Breaking News

VITENDO VYA UKATILI KWA WATOTO BADO TATIZO MWANZA, WANAUME WARIPOTIWA KUTELEKEZA FAMILIA ZAO


Na Tonny Alphonce, Mwanza.

Imeelezwa kuwa matukio ya Ukatili dhidi ya Watoto yameendelelea kuongezeka Mkoani Mwanza na kufikia 31 huku matukio ya wanaume kutelekeza familia yakiripotiwa 28 katika kipindi cha mwezi januari na march mwaka huu.

Faraja Mkinga ambae ni Mkuu wa dawati la Jinsia na watoto mkoani Mwanza ameyasema hayo katika kikao maalumu cha wajumbe wa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.

Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mwanza Bwana Isack Ndasa akizungumza katika kikao cha maalumu cha wajumbe wa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.

Faraja amesema ukatili ambao watoto wamekuwa wakifanyiwa ni pamoja na vipigo vilivyopitiliza pamoja na matukio ya kuingiliwa kimwili ambapo matukio 19 ya ulawiti yaliripotiwa.

Kwa upande wa matukio yaliyowagusa wanawake na watoto wachanga,Faraja ameyataja kuwa ni matukio 92 ya ubakaji, shambulio kwa mwenzi 13, kutoa mimba matukio 3 na tukio moja la kutupa mtoto.


Amesema katika orodha matukio ya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa kwenye Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoani Mwanza katika kipindi cha miezi mitatu ni matukio 347 ya ukatili wa kijinsia huku 96 kati yake yakiwa ni matukio kuwapatia wanafunzi mimba.

Akielezea sababu za matukio mengi kuripotiwa tofauti na miaka ya nyuma amesema kwa sasa jamii imepata elimu ya kutosha kuhusia na vitendo vya ukatili hivyo kupelekea kutoa taarifa katika vituo vya Polisi pindi matukio yanapotokea.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto la Kivulini, Yassin Ally ameitaka jamii kubadilika katika suala zima la malezi ili kuwa na jamii yenye hofu ya Mungu na hivyo kuchangia kupunguza matukio hayo.


Yasini amesema wimbi la vitendo vya Ulawiti,Ulevi,Utoro na Madawa ya kulevya limeanza kuingia katika shule za msingi zilizopo katika kata ya Mirongo jijini Mwanza hivyo kuitaka jamii wakiwemo viongozi wa dini na serikali kuchukua hatua za haraka ili kuwanusuru Watoto walioko mashuleni.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Makanisa mkoani Mwanza, Dkt Robert Bundala amesema mmonyoko wa maadili ,wazazi kutokuwa na muda wa kutosha kuwa karibu na watoto kunachangia kutokea matukio ya kikatili hivyo ameitaka jamii kuwa na hofu ya Mungu na kumrudia Mwenyezi Mungu ili kuepukana na vitendo hivyo.

“Ukiangalia suala hili katika ulimwengu wa kiroho unaona kabisa matendo haya yote yaliyoripotiwa hapa yana shetani ndani yake na pia kukosekana kwa upendo wa kweli katika familia zetu  kama mama atampenda baba na watoto kuwapenda wazazi wao litakuwa ni suluhisho la kudumu katika kukabiliana na ukatili”.alisema Dkt Bundala.

Isack Ndasa afisa maendeleo ya jamii mkoa wa Mwanza kwa upande wake amewataka wazazi na walezi kuwa karibu na Watoto wao na kuwadadisi changamoto wanazokutananazo shuleni na mtaani ili waweze kuwasaidia mapema kabla hawajaathirika.

Katika kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto,Serikali iliandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2016/17 – 2021/22 (MTAKUWWA).

Mpango huu jumuishi unalenga kutokomeza ukatili kwa kina ukiwa na afua ambazo zimelenga Elimu ya malezi,usalama shuleni,utekelezaji wa sheria,mazingira salama katika maeneo ya umma na maeneo mengine.

 Credit: AFP (photo).

 

No comments