Breaking News

UNFPA NA WADAU WA AFYA KUENDELEA KUSAIDIA MAPAMBANO YA UGONJWA WA FISTULA NCHINI


Na Tonny Alphonce, Mwanza.

Umbali wa huduma za afya,Kukosekana kwa huduma ya dharura kwa mama anapojifungua mbali na kituo cha afya,kukosekana kwa elimu dhidi ya ugonjwa wa Fistula na upasuaji usio salama ni sababu moja wapo zilizotajwa kusababisha ugonjwa wa Fistula.

Meneja miradi ya afya ya uzazi Mama na Mtoto kutoka Shirika la umoja wa mataifa afya ya uzazi (UNFPA) Felister Bwana akitoa salamu za Shirika la UNFPA katika maadhimisho ya Siku ya Fistula Duniani.

Hayo yamesemwa na Meneja miradi ya afya ya uzazi Mama na Mtoto kutoka Shirika la umoja wa mataifa afya ya uzazi (UNFPA) Felister Bwana wakati wa maadhimisho ya siku ya Fistula Dunia yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza tarehe 23/05/2022 katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.

Felister amesema katika kukabiliana na ugonjwa huo wa Fistula ambao chanzo kikubwa ni uzazi pingamizi UNFPA imekuwa ikiwapatia mafunzo madaktari ili waweze kupata utalaam wa kumzalisha mama salama,kutoa elimu ya uzazi wa mpango kwa lengo kuzuia mimba katika umri mdogo na kuhakikisha huduma za dharura kwa mama mjamzito anayepata uzazi pingamizi aweze kusaidiwa kwa haraka na hatimaye ajifungue salama.

“Kwa hiyo sisi UNPA tunawekeza rasilimali, pesa,ujuzi na utaalamu kupitia wizara ya afya kuhakikisha hayo mambo matatu yanatekelezeka,kwa sababu tukiweza kuyafanya hayo mambo matatu ni wazi tutapunguza vifo vinavyotokana na uzazi lakini tunakuwa tumezuia Fistula”.alisema Felister.

Kwa upande wake Dkt Issa Rashid kutoka CCBRT amesema wao wameitekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya mwaka huu inayosema Tokomeza Fistula,Wekeza Imarisha huduma ya afya na Wezesha Jamii kwa kuzindua hospital mpya ya kina mama na wajawazito yenye uwezo wa kubeba wagonjwa kuanzia 200 wakiwemo wale wenye Fistula.

Dkt Issa Rashid kutoka CCBRT akielezea shughuli zinazofanywa na CCBRT katika kupambana na ugonjwa Fistula nchini.

Dkt Issa amesema hospital hiyo itakapoanza kufanyakazi itawahudumia wanawake wenye historia ya fistula,wanawake walemavu na mabinti wanaopata mimba chini ya miaka 20 bila malipo kwa lengo la kuzuia fistula mpya,Ulemavu na vifo vya mama na mtoto.

Amesema CCBRT tangu ianze mapambano ya kutoa matibabu ya Fistula mwaka 2003 wagonjwa zaidi ya 8000 walitibiwa kwa mafanikio makubwa na zaidi ya asilimia 90 kati yao walirudi nyumbani wakiwa wamepona na kubadilisha maisha yao.

Akizungumza na wananchi mgeni rasimi katika maadhimisho hayo Mkurugenzi wa Tiba Asili na Mbadala kutoka wizara ya afya Dkt Paul Mhame amesema jitihada za wadau zinaonekana kuzaa matunda kwa kuwa ugonjwa wa Fistula umepungua kwa asilimia 30 ukilinganisha na mwaka 2015 na 2019.

Mkurugenzi wa Tiba Asili na Mbadala kutoka wizara ya afya Dkt Paul Mhame akiongea na wageni waalikwa (hawapo pichani) katika maadhimisho ya Siku ya Fistula Duniani.

Akizungumzia kushuka kwa idadi ya wagonjwa Fistula Dkt Mhane amesema idadi hiyo imeshuka kutokana na kuimarika kwa huduma za afya kwa mama wajawazito na upatikanaji wa huduma za upasuaji za dharura ambao unatolewa katika hospitali zaidi ya tano hapa nchini.

Naye Mkurugenzi wa Hospital ya Rufaa ya Kanda ya Bugando Dkt Fabian Massaga amesema uzazi pingamizi unaweza kuzuilika kwa kuwa viashiria vyake vinajulikana ikiwemo mama mjamzito anapokaribia kujifungua asindikizwe hospital ili akipata tatizo msindikizaji anaweza kumsaidia mama na hatimaye kuzuia Fistula.

Mkurugenzi wa Hospital ya Rufaa ya Kanda ya Bugando Dkt Fabian Massaga akielezea namna Hospitali ya Rufaa ya Bugando inavyotoa huduma za Fistula kwa kina mama.

Dkt Massaga amesema takwimu za mwaka2020/2021 zinaonyesha  hospitali ya Rufaa ya Bugando inapokea wagonjwa wa Fistula 300 hadi 400 kwa mwaka ambao hupatiwa huduma za upasuaji kwaajili ya kuhakikisha wanarudi katika hali yao ya kawaida.

Muhanga wa ugonjwa wa Fistula Neema Constantine ameitaka serikali na wadau wa afya kuendelea kutoa elimu ya uelewa kwa jamii kwa kuwa bado wanawake wengi hawaujui ugonjwa huu wakiuhusisha na Imani za kishirikina na hivyo baadhi yao hupoteza maisha na kuacha Watoto wachanga wakikosa malezi muhimu ya mama.

Muhanga wa ugonjwa wa Fistula Neema Constantine akieleza namna alivyoweza kupambana na ugonjwa wa Fistula.

Neema amesema alipitia mateso makubwa alipopatwa na ugonjwa huo mara baada ya kujifungua ambapo alichanika vibaya na alivyofanyiwa upasuaji na kushonwa hali ilikuwa mbaya kwa kuwa upasuaji hakwenda vizuri na hivyo kuanza kutokwa na haja kubwa katika sehemu zake zote za siri bila kujitambua.

Zaidi ya wanawake 3000 nchini wanapatwa na ugonjwa wa Fistula kila mwaka mara baada ya kujifungua kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya mama kuugua uchungu kwa muda mrefu kabla kujifungu.

Shinikizo la muda mrefu linalotokana na kichwa cha mtoto kulazimisha kutoka na kusababisha kovu kubwa ambalo hugeuka shimo katika njia ya uzazi na kusababisha mama kuanza kutokwa na haja ndogo na kubwa bila kujitambua.


Fistula inachangia asilimia 8 ya vifo vya uzazi,asilimia 90 ya visa vya kujifungua Watoto wafu ,hii ni Kwa mujibu wa shirika la UNFPA.

Ugonjwa wa Fistula ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha msongo na mashaka yanayohusiana  na uzazi katika kipindi cha ujauzito na miaka ya mwanzo  ya Maisha ya mtoto ambapo huleta athari ya afya kwa mama ambapo husababisha mama kushindwa kujitunza na kuathiri ukuaji na maendeleo ya mtoto.

No comments