Breaking News

TATIZO LA KIUCHUMI KATIKA FAMILIA CHANZO CHA MIMBA ZA UTOTONI

Na Tonny Alphonce,Mwanza.

Imeelezwa kuwa chanzo kikubwa cha mimba za utotoni ni tatizo la uchumi katika familia hali ambayo hupelekea Watoto wengi wa kike kujiingiza katika mahusiano ili waweze kupata mahitaji yao ya lazima zikiwemo taulo za kike.

Hayo yamesemwa na mratibu wa shirika la Wadada Solution  Elihaika Mgeni wakati akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Nyafula iliyopo wilayani  Ilemela mkoani Mwanza katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani.

Mratibu wa shirika la Wadada Solution  Elihaika Mgeni akizungumzia namna shirika la Wadada Solution walivyoadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani.

Elihaika amesema Watoto wengi wakike hasa wa maeneo ya karibu na ziwa wamekuwa wakijiingiza katika mahusiano na wavuvi na  kujikuta wanashika ujauzito katika umri mdogo na hivyo kukatiza ndoto zao.

“Watoto hawa wakike ambao wapo katika elimu ya msingi wamekuwa wakidanganywa na wanaume kuwa wanaweza kuwasaidia kuikata hedhi na akikubali kufanya mapenzi anashangaa hedhi inakata kwa kuwa anakuwa ameshika ujauzito na kuanzia hapo Maisha yake yanaharibika”alisema Elihaika

Amesema mbali na kugawa taulo za kike lakini shirika la Wadada limekuwa likitoa elimu kwa Watoto wakike kujua mabadiliko ya mwili likiwemo suala zima la balehe ili mtoto wakike ajue akiisha anza kuona hedhi wakati wowote anaweza kupata ujauzito hivyo lazima ajiepushe na wanaume hadi muda sahihi utakapofika.

“Hawa ndio ndio kina mama wajao ndio maana tunawafundisha pia umuhimu wa kupata ujauzito katika muda sahihi kwa sababu atakuwa amejiandaa hivyo atajifungua salama na kulea mtoto vizuri bila tatizo lolote”aliongeza Elihaika.

Kwa upande wake mwalimu wa malezi shule ya msingi Nyafula Joyce Sikwembe amelishukuru shirika la wadada solution kwa kuwapatia taulo za kike kwa kuwa zitawasaidia kuhudhuria masomo katika kipindi chote hata watakapokuwa katika siku zao.


Mwalimu wa malezi shule ya msingi Nyafula Joyce Sikwembe akilishukuru shirika la wadada Solution kwa msaada wa taulo za kike walizozitoa kwa wanafunzi wa shule ya msingi Nyafua na Sangabuye.

Ameyataka mashirika mengine kujitokeza na kuwapa msaada wa taulo za kike kwa sababu uhitaji bado ni mkubwa na kuongeza kuwa badhi ya Watoto wazazi wao hawana uwezo wa kuwanunulia taulo za hedhi kwa kila mwezi hivyo Watoto wengine kushindwa kwenda shule wakati wote wa hedhi na kupitwa na masomo.

“Watoto ambao hawana uwezo wa kununua taulo wanapata tabu maana wengine wanatumia vipande vya magodoro matokeo yake wanatoa harufu kali na kujikuta wanatengwa na wenzao na ndio maana wengine huamua kuacha kuja shule.”alisema Mwl Joyce.

Naye mtoto Salome Zakaria mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Sangabuye amelishukuru shirika hilo kwa kuwapatia taulo za kike kuwa zitawasaidia na kuacha kutumia vitambaa na karatasi kujistiri wanapokuwa katika siku zao na itawasaidia kusoma vizuri bila hofu.


Salome Zakaria mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Sangabuye akilishukuru shirika la Wadada Solution  kwa kuwapatia taulo za kike.

Kauli mbiu ya siku ya mtoto wa kike dunia mwaka huu inasema kizazi cha kidigitali  ni kizazi cha kwetu ikilenga wazazi na walezi kuangalia matumizi sahihi ya teknolojia kwa Watoto wa kike.

No comments