Breaking News

WATOTO WANAOFUNGIWA NDANI HATARINI KUUGUA UGONJWA WA MACHO WA MYOPIA

 

Na Tonny Alphonce, Mwanza

Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, watoto wengi siku hizi wanapenda kutumia vifaa vya kisasa na kuingia kwenye hatari ya kupata ugonjwa wa macho wa Myopia ambapo husababisha mtoto kuona vitu vya karibu, lakini hawezi kuona mbali.


Sababu kubwa ya ugonjwa huo husababishwa na matumizi ya vifaa vya kisasa kama vile simu za viganjani, tableti na kompyuta kucheza michezo ya kwenye simu kwa muda mrefu bila kutoka nje na kucheza michezo mingine.

Tatizo hili limekuwa sugu kwa watoto wengi hasa wale wa miaka 2-10 maana hufurahia sana michezo hiyo ya kwenye simu na matokeo yake ni kwamba, wanakosa mwanga wa jua, ambao ni muhimu sana na hivyo kuwasababishia tatizo hilo la macho.

Mkuu wa Idara ya macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya  Bugando, Dk Christopher Mwanansao amesema watoto kutopata muda wa kucheza nje na badala yake kushinda ndani wakichezea simu za wazazi wao na kutazama runinga ni hatari kwa afya ya macho yao hali ambayo inasababisha watoto wengi wa kizazi hiki kusumbuliwa na maradhi ya macho.

Mkuu wa Idara ya Macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya  Bugando, Dk Christopher Mwanansao akielezea sababu zinazoweza kusababisha uoni hafifu

“Vema watoto wakapewa muda wa kucheza nje na wenzao ili wapate mwanga wa jua lakini pia iwasaidie kuona mbali maana wakicheza nje watakuwa na uwezo kuangalia umbali wa hata mita 10 kutoka sehemu wanayochezea kwa kufanya hivyo itawasaidia kuona mbali na kuimarisha misuli ya macho”, alisema Dk Mwanansao.

Dk Mwanansao amesema wagonjwa wengi wanaohudumiwa katika kliniki ya Bugando hukutwa na tatizo la saratani ya mtoto wa jicho, mzio wa macho, presha ya macho, kisukari cha macho na uoni hafifu, ambapo asilimia 60 ya watu wanaopata upofu hutokana na tatizo la mtoto wa jicho ambalo huwakumba zaidi wazee na watoto wenye umri wa miaka 0-8.

Amesema "kwa sehemu kubwa matatizo ya macho yanasababishwa na umri unapoenda ndipo watu wengi wanapata matatizo hayo, hivyo unapofikisha miaka 40 walau uende hospitali kuchunguza uwezo wako wa kuona. Pia watoto wengi wanazaliwa na mtoto wa jicho kutokana na maambukizi ya mama, magonjwa ya kurithi na kisukari".

Ameongeza kuwa, baada ya kliniki ya Bugando upande wa macho kuboreshwa wamekuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa takribani 100 kwa siku, 500 kwa wiki na 2,400 mpaka 2,600 kwa mwezi na visababishi vikubwa vya magonjwa ya macho ni umri, mazingira yanapelekea kupata mzio kwenye macho, kurithi upande wa watoto wadogo, kisukari na presha.

Kwa upande wake Mkurugenzi Hospitali ya Rufaa ya Bugando Dk Fabian Masaga amewataka wazazi kuwaruhusu  watoto wadogo  kushiriki michezo ya nje ili  kuwapa nafasi ya kuona mbali na siyo karibu peke yake pamoja na kuwavalisha miwani ya kukinga miale ya jua pindi jua linapokuwa kali wakati wa matembezi ya mchana.

Mkurugenzi Hospitali ya Rufaa ya Bugando Dk Fabian Masaga akiongea na wananchi waliofika katika viwanja vya Bugando

Dk Masaga amewataka wazazi na walezi kuwapatia watoto mlo kamili wenye kurutubisha afya ya macho pamoja na kujenga tabia ya kuwapima macho  mara kwa mara hata kama hayana tatizo.

Dk Fabian Masaga amesema hospitali ya Bugando inafanya jitihada kuhakikisha hakuna mwananchi anayepoteza uoni kwa changamoto za macho kwa kuboresha miundombinu, kutoa huduma za kibingwa katika hospitali za wilaya na mikoa, kutoa huduma za upasuaji kwa gharama nafuu na vipimo vya bure.

Naye mmoja  wa wagonjwa  aliyefika hospitalini hapo Suzana Steven akiwa ameambatana  na mtoto wake mwenye umri wa miaka mitano ili kupata huduma ya uchunguzi wa macho, amewashauri wazazi na walezi kuwa utaratibu wa kufanya uchunguzi wa macho mara kwa mara ili kubaini matatizo ya macho angali mapema.

"Nimesumbuliwa na tatizo la uoni hafifu kwa miaka mitatu sasa, baada ya kufanya kazi ya katibu muhtasi muda mwingi nilitumia kompyuta ambapo imenipelekea kupata taitizo la uoni hafifu.Nae na mtoto wangu baada ya vipimo amegundulika kuwa  na tatizo kama langu ambalo kwake limesababishwa na kuchezea simu kwa muda mrefu pamoja na kuangalia runinga kwa muda mrefu".alisema Suzana.

Dkt Masaga amehitimisha kwa kusema wazazi na walimu wanaweza kugundua kama mtoto  ana ugonjwa wa macho kwa kuangalia dalili zifuatazo; mtoto kama anafinya macho akiwa anasoma, anasogeza kitabu usoni wakati wa kusoma, akiwa anaangalia  runinga anaisogelea na watoto wengine hufikicha macho sana, hizo ni dalili za awali na ukiziona kama mzazi au mlezi mpeleke mtoto hospitali kwa uchunguzi mara moja.



No comments