Breaking News

POMBE CHANZO CHA TATIZO LA AFYA YA AKILI KWA WATOTO.


Na Tonny Alphonce,Mwanza.

Wazazi wanao wanywesha pombe watoto wanapolia kwa muda mrefu kwa lengo la kuwafanya walale wametakiwa kuacha tabia hiyo kwasababu inachangia ongezeko la watoto wenye matatizo ya afya ya akili hapa nchini.

Wito huo umetolewa na Daktari bingwa na mbobezi wa watoto na vijana ,Dkt Gema Sembele wakati akizungumzia sababu za matatizo ya afya ya akili katika jamii na namna kujikinga na matatizo hayo.

Dkt Gema amesema mzazi anapompa pombe mtoto anamuweka kwenye hatari ya kupata matatizo ya afya ya akili kwa kuwa katika kipindi cha mwaka 0 – 5 hiki ni kipindi cha ukuaji wa ubongo wa mtoto hivyo kumnywesha pombe mtoto katika umri huo kunaweza kuathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto.

‘Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha tatizo la afya ya akili ikiwemo lishe duni wakati wa ujauzito wa mama,matumizi makubwa ya pombe wakati mama anapokuwa mjamzito lakini pia tabia ya kuwanywesha pombe Watoto wadogo ili waache kusumbua na kulala,hayo yote yanaweza kuwa sababu’alisema Dkt Gema.

Kwa upande wake afisa lishe wa jiji la Mwanza, Joyce Zelamala amesema lishe bora kwa mama mjamzito ni muhimu kwaajili ya maendeleo ya mtoto na humsaidia mtoto kukua vizuri kimwili na kiakili.

Amesema kama mama mjamzito hatopata lishe bora kuna uwezekano mkubwa kwa mama kupata madhara ya kiafya kama vile kutoongezeka uzito,kupungukiwa damu na hata kujifungua mtoto mfu na kwa upande wa mtoto lishe duni inaweza kusababisha ubongo kudumaa na mama kujifungua mtoto mwenye tatizo la afya ya akili.

‘Mama ili ajifungue mtoto ambae yupo timamu kimwili na kiakili lazima awe makini kipindi chote cha ujauzito wake,ale vizuri aache kunywa pombe,kuvuta sigara au bangi na hata miadarati kwa sababu kipindi cha ujauzito ni kipindi cha uumbaji kwa maana hiyo vitu vyote vya hatari mama mjamzito lazima aviache’alisema Bi Zelamala.


Mwanasaikolojia Bwana Bosco Bosco amesema tatizo la afya ya akili wakati mwingine husababishwa na sababu za kisaikolojia hasa kwa watu wazima tofauti na watoto ambao wao sababu huwa ni za kibailojia zaidi.

Mwanasaikolojia Bwana Bosco Bosco akizungumzia  namna pombe inavyoweza kusababisha tatizo tatizo la akili.

Bw Bosco amesema watu wazima wengi wamepatwa na tatizo la afya ya akili kutokana na unywaji wa pombe kupitiliza,uvutaji wa vitu vya kulevywa  kama Petroli,Mafuta ya taa,Gundi na matumizi ya dawa za kulevya kama heroin.

Amesema mtu akitumia vilevi hisia zake na mawazo yake yanavurugika na hivyo kupelekea matatizo makubwa ya kitabia na kwa mtazamo wa nje mtu huyu anaonekana hayupo sawa na amechanganyikiwa na kwa upande wa kiafya mtu huyu tayari anakuwa na tatizo la afya ya akili.

Kauli mbiu ya Siku Ya Afya Ya Akili Duniani mwaka huu inasema Afya ya akili katika Ulimwengu usio na usawa msisitizo ukiwa katika upatikanaji wa huduma ya matatizo ya afya ya akili kutoka kwenye miji mikubwa na kushuka chini hadi ngazi ya Zahanati ili kila mwananchi mwenye matatizo ya afya ya akili apate matibabu.

No comments