mama kujifungua chini ya siku 37 (Mtoto Njiti).



Mganga Mfawidhi na Dakatari bingwa wa Watoto kutoka hospitali ya mkoa ya Souko Toure Dr Bahati Peter Msaki amesema mama anapotumia dawa kali kipindi cha ujauzito anaweza kusababisha kuzaa mtoto njiti kutokana na dawa hizo kuwa kali na kumsababishia mama mjamzito uchungu wa kujifungua kabla ya muda.

Dk amesema sababu nyingine kubwa ambayo husababisha mama kujifungua mtoto njiti ni maambukizi katika njia ya uzazi ambayo husababisha baadhi ya mambo kutokwenda sawa na hivyo mtoto kulazimishwa kutoka kabla ya wakati.

‘Kama utakumbuka madaktari huwa hatushauri kabisa mama anapokuwa mjamzito kutumia dawa hovyo sababu mojawapo ni hiyo tusimsumbue mtoto aliyepo tumboni,kipindi cha uumbaji havitakiwi vitu vikali au visivyo vya lazima kuliwa au kunywewa na mama mjamzito na mfano kipindi hiki cha Uviko 19 mwanzoni  hatukuruhusu mama mjamzito kuchanjwa hadi pale utafiti ulipofanyika na tukakubaliana tunaweza kuwachanja’.alisema

Amesema matatizo ya kifamilia, msongo wa mawazo na ya kisaikolojia kama kupigwa na kuteswa wakati wa ujauzito, kufanya kazi za kusimama kwa muda mrefu ni moja ni sababu moja wapo ya mama kujifungua kabla ya wakati.

Dk Bahati amesema watoto wanaozaliwa njiti wana changamoto za kiafya likiwemo tatizo la uono hafifu ambalo baadae husababisha upofu.

‘Changamoto hizi kwa Watoto njiti ni za kawaida lakini kwa mazazi humsumbua kwa sababu kila mzazi hutamani kumpata mtoto aliyekamilika lakini Watoto hawa hawapendi baridi hii ni asili yao na ndio maana hukulia kwenye vyumba vya joto lakini pia baadhi ya viungo vyao kwa kawaida huwa havipo sawa’.alisema

Kwa upande wa kinga za mwili Dk Bahati amesema changamoto kubwa ni kwa mtoto mwenye umri wa mwa 0-5 lakini akivuka hapo uwezo wa kuishi mtoto njiti mkubwa kama ilivyo kwa watoto wengine.


Amesema vifo vingi vya watoto chini ya miaka mitano huwapata watoto waliozaliwa kabla siku 37 kutokana na sababu za kiafya na kimazingira.

Kama nilivyosema watoto hawa huzaliwa na kasoro na kinga mwili zao zinakuwa chini wengi wao husumbuliwa na tatizo la upumuaji kutokana na kutokomaa kwa viungo vyao hivyo huwa rahisi sana kushambuliwa na magonjwa ambayo yanaweza kusababisha kifo lakini kwa upande wa mazingira watoto hawa huitaji chumba chenye joto na mashine za joto sasa ikitokea vitu hivi vikakosekana husababisha vifo kwa Watoto hawa,alisema.

Kwa upande wake afisa lishe wa jiji la Mwanza Joyce Zelamala amesema malezi ya mtoto njiti ni gharama kwa kuwa anahitaji kuwa chini ya uangalizi wakati wote hasa upande wa kumkinga na baridi baada ya kutoka hospitali kwa kuwa watoto hao hupoteza joto kwa haraka kupitia ngozini kutokana na Watoto hawa kuwa na kiwango kidogo cha mafuta ya Ngozi.


‘Silaha kubwa  kwa mtoto njiti ni kumnyonyesha vizuri ili kumkinga na magonjwa nyemelezi na hata akifikia umri wa kula chakula lazima umsimamie kula vyakula vya kujenga mwili kwa sababu watoto hawa huwa dhaifu sana na wanaweza kutokula vyema’.alisema Bi Joyce.

Amesema pamoja na usimamizi wa chakula lakini mama anatakiwa kuwa msafi wakati wote ili kumkinga mtoto asipate maambukizi ya magonjwa ikiwemo kunawa mikono vyema kila anapotaka kumshika mtoto na kujiepusha kumchubua ngozi na kumsababishia maambukizi ya magonjwa kutokana na Ngozi yake kuwa laini.

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikadiria takribani watoto milioni moja walipoteza maisha kutokana na tatizo hili mwaka 2015, hata hivyo, inaelezwa robo tatu ya vifo hivyo vingeweza kuzuilika.


Inaelezwa kuwa kwa kila watoto kumi wanaozaliwa, mmoja kati yao ni njiti ambapo takribani watoto milioni moja hupoteza maisha kila mwaka kutokana na tatizo hilo kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na WHO.


No comments