Breaking News

SERIKALI YATAKIWA KUSOGEZA HUDUMA YA MAMA NA MTOTO KISHIRI MWANZA

 Na Tonny Alphonce,Mwanza

Wakazi wa kata ya Kishiri wilayani Nyamagana mkoani Mwanza wamekuwa wakilazimika kutembea umbali wa kilometa zaidi ya sita ili kupata huduma ya kujifungua kwa mama wajawazito.


Wakazi hao ambao kwa sasa wanapata huduma ya mama na mtoto katika kituo cha afya Igoma au katika hospitali ya mkoa ya Sekou Toure na hupelekea baadhi ya wanawake wajawazito kujifungua wakiwa njiani na kuhatarisha afya ya mama na mtoto.

Kituo cha Afya Igoma ambacho kwasasa ndio kimbilio la wakazi wa kata ya Kishiri

Emmaculata Masanja mkazi wa Kishiri anasema serikali iliwahi kutangaza kumaliza tatizo hilo kwa kujenga jengo la Mama na Mtoto  kupitia mfuko wa kusaidia Kaya Masikini (TASAF) lakini hadi sasa ujenzi huo bado haujakamilika.

“Kwa hivi sasa mama akikaribia kujifungua lazima uhakikishe unapesa ya usafiri wa kumpeleka hospitali vinginevyo mjamzito anaweza kujifungua mkiwa njiani na tukifika hospitali mama ameishajifungua wahudumu wa afya wanakuwa wakali kwanini tumemchelewesha mama”. alisema Emmaculata

 Ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto Fumagila Kishiri ukiwa unaendelea.

Emmaculata ameitaka serikali kuhakikisha inamaliza ujenzi wa jengo la mama na mtoto ambalo linaendelea kujengwa kwa hivi sasa ili kuwapunguzi umbali na gharama kina mama wenye ujauzito.

"Ili kuwa na uhakika wa usalama wa mama na mtoto huwa tunalazimika kukusanya fedha za usafiri wa kumsafirisha mama kwenda kituo cha afya mara baada ya kushikwa na ujauzito na kina mama wengine huwa wanalazimika kuomba hifadhi hapo Igoma wakisubiria mama kujifungua".alisema Emmaculata

Akizungumza na wakazi wa kata hiyo katika ziara ya kukagua miradi inayotekelezwa na TASAF katika wilaya ya Nyamagana Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe.Amina Makilagi ameutaka mfuko wa kusaidia Kaya Masikini (TASAF) kuhakikisha unakamilisha ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto Fumagila Ili kuwapunguzia umbali mrefu wa kutafuta huduma bora ya Kijifungua.

Baadhi ya majengo ya jengo la  Mama na Mtoto Fumagila yakiwa katika hatua ya mwisho kukamilika.

Makilagi amesema malengo ya kujenga jengo la mama na mtoto katika kata ya Kishiri ni kuwapunguzia adha akina mama wa ukanda wa huo waliokuwa wakifuata huduma umbali mrefu hadi Igoma na kusababisha kujifungulia njiani na watoto pamoja na mzazi kupata matatizo mbalimbali ya kiafya.

Nyamagana Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe.Amina Makilagi akizungumza na viongozi wa TASAF na Viongozi wa kata ya Kishiri juu ya ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto.

"Mratibu wa TASAF hakikisheni jengo hili linakamilika kwa wakati na kuanza kutumika maana linavyozidi kuchelewa ni wazi linakwamisha juhudi za wananchi waliojitolea nguvu kazi kuhakisha mradi haukwami ili umalizike kwa wakati na wananchi wapate huduma wanayohitaji," amesema Makilagi.

Akizungumzia madhara ya mama mjamzito kucheleweshwa  hospitali  Getrude John Ndalifashe mkunga na mtaalamu wa masuala ya mama,uzazi na mtoto kutoka shirika la Uzao Wetu amesema mama na mtoto wote wanaweza kupata madhara ukiwemo ugonjwa wa Fistula,kupoteza damu nyingi na mtoto anaweza kupata tatizo la mtindio wa ubongo endapo ubongo wake utatikisika wakati wa kuzaliwa.

Getrude amesema ni muhimu mama kuhakikisha anajifungulia hospitali kwa kuwa wakati mama anapojifungua anaweza kupata changamoto zitakazohitaji kutatuliwa na wataalamu wa afya wakiwemo madaktari bingwa.

"Mama anapojifungua huwa  tunangalia mambo mengi lakini pia huwa tunaangalia  kama mtoto amepata maambukizi kwenye kitovu wakati wa kuzaliwa kwasababu  tofauti yoyote inaweza kusababisha utofauti katika ukuaji wa mtoto".alisema Getrude

Malengo 17 ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa ambayo yanatarajiwa kufikiwa mnamo mwaka 2030, yaani kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi hadi kufikia uwiano wa 70 kwa vizazi hai 100,000.

Ripoti ya jamii na afya ya ofisi ya Taifa ya Takwimu, 2015-16 TDHS-MIS yaonyesha kuwa kuna vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000.

Pamoja na kuwa baadhi ya kata za mkoa wa Mwanza bado hazina huduma za Mama na Mtoto takwimu zinaonyesha kuwa Mwanza ni miongoni mwa mikoa mitano ambayo inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanawake wanaojifungua kwenye vituo vya matibabu hii ni kwa utafiti uliofanywa mwaka 2018.

Mikoa mingine ni mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na wanawake 128,853 wanaojifungua kwenye vituo vya matibabu (asilimia 10.8). Mwanza, wanawake 79,077 (7%); Mbeya, wanawake 78,732 ( 7 %); Dodoma, wanawake 63,208 ( 5 %); na Tabora, wanawake 61,457 (5%).

Tanzania imekuwa ikitekeleza Program Jumuishi ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto yenye lengo la kumaliza changamoto ya lishe duni na changamoto nyingine dhidi ya watoto hususani walio chini ya umri wa miaka nane.

Kukamilika kwa ujenzi huo wa jengo la mama na mtoto utasaidia ulinzi wa mtoto kuanzia akiwa tumboni kwa mama mpaka hatua ya awali ya makuzi yake.

No comments