Breaking News

WIZARA ISIDHALILISHE TAALUMA YA HABARI

 

Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Mhariri na Mwandishi wa Habari -Salome Kitomari

Wizara ‘isidhalilishe’ taaluma ya habari

Kwa miaka 19 ya uzoefu kwenye uandishi wa habari leo (Julai 17,2023), nimekutana na jambo ambalo nisipopaza sauti nitakuwa sijaitendea haki taaluma yangu, nafasi yangu kama kiongozi wa taasisi ya habari ya MISA TANZANIA, Mhariri na mwandishi wa habari wa muda mrefu.


Leo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilialika wahariri na waandishi wa vyombo vya habari kwenye mkutano wa Waziri, Dk. Stergomena Tax, tuliitika wito kwa kufika kwenye ukumbi wa Mwalimu JNCC saa nne kamili, lakini bahati mbaya alifika baada ya saa tano unusu, alituomba radhi kwa kuchelewa kutokana na majukumu mengi aliyonayo.Hili halikuwa tatizo.


Lengo la mkutano ni waandishi wa habari kuujulisha umma kuhusu ujio wa Rais wa Hungary, Katalin Novak mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki kuhusu raslimali watu utakaofanyika nchini  Julai 25 na 26, mwaka huu.


Kilichonishtua na kunisukuma kuandika haya ni muda mfupi kabla ya kiongozi huyo kufika alitokea Ofisa mmoja aliomba wahariri na waandishi kukaa nafasi za mbele kwa kuwa Waziri amekaribia kufika, tulitii wito na kwenda kukaa mbele.

Muda mfupi tuliona idadi wasanii kadhaa kama kumi wakiingia kwenye chumba hicho, haraka ofisa mmoja alitufuata kututaka tupishe nafasi hizo kwa kuwa zilikuwa maalum kwa ajili ya wageni ‘maalum’ wa Waziri,tulipisha.


Kilichoshangaza ni kwamba wote tuliitwa kama waandishi wa habari na wale wageni maalum walitambulishwa kama waandishi wa ‘kisasa’ nasi tulitambulishwa kama waandishi wa ‘zamani’, na walipewa nafasi maalum kwa ajili ya kumsikiliza waziri na kuuliza maswali pamoja nasi wa ‘zamani’ kuuliza maswali.


Taaluma hii inatambuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, 2016 na huwezi kufanya majukumu ya habari kama hujasoma kwa kiwango cha Diploma, lakini leo hii wasanii na influencer wanaitwa kwenye mkutano wa waandishi na kutambuliwa kama waandishi wa ‘kisasa’ na wale waandishi wenye taaluma yao wanapaswa kupisha ‘wageni maalum’ ‘waandishi wa kisasa’


Ni muhimu kuandika haya ili Serikali, Wizara na Taasisi nyingine zikajua tofauti kati ya mwandishi wa habari na mtu mwenye wafuatiliaji wengi kwenye mitandao ya kijamii aliyeamua kutumia ukurasa wake kwa madhumuni tofauti, haipendezi kabisa kuishusha hadhi taaluma yetu kiasi hiki, tena kwa Wizara yenye watu ambao wamewahi kufanyakazi ya uandishi wa habari sio kwa ‘kujipenyeza’ tu bali kwa kusoma darasani kwa ngazi tofauti tofauti.

Tabia hii ikiachwa hivi maana yake leo ni kuruhusu kuendelea kuitukanisha na kuidharaulisha taaluma ya habari nchini, ambayo inaonekana kila mtu anaweza kufanya, HILI HALIKUBALIKI.


Napendekeza Serikali ambayo ndiyo inayosimamia wa sheria iliyotungwa na Bunge, ilinde sheria kwa wivu mkubwa, pia lazima kutofautisha mkutano wa waandishi wa habari na mkutano wa wasanii na influencer.

Mara kadhaa waandishi wa habari wamekuwa wakitupiwa lawama ya kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii kwasababu baadhi ya watu wanshindwa kutofautisha na kuona wote ni waandishi wa habari, na kama hili linaanza kufanywa na mamlaka maana yake ni kuhalalisha ‘kusigina’ Sheria iliyopitishwa na Bunge.


Salome Kitomari- Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Mhariri na Mwandishi wa Habari.


No comments