Breaking News

Mabalozi Waaswa Kutekeleza Diplomasia Ya Uchumi

 


Na Mwandishi Wetu, 

Serikali imewaelekeza mabalozi walioteuliwa hivi karibuni kuhakikisha kuwa wanatekeleza na kusimamia diplomasia ya uchumi kwa maslahi mapana ya Taifa.

Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) katika hafla ya kufunga mafunzo maalumu ya wiki mbili yaliyokuwa yanatolewa kwa mabalozi hao katika Chuo cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam.

“Leo nimefunga mafunzo ya wiki mbili kwa mabalozi wetu walioteuliwa hivi karibuni, na imekuwa ni utaratbu wa Wizara kuwanoa kabla ya kwenda katika vituo vyao vya kazi. Mafunzo haya huwajengea uwezo mabalozi kupata ufahamu zaidi pamoja na kujua majukumu yao katika kuendeleza diplomasia ya uchumi, kuhamasisha wawekezaji, utalii na maeneo mengine mengi,” Amesema Balozi Mulamula.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula amewasisitiza mabalozi umuhimu wa kufahamu na kutekeleza Diplomasia ya Siasa iliyopo ndani ya Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi CCM (2020-2025) ili kuweza kuwasaidia kujua dira a nchi.

Pia Balozi Mulamula aliwataka mabalozi kuhakikisha kuwa wanaendeleza lugha ya Kiswahili katika mataifa wanayoenda kuiwakilisha Tanzania kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia sana kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili.

“Kubwa zaidi nimewaagiza kuhakikisha kuwa wanaendeleza lugha ya Kiswahili, kwa sasa lugha ya Kiswahili imekuwa ni bidhaa muhimu sana……..kiswahili ni muhimu sana na sasa Kiswahili kinazungumzwa na zaidi ya watu milioni 500 duniani,” Amesema Balozi Mulamula.

Aidha, Waziri Mulamula amewataka mabalozi kuhakikisha pamoja na mambo mengine, wanatekeleza majukumu yao vyema na kujenga taswira nzuri ya Serikali.

Awali akiongea na mabalozi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab aliwapongeza kwa uteuzi na kuwashauri kuendelea kujituma katika kazi na kuleta mabadiliko ambayo Serikali imeyapanga hasa katika diplomasia ya uchumi.

Balozi Fatma amewaasa mabalozi waliomaliza mafunzo yao kuhakikisha kuwa wanatekeleza diplomasia ya uchumi pamoja na diplomasia ya siasa kwa weledi ili kuleta manufaa ya Taifa.

Tarehe 27 Julai, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliwaapisha mabalozi 13 Ikulu jijini Dar es salaam.

No comments