Breaking News

WADAU WANAOTOA HUDUMA ZA WATOTO WATAKIWA KUWAKUMBUKA WATOTO WALIOKO PEMBEZONI

 

Na Tonny Alphonce,Dodoma.

Serikali imewataka wadau wanaotoa huduma za watoto nchini kuangalia pia namna ya kutoa huduma hizo kwa watoto waliopo pembezoni ili nao waweze kupata huduma muhimu kama ilivyo kwa watoto wanaopatikana katika miji mikubwa.

Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mh Mwanaidi Ally Khamisi akiongea na Wanahabari Vinara wa habari za Watoto.

Kauli hiyo imetolewa na yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mh Mwanaidi Ally Khamisi wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari za watoto 26 uliofanyika mkoani Dodoma ikiwa ni maandalizi ya kuanza kwa mradi mpya uliopewa jina la mtoto kwanza.

Amesema kukosekana kwa wadau wanatoa huduma za Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto katika maeneo ya vijijini inasababisha kukosekana kwa uwiano sawa na kusababisha makuzi yasiyo timilifu kwa watoto.

Naibu Waziri amewataka wadau wote wa Watoto kuwasiliana kabla ya kuanza kutoa huduma ili kujua ni maeneo gani yanye uhitaji mkubwa na nguvu zielekezwe huko ili kuhakikisha Watoto wote wa Tanzania wanapata huduma muhimu ya Malezi na Makuzi kwa usawa.

Akizungumzia baadhi ya hatua ambazo serikali imechukua katika kuboresha huduma za Malezi,Makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto Naibu Waziri amesema tayari serikali imeandaa miongozo na sera mbalimbali ikiwa ni pamoja na sera ya maendeleo ya mtoto ya mwaka 2008,kutunga sheria ya mtoto no 21 ya mwaka 2009,sheria ya elimu yam waka 1978 pamoja na serikali kuwashirikisha wadau kutekeleza mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na Watoto kwa kipindi cha mwaka 2017/2018 hadi 2021/2022.

Wanahabari Vinara wa Habari za Watoto wakifatilia hotuba ya Naibu Waziri Mh Mwanaidi hayupo pichani.

Akizungumzia kuwepo kwa wanahabari bingwa wa habari za watoto,Naibu Waziri Mh Mwanaidi amewataka wanahabari hao kuendelea kuihabarisha jamii kuhusu umuhimu wa Malezi na Makuzi kwa mtoto kwa kuwa bado wananchi wengi hawana ufahamu wa huduma za Malezi na Makuzi ya awali ya  mtoto.

Awali akitoa salamu za UTPC katika ufunguzi huo wa mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari za Watoto mkurugenzi wa UTPC,Abubakari Karsan amewapongeza vinara hao kwa kuandika Habari zaidi ya 1000 ndani ya miaka mitatu.

Mkurugenzi wa UTPC,Abubakari Karsan akitoa salamu za UTPC

Karsani amesema jambo hilo si dogo na linapaswa kupongezwa kwa kuwa tangu kuanza kuandikwa kwa habari za watoto kumesaidia kuleta matokeo chanya katika baadhi ya maeneo hapa nchini.

‘Mgeni rasimi nataka niseme tu yawezekana jambo hili likaonekana la kawaida lakini si la kawaida waandishi hawa wanastahili pongeze na wamefanyakazi kubwa sana katika kuandika habari hizi za watoto’,alisema Karsan.

Mkurugenzi Karsani amewataka pia wadau wengi ambao wanahitaji waandishi wenye uwezo mkubwa kama ilivyo kwa vinara hao wa ECD kuwasiliana na uongozi wa UTPC ili waweze kufanikiwa katika jambo ambalo wamekusudia kulifikisha katika jamii.


No comments