Breaking News

Umoja wa Kitaifa wa Wanawake Wavuvi (TAWFA) Ilemela na Nyamagana ,Watakiwa kuwatumia Wataalamu kutoka Halmashauri.

Na Tonny Alphonce,Mwanza.

Umoja wa Kitaifa wa Wanawake Wavuvi (TAWFA) wa wilaya za Ilemela na Nyamgana jijini Mwanza waliochaguliwa kuongoza umoja huo wametakiwa kuhakikisha wanatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake Wavuvi na wachakataji wa Dagaa kwa kuwatumia wataalamu waliopo katika halmashauri zao.

Wawakilishi wa TAWFA waliochaguliwa  kutoka Wilaya za Ilemela na Nyamagana wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa serikali pamoja na viongozi wa EMEDO.

Kauli hiyo imetolewa na afisa maendeleo ya jamii mkoa wa Mwanza Isack Ndasa wakati akifungua kikao cha kuwapata Wawakilishi wa TAWFA wa wilaya za Ilemela na Nyamagana.

Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mwanza Isack Ndasa akizungumza na vikundi vya kina mama wavuvi(hawapo kwenye picha) wakati akifungua kikao cha kuwapata Wawakilishi wa TAWFA wa wilaya za Ilemela na Nyamagana.

Bwana Ndasa amesema wanawake wavuvi na wachakataji wa Dagaa wanatakiwa wajiamini katika utendaji wao wa kazi kwa kuwa bila wao jamii inaweza isipate mazao ya Samaki yaliyo bora na hata halmashauri inaweza ikapoteza mapato kama wanawake wakiamua kuacha kufanya shughuli za kiuchumi.

Amesema hata takwimu za kundi linaloongoza katika ufanyajikazi za kiuchumi kwa Tanzania  bado ni kundi la wanawake linaloongoza kwa asilimia 75 hivyo amewataka wanawake wasiwe wanyonge mbele ya mteja na badala yake watafute  faida katika kazi hizo wanazofanya.

Baadhi ya wanavikundi vya wanawake wachakataji walioshiriki katika kikao cha kupata Wwakilishi kutoka wilaya za Ilemela na Nyamagana.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO), Eltrudith Lukanga amewataka viongozi hao wakahakikishe wanajenga taasisi imara ya wanawake katika ngazi hiyo ya wilaya kwa kuanza kushungulikia kero walizonazo wanawake wachakataji.

Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO), Eltrudith Lukanga akitoa neno kwa Wawakilishi waliochaguliwa.

Bi Lukanga amesema EMEDO kwa ushirikiano na Wizara ya Mifugo na Uvuvi wataendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wa TAWFA ili kuhakikisha mazingira  wezeshi yanapatikana kwaajili ya uvuvi endelevu utakaowasaidia wavuvi wadogo.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi huo Lucy Kilanga amesema viongozi hao wanne ambao wamechaguliwa watakuwa na jukumu la kutatua kero za wanawake wachakataji walioko katika ngazi hiyo ya wilaya.

Mratibu wa Mradi huo Lucy Kilanga kiongea na aVikundi vya Wanawake Wachakataji wa Dagaa na Samaki kabla ya zoezi la kuwapata wawakilishi wa Umoja huo.

Amesema baada ya viongozi hao ambao watawawakilisha kina mama kutoka vikundi 20 vilivyoko Ilemela na Nyamagana watakuwa na nafasi pia ya kushiriki vikao katika ngazi ya mkoa ambapo changamoto mbalimbali zitakazoibuka wilayani zitatafutiwa ufumbuzi.

Wawakilishi wa TAWFA waliochaguliwa kutoka Nyamagana ni Angelina Deogratius na Catherine Fransis na kwa upande wa Ilemela ni Maimuna Rajabu na Ela Livingstone.

No comments