Breaking News

SARATANI YA JICHO BADO NI HATARI KWA WATOTO, WAZAZI WATAKIWA KUWAFANYIA WATOTO UCHUNGUZI MAPEMA


Na Tonny Alphonce, Mwanza.

Imeelezwa kuwa Saratani ya JICHO ni moja ya Saratani inayoongoza kuwashambulia Watoto nchini ambapo kidunia kumekuwa na wagonjwa wapya takribani 9000 kila mwaka ikiwa ni sawa  na mgonjwa mmoja kwa kila watoto elfu 15 wanaozaliwa.


Kaimu Mkurugenzi na Utumishi Lilian Shao akiongea na Wazazi katika kilele cha Siku ya Jicho Duniani.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi na Utumishi Lilian Shao wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando katika hotuba yake wakati maadhimisho ya wiki ya Saratani ya Jicho ambapo amesema kuchelewa kufanyiwa uchunguzi mapema kwa Watoto wanaopata matatizo ya macho kunasababisha asilimia 50 ya watoto kushambuliwa na Saratani ya Jicho na hata kupoteza Maisha.

Amesema kwa hospital ya Bugando Takwimu za mwaka 2021 zinaonyesha Watoto 46 walitibiwa,Watoto 8 sawa na asilimia 18 hawakuendelea na matibabu kutokana na sababu mbalimbali,Watoto 13 sawa na asilimia 28 walipoteza Maisha na Watoto 25 ambao ni sawa na asilimia 54 walipatiwa matibabu na kupona.


Akizungumzia upande wa vifaa na wataalamu wa kupambana na Saratani ya Jicho ,Mkurugenzi amesema hospital ya Bugando ina wataalamu wa kutosha na vifaa tiba vya kutosha vya kupambana na ugonjwa huo wa Saratani ya Jicho kwa Watoto.

"Hivi karibuni tutafungua kliniki yetu mpya ya kisasa yenye vifaa vya kisasa ambapo wagonjwa wetu watahudumiwa katika mazingira mazuri zaidi,na niwakumbushe wazazi ukiona mboni nyeupe au kengeza kwenye jicho la mtoto hiyo ni dalili ya saratani ya jicho mlete mtoto afanyiwe uchunguzi mapema ili atibiwe na tuweze kupunguza vifo vya Watoto vinavyotokana na saratani".alisema Shao

Kwa upande wake Daktari Mbobezi wa Magonjwa ya Saratani Heroniam Joas amesema ugonjwa wa Saratani ya jicho kwa Watoto ni tatizo kubwa ambapo takwimu kwa mwaka jana zinaonyesha kwa ujumla Watoto waliopata kansa ni 250.

Daktari mbobezi wa magonjwa ya Saratani Heroniam Joas akizungumzia ukubwa wa tatizo la Saratani ya Jicho kwa watoto wadogo.

Dkt Joas amesema Saratani za Watoto mara nyingi hazina sababu kama ilivyo kwa Saratani za watu wakubwa ambao hupata saratani kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo unywaji wa pombe,uvutaji wa Sigara au ulaji wa vyakula vinavyoweza kusasababisha saratani.

"Japo hakuna Ushahidi wa kutosha lakini inaonyesha kuwa sababu zinazoweza kusababisha Saratani ya Jicho mtoto anaweza kuzipata kutoka kwa wazazi wake,vinasaba vya mzazi vinapobadilika na kupita na kwenda kwa mtoto kunaweza kusababisha mtoto kupata saratani,mtoto akipigwa na mionzi na umri wa wazazi ukienda sana kwa wazazi inaweza ikawa sababu ya mtoto kupata hiyo saratani ya Jicho."Alisema Dkt Heroniam.


Naye Daktari Everista Mgaya ambae ni daktari bingwa macho kwa watoto amesema mara nyingi dalili za Saratani ya Jicho huwa hazionyeshi moja kwa moja na mzazi au daktari anaweza asijue hivyo uchunguzi wa mara kwa mara unahitajika kwa ukaribu wa wazazi na madaktari.


Dkt Everista Mgaya ambae ni Daktari Bingwa wa Saratani ya Macho kwa Watoto. 

"Matibabu ya Saratani ya Jicho ni magumu yanahitaji ushirikiano mkubwa kati ya madaktari na wazazi maana kuna wakati baada ya uchunguzi wakati mwingine hutulazimu kutoa jicho la mtoto nah apo ndio mvutano hutokea,mzazi anaweza akagoma jicho la mtoto wake lisitolewe wakati tunatakiwa kuokoa uhai wa mtoto lakini angalau jicho moja litoke na mtoto aendelee na Maisha".Alisema Dr Mgaya.


Mkurugenzi wa idara ya macho katika hospitali ya Bugando Daktari Christopher Mwananjao akizungumzia namna ya kupata matibabu ya Saratani kwa Mtoto.

Daktari Christopher Mwananjao ambae ni Mkurugenzi wa idara ya macho katika hospitali ya Bugando amewapongeza wazazi ambao wanaendelea kuwa wavumilivu na kufatilia matibabu ya Watoto wao ambapo wengine wamepona na wamerudi shule na kuwataka wazazi hao kuwa mabalozi kwa kutoa elimu kwa wazazi wengine kuwapeleka Watoto Bugando kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi.


Diana John ambae ana mtoto mwenye Saratani akizungumzia changamoto za malezi ya mtoto mwenye Saratani.

Diana John ambae ana mtoto mwenye Saratani amesema changamoto kubwa ya matibabu ya Saratani ya Jicho anayopata ni muda wa matibabu ambao unachukua muda wa miezi sita hadi saba na wakati mwingine mzazi huitajika kununua miwani ambayo ni gharama kubwa hali ambayo husababisha wazazi wengi kuingia kwenye madeni makubwa.

"Tulianza wengi hapa wazazi ambao walifika kwaajili ya matibabu,wengi walikimbia tulipoanza tu matibabu na wengine wamepoteza Watoto wao baada ya kukatiza matibabu yaani wamekuja kurudi kwenye matibabu hali yam toto tayari mbaya".Alisema Diana.

Naye Nariba Luwecha mkazi wa Geita amewaomba wasamalia wema wamsaidie ili aweze kuendelea na matibabu ya kansa ya jicho kwa mtoto wake ambapo kwa sasa hawezi kupata nauli ya kuhudhuria Kliniki kila anapopangiwa kutokana na ugumu wa Maisha alionao.


Nariba Luwecha mkazi wa Geita Mzazi mwenye mtoto mwenye Saratani.

Hospitali ya Rufaa ya Bugando ambayo inashirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma inatekeleza sera ya Afya 2007 ambayo imelenga kuboresha uhai wa mtoto kupitia utoaji huduma bure za afya kwa kina mama wajawazito na Watoto chini ya miaka mitano kama Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali Awali ya Mtoto inavyoelekeza.


Mpango Mkakati wa Taifa wa Kuboresha Afya ya Uzazi,Mzazi,Mtoto na Vijana nchini Tanzania  (2016 – 2020) umewekeza mazingira wezeshi ya kupunguza magonjwa,vifo vya kina mama ,Watoto wachanga,Watoto na vijana kwa kutoa huduma bora endelevu na jumuishi zinazowafikia watu wote katika ngazi mbalimbali za utoaji huduma katika vituo vya afya na kwenye jamii.

No comments