WATAALAMU WA AFYA:MTOTO ALIYEKO TUMBONI HAWEZI KUPATA UVIKO 19
Na Tonny Alphonce,Mwanza.
Kisayansi mtoto aliyepo tumboni kwa mama hawezi
kupatwa na ugonjwa wa UVIKO 19 kwa kuwa maambukizi ya ugonjwa huo yanaenea kwa
njia ya hewa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Utafiti Chuo Kikuu Bugando Mwanza Dkt Benson Kidenya wakati wa mkutano
wa maswali na majibu juu ya UVIKO 19 baina ya waandishi wa habari wa mkoa wa
Mwanza na Ofisi ya Mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza.
Dkt Kidenya amesema mtoto anaweza kuambukizwa ugonjwa wa UVIKO 19 mara baada ya kuzaliwa japo kuwa kisayansi watoto wachanga wamekuwa hawapatwi na ugonjwa UVIKO 19 japo wanaweza kuwa na virusi vya UVIKO 19.
Amesema kuhusu chanjo kwa kina mama wajawazito bado
serikali inaendelea kufanya utafiti
kujua ni wakati gani mzuri kwa mama mjamzito kupatiwa chanjo.
Dkt Kidenya amesema kwa kawaida mama mjamzito kinga
zake huwa zinashuka hivyo ni vema akapatiwa chanjo kwa katika kipindi hicho kwa
kuwa anaweza kushambuliwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa UVIKO 19.
”Utafiti wa awali ulipendekeza mama mjamzito ni vema
akachanjwa wakati mimba yake ikiwa imesogea kidogo kwa sababu katika kipindi
cha mwanzo cha ujauzito ndio mtoto anaumbwa sio vema mama kutumia dawa
nyingi,hivyo tunasubiri maelekezo ya serikali katika hili”alisema Dkt Kidenya.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Dkt Thomas
Rutachunzibwa amewataka kina mama wajawazito wasiwe na haraka ya kutaka
kupatiwa chanjo ya UVIKO 19 kwa kuwa serikali itatoa mwongozo juu ya wajawazito
na kina mama wanaonyoshesha kipindi gani wapatiwe chanjo hizo.
Dkt Rutachunzibwa amesema lengo la serikali ni zuri
kwa kuwa kipindi cha miezi mitatu ya ujauzito hiki ndio kipindi mtoto anaumbika
hivyo sio vizuri mama kupatiwa dawa nyingi kwa sababu mtoto anaweza kuzaliwa
akiwa na kasoro za kimaumbile.
“Watoto wengi wanaozaliwa na matatizo kama ya mgongo
wazi au kichwa kikubwa sababu huwa ni mama kutumia dawa nyingi wakati wa
ujauzito wake ndio maana miezi hii ya awali ya ujauzito hatutaki kumpatia mama
mjamzito dawa nyingi”alisema Dkt Rutchunzibwa.
Akizungumzia zoezi la chanjo ya UVIKO 19
linavyoendelea mkoani Mwanza Dkt amesema wananchi wanahamasika na hadi hivi
sasa watu zaidi ya elfu 28 wamepata chanjo na hakuna madhara yoyote
yanayotokana na chanjo yameripotiwa.
Dkt Rutachunzibwa amesema mwako mkubwa wa wananchi kuchanja kwa mkoa wa Mwanza ni kutoka
vijijini hasa katika wilaya za Kwimba,Misungwi na Magu na kuwataka waandishi
kuwahimiza wananchi wanaoishi mijini kwenda kuchanja.
No comments