Breaking News

MATUKIO YA MIMBA KWA WANAFUNZI MWANZA YAONGEZEKA

 Na Neema Emmanuel.


IMEELEZWA kuwa matukio ya kuwapa wanafunzi mimba yanaongezeka na kufikia 96 mkoani Mwanza kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu huku jamii ikitakiwa kuamka na kuwa mstari wa mbele kupinga ukatili kwa vitendo dhidi ya watoto.



Hayo yamebainishwa na Mkuu wa dawati la Jinsia na Watoto mkoani Mwanza, Faraja Mkinga katika kikao maalumu cha wajumbe wa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) .

Ameeleza kuwa matukio ya mimba kwa wanafunzi ndio yanayoongoza , yakifuatiwa na matukio ya ubakaji 92, kutorosha wanafunzi 32, ukatili dhidi ya mtoto ikiwemo kipigo 31, kutelekeza familia 28 na shambulio la aibu 20.

Huku matukio ya kulawiti yakiwa 19, shambulio kwa mwenzi 13, matukio nane ya kufanya mapenzi na wanafunzi, matatu ya kutoa mimba, matatu ya kutupa watoto, moja la kujeruhi na moja la mtoto kukinzana na sheria.

"Katika orodha matukio ya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa kwenye kitengo cha dawati la Jinsia na Watoto mkoani Mwanza katika kipindi hicho ni matukio 347 ya ukatili wa kijinsia yaliripotiwa katika dawati huku 96 kati yake yakiwa ni matukio kuwapatia wanafunzi mimba"ameeleza Mkinga.

Ameongeza takwimu zinaonyesha matukio kuwa matukio yanaongezeka mara baada ya jamii kuwa na uelewa kuhusu vitendo vya ukatili hivyo kupelekea kutoa taarifa katika vituo vya Polisi pindi matukio yanapotokea.

" Mwarobaini ya haya yote ni kuwachukulia hatua wahusika ,elimu ya afya ya uzazi itolewe kikamilifu kwa wanafunzi hii itasaidia kuwanusuru na wimbi ili la mimba pia wazazi nao wasikae nyuma kutoa elimu kwa watoto na kuwa karibu nao" anaeleza

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto la Kivulini, Yassin Ally amesema sasa ni wakati wa jamii kubadilika kwani malezi mabovu kuchangia mwendelezo wa matukio hayo .

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Makanisa mkoani Mwanza, Dk Robert Bundala ametaja mmonyoko wa maadili ,wazazi kutokuwa na muda wa kutosha kuwa karibu na watoto kunachangia kutokea matukio hivyo aliitaka jamii kuwa na hofu na kumrudia Mwenyezi Mungu ili kuepukana na vitendo hivyo.

Mwisho.

No comments